Straika Stellenbosch aingiwa ubaridi, adai Simba ni hatari

Kwa mara nyingine macho na masikio ya wapenda soka yataelekezwa Zanzibar, Jumapili hii, pale Simba  itakapoumana na Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya  Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

Katika kuelekea mchezo huo mshambuliaji wa Stellenbosch, Andre Ernest de Jong, raia wa New Zealand, amesema kikosi chao kimejiandaa kimwili na kiakili kuhakikisha kinapata matokeo chanya katika ardhi ya ugenini ili kuweka mazingira mazuri ya kutinga fainali kwenye mechi ya marudiano nyumbani, Afrika Kusini.

“Tuna furaha kubwa sana kucheza dhidi ya Simba,” amesema De Jong. 

“Tunatambua ni klabu kubwa barani Afrika na tumejifunza mengi katika hatua zilizopita, hasa tulipoikabili Zamalek.  Tumethibitisha kwamba tunaweza kupambana na vigogo wa bara hili, na malengo yetu ni kupata matokeo mazuri hapa Zanzibar kabla ya kurudiana nyumbani.”

HAKUNA UNAFUU NEW AMAAN

Wakati wengi wakidhani kucheza nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa ni nafuu kwa wapinzani wa Simba, De Jong anaamini hakuna tofauti kwani wachezaji wa Simba wamezoea mazingira ya Tanzania kwa ujumla. 

Hata hivyo, amesema kucheza Zanzibar ni fursa pia kwa Stellenbosch kujipima dhidi ya presha ya mashabiki wa Simba.

“Tunaelewa kuwa Simba ni timu imara sana, hasa wanapocheza nyumbani. Tunajua wanashinda mechi nyingi mbele ya mashabiki wao. Hii haitakuwa kazi rahisi,” amesema.

” Lakini hata sisi tumeshazoea kucheza ugenini na nyumbani, kwa hiyo hatuoni kama ni faida kubwa kwa upande wetu. Tunajiandaa kwa dakika 180 za vita kali.”

HALI YA HEWA NA MZUKA WA MECHI

Akizungumzia hali ya hewa ya Zanzibar, De Jong amesema: “Ni joto, lakini tumeshazoea mazingira ya namna hii. Tuna wachezaji waliokaa kwenye hali ngumu zaidi. Hii haitakuwa sababu ya kushindwa.”

Stellenbosch wamewasili mapema Zanzibar na kufanya mazoezi katika uwanja mdogo wa Amaan ili  kuzoea  mazingira, huku wakionekana kuwa na morali kubwa na ari ya ushindi.

HATARI YA SIMBA

Wakati Simba ikijivunia safu ya ushambuliaji inayoongozwa na nyota kama Leonel Ateba, Elie Mapanzu, Kibu Denis na Charles Ahoua, De Jong hakusita kuonyesha heshima kwa wapinzani wao, akisema: “Simba wana washambuliaji hatari sana, ni wenye nguvu na kasi. Lakini si hao tu, timu nzima ni imara kuanzia nyuma hadi mbele.

“Kwa hiyo tunajiandaa kupambana kisawasawa. Tutahitaji kuwa imara kimwili na kisaikolojia ili kuwazuia.”

SIMBA KUPAMBANA NA HISTORIA 

Simba chini ya kocha Fadlu Davids wamekuwa na msimu mzuri kwenye michuano ya CAF, wakivuka hatua ya robo fainali dhidi ya Al Masry, huku wakiwa na ari ya kutinga fainali ya kwanza ya kimataifa tangu 1993.

Wekundu wa Msimbazi wanatarajiwa kutumia kila mbinu kufanikisha ndoto hiyo.

Tayari Uwanja wa New Amaan umetangazwa kuwa tayari kwa ajili ya mchezo huo mkubwa, huku mashabiki wa soka wakitarajiwa kufurika kwa wingi.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Simba msimu huu kucheza mchezo wa kimataifa wa CAF katika ardhi ya Zanzibar, jambo linaloongeza mvuto wa kihistoria katika pambano hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *