Rais wa Sudan Kusini amewafuta kazi Makamu wake wawili na Mkuu wa kitengo cha usalama wa taifa,yakiwa ni mabadiliko ya hivi punde kwenye serikali ya Umoja wa kitaifa.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Waliokuwa makamu wa rais James Wani Igga, ambaye ni mwanasiasa mkongwe na Hussein Abdelbagi Akol, wameondolewa kwenye nafasi hizo, kupitia amri ya kiongozi huyo wa Sudan Kusini.
Hakuna sababu yoyote iliyotolewa kuelezea maamuzi hayo ya rais Kiir ambaye pia amemfuta kazi, Akech Tong, mkuu wa kitengo cha usalama wa taifa aliyemteua mwezu Oktoba mwaka uliopita.

Katika hatua nyingine, rais Kiir amemteua mshirika wake wa karibu Benjamin Bol Mel, kuwa Makamu wake anayeshughulikia masuala ya uchumi.
Mabadiliko haya yamekuja wakati huu kukiwa na mino’ngo’no kuwa rais Kiir mwenye umri wa miaka 73 huenda anajiandaa kuondoka madarakani na anamwandaa Bol Mel kama mrithi wake, iwapo atalazimika kuachia uongozi wa nchi hiyo kwa sababu za kiafya.
Rais Kiir anaongoza serikali ya Umoja wa kitaifa na mpinzani wake mkuu Riek Machar ambaye ni Makamu wa kwanza wa rais kwa mujibu wa mkataba wa amani wa mwaka 2018