‘Stress’ za mjamzito zinavyomuathiri mtoto anayezaliwa

Dar es Salaam. Wapo wajawazito katika mazingira tofauti na sababu zilizo nje ya uwezo wao wanapitia msongo wa mawazo ‘stress’, jambo linaloelezwa si hatari tu kwake, bali pia hata kwa mtoto atakayezaliwa na katika makuzi yake.

Msongo wa mawazo husababishwa na mambo mbalimbali, ikiwemo kutengana na mume wake katika kipindi hicho,  kugombana, kupigwa na masimango. Pia wapo waliobeba ujauzito bila kutarajia au kukataliwa na wenza wao na hawana vipato.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Dk Issack Mhando anasema mjamzito hapaswi kuwa na msongo wa mawazo kwa kuwa ujauzito wenyewe ni msongo wa mawazo tosha.

“Kipindi cha ujauzito mama anapitia mabadiliko mengi, ikiwemo katika mfumo wake wa damu, upumuaji na wakati mwingine hata ngozi, hivyo anapoongezewa mawazo mengine ni kwenda kumsababishia matatizo yeye pamoja na mtoto atakayezaliwa,” anasema.

Dk Mhando anasema msongo humfanya mama kushindwa kula vizuri, chakula ambacho ni muhimu kwa mtoto tangu akiwa na umri sifuri tumboni, hivyo baadaye anaweza kuzaliwa kiumbe mwenye upungufu, ikiwemo utapiamlo, ulemavu na mambo mengine.

Hivyo, anashauri wanaomzunguka mjamzito wasaidie kuondoa au kutokuwa chanzo cha msongo wa mawazo kwa mama na kumwonyesha upendo, kumjali katika kipindi chote cha ujauzito.

Kwa upande wake, daktari wa watoto, Davidson Emmanuel anasema mtoto aliyezaliwa na mama wa aina hiyo anaweza kuchelewa kupona kitovu, kutoongezeka uzito na kushauri wakati wa kuwatibu watoto wanaopitia hayo ni vema mtaalamu akapata historia kwa kina ya mama tangu alivyopata ujauzito hadi kujifungua.

Anafafanua kuna wengine hushindwa kuhimili  hali hiyo, hivyo huingia kwenye utumiaji wa sigara, pombe au dawa za kulevya kwa lengo la kujifariji bila kujua wanasababisha athari kwa mtoto aliye tumboni.

“Pia mama kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya au ulevi uliopindukia, tusitarajie atakumbuka kumpeleka mtoto kwenye chanjo anazopaswa azipate katika miaka mitano yake na hapo ndipo mtoto ataanza kuandamwa na magonjwa nyemelezi,” anasema Dk Emmanuel.

Athari kwa mtoto

Anita Mganga, mkunga mtaalamu anayejishughulisha na masuala ya wajawazito, unyonyeshaji pamoja na malezi na makuzi ya awali ya mtoto, anasema watoto wanaozaliwa na mama aliyekuwa na msongo wa mawazo wanaweza kupata baadhi ya tabia na changamoto mbalimbali.

Anasema mtoto anaweza kuonyesha tabia kama vile ugomvi, ujeuri, hasira za ghafla au kupoteza uwezo wa kujidhibiti na hiyo inaweza kuanza utotoni na kuendelea kadri anavyokua.

Pia anasema msongo wa mawazo wa mama unaweza kusababisha watoto kuwa na viwango vya juu vya wasiwasi, woga au mashaka.

“Mtoto wa aina hii anakuwa na hali ya kutotulia au woga wa kushughulika na changamoto za maisha, na hii kama hatapata tiba mapema inaweza kwenda hadi anapokuwa mtu mzima,” anasema Anita.

Matatizo ya usingizi

Mkunga huyo anasema mtoto anayezaliwa katika hali hiyo anaweza kukosa usingizi mzuri au kuwa na usingizi wa mara kwa mara usio tulivu, hali inayoweza kuathiri ukuaji wake wa kiakili na kimwili.

“Mtoto anaweza kupata changamoto za kiakili. Msongo wa mawazo wa mama unaweza kuathiri uwezo wa mtoto kujifunza au kumudu masomo shuleni na anaweza kuwa na matatizo ya kumbukumbu, umakini au uwezo wa kushughulikia taarifa mpya,” anasema Mganga.

Anataja kuhisi hali ya huzuni au sonona, akisema baadhi wanaweza kuwa na hali hiyo katika umri mdogo kutokana na athari za homoni za msongo walizoathiriwa nazo wakati wa ujauzito.

“Pamoja na hayo, watoto wanaweza kuwa na matatizo ya kuwasiliana au kushirikiana vizuri na wenzao. Wanakuwa na hali ya kutokujiamini, kuepuka mawasiliano au hata kushindwa kuunda uhusiano mzuri na watu wa karibu,” anasema.

Pia anasema mtoto anaweza kuwa na viwango vya juu vya matatizo kama vile pumu, mzio au matatizo ya mfumo wa kinga kutokana na kuathirika kwa mifumo ya mwili wakati wa ukuaji wa fetasi (mlalo wa mtoto tumboni mwa mama).

Mwanasaikolojia, Sylvia Sostenes anasema uumbaji wa mtoto unaanza pale mimba inapotungwa, hivyo makuzi yake yanaanza akiwa ndani ya tumbo la mama yake.

“Makuzi yake haya yanategemea pia mchanganyiko wa mambo,  ikiwemo afya ya akili ya mama inayobeba hisia, tabia na akili ndani yake.

“Kutokana na mchanganyiko huo, watoto wanaozaliwa na mama waliopitia msongo wa mawazo, wapo wanaoathirika na tabia za mama zao na wapo wanaothirika na hisia za mama zao,” anasema Sylvia.

Hata hivyo, mwanasaikolojia huyo anasema wengi wa watoto wanaopata matatizo ni wale walioathirika na hisia za mama zao.

Mtoto wa aina hiyo anasema huwa ni mzubaifu, hajiamini, hana raha ama ana tabia za kuogopa.

Aidha, kwa mtu wa kawaida anasema hawezi kugundua tatizo hilo haraka kama hana utaalamu.

Ili kusaidia haya yasitokee, mganga huyo anasema kuna haja ya kumsaidia mama kupunguza msongo wa mawazo kipindi chake chote cha ujauzito,, kwani hiyo itasaidia kupunguza athari zisije kutokea kwa mtoto katika makuzi yake.

Sylivia anasema cha kwanza ni muhimu kumtambua mtoto mwenye tatizo hilo, kisha kumpeleka kwa wasaikolojia tiba ili watambue tatizo lake na  kumsaidia.