
Dar es Salaam, Mara nyingi kwenye kiwanda cha burudani jina la msanii linaweza kuwa silaha yenye nguvu ya kumfanya aweze kufahamika kwa kiasi kikubwa na kujizolea mashabiki.
Wakati mwingine majina hayo hutengenezwa kwa ushindani miongoni mwa wasanii wenyewe, huku wengi wakichagua kutumia majina ya ‘aka’ ili kuunda taswira maalumu kwa mashabiki katika utambulisho wao.
Majina ya umaarufu kwa baadhi ya mastaa hutokana na mambo mbalimbali kama vile mambo wanayopenda kufanya, wanyama, kupewa na watu na hata kwa kuigiza uhusika wa watu wengine kama ilivyo kwa Steve Mengele ‘Steve Nyerere’ ambaye amepata umaarufu kutokana na kuigiza sauti ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Kutokana na matumizi ya majina hayo ya umaarufu wakati mwingine huingia kwenye vichwa wa mashabiki na kuwafanya wasahau kabisa majina asili ya mastaa wao.
Na hii inajionesha kwa Steve Nyerere ambaye hivi karibuni msemaji wa familia ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye ni mtoto wake wa sita Madaraka Nyerere wakati akifanyiwa mahojiano na Televisheni ya Taifa (TBC), alitoa ushauri kwa wasanii hao akiwemo Steve kuenzi majina ya wazazi wao kwanza kabla ya kujiita ya viongozi.
“Jambo la kumuenzi mtu ni jambo zuri lakini imetokea kwa baadhi ya wasanii baada ya kuwa fulani bin fulani anayemuenzi mwalimu Nyerere, ameanza kuwa fulani bin Nyerere hiyo naona ni tatizo kuna ndugu yetu anaitwa Steve Nyerere nimegundua leo kuna hata waandishi wa habari hawajui kama anaitwa Steve Mangele.
“Kabla ya kuenzi viongozi tuanze kuenzi wazazi wetu, nafikiri hii lawama nairusha kwa waandishi wa habari nawaomba rudini kwenye weledi wenu, namuomba yeye mwenyewe huyo msanii aanze kutumia jina lake lakini sidhani kama ataweza kwa sababu amekuwa mashuhuri sana,”alisema.
Hata hivyo, kwa wakati mwingine tofauti Madaraka alisema anashangazwa na msanii huyo kumpa mwanaye jina la Alex Nyerere
“Nimeambiwa leo kuna mtoto wake anaitwa Alex Nyerere, ni jambo ambalo haliwezekani, si kwa kumzuia mtu kwenda mahali akafanya kazi yake ya usanii akajiita Steve Nyerere bali ni kwa kumshangaa kuacha jina lake Mengele na kujiita Steve Nyerere hilo tu na kaongezeka Alex Nyerere. Baada ya miaka miwili huwa tuna kikao cha ukoo sasa sijui watakuja?”, alisema Madaraka.
Hivyo kutokana na Steve kutajwa kama mfano wa wasanii wanaotumia majina ya viongozi na kushauriwa kuenzi ya wazazi wake mwigizaji huyo ameiambia Mwananchi yeye atabaki kuwa Steve Nyerere.
“Jina nimetumia miaka 30 haya ndiyo yanajitokeza leo, lakini kibaya zaidi nimeshiriki kazi nyingi mpaka viongozi wa nchi hii wananiita Nyerere sijawahi kuwa mwizi, jambazi, sijawahi kuuza mirungi, kusafirisha maharamia, kuuza madawa ya kulevya. Ungesema hili jina lisitumike kwa hoja hizo, sawa,”alisema.
Alisema kwenye vitambulisho vyake anatumia jina la Steve Mengele lakini Watanzania ndiyo wameamua kumuita jina hilo hivyo atabaki kuwa Steve Nyerere
“Vijana wasirudi nyuma wasiogope kauli wasiwe waoga kwa sababu maisha hayahitaji uoga ilimradi hauvunji katiba ya nchi hii, hutukani mtu fanya kile kinachostahili kwa maendeleo ya Taifa letu. Wasiogope, wasione kama mimi imenitokea na wao itawatokea mimi ni mkubwa mno wajifunze kuwa wavumilivu,” alisema
Hata hivyo, akizungumzia faida na hasara za wasanii kutumia majina ambayo siyo halisi (AKA) Mbobezi katika Sanaa za maonyesho na mhadhiri wa UDSM, Dk Delphine Njewele amesema ni vyema msanii kutumia jina lisilo halisi ili kutofautisha maisha yake binafsi na kazi anayofanya.
“Mara zote msanii inabidi aji-brand anatakiwa kutafuta namna ya kufanya hivyo ikiwa ni pamoja na kutafuta jina ambalo litamuuza mfano msanii tunayemuita Konde Boy angetumia jina lake la kwanza lakini Rajab watu wenye jina hilo wapo wengi sana.
“Ili ajiweke pekee kajiita Konde Boy moja kwa moja watu wanaotoka kanda hiyo amewapata lakini hasara yake kuna mwingine hataki ukabila anaweza akakosa hadhira nyingine isiyopenda ukabila kwa sababu katumia Konde Boy lakini faida ni nyingi zaidi kuliko hasara,”alisema
Alisema maisha ya jukwaani siyo maisha halisi ya wasanii kwa hiyo ni muhimu sana wasanii kuwa na majina hayo ya kutunga ili kuweka mstari kati ya maisha yao halisi na yale ya usanii lakini pia kuwa wabunifu kwenye majina waliyochagua na ujumbe wanaopeleka.