Stendi ya Mafiga inavyoyapasua vichwa daladala, mabasi Morogoro

Licha ya manispaa ya Morogoro kuyaondoa mabasi ya wilayani kwenye kituo cha mabasi Msamvu na kuyapeleka kwenye kituo cha Mafiga, bado madereva wa daladala wameendelea na msimamo wao wa kutopeleka daladala zao katika kituo hicho, ambacho awali kilijengwa kwa ajili ya daladala zinazofanya safari ndani ya manispaa hiyo.

Mbali ya kupeleka mabasi ya wilayani, pia Manispaa hiyo imepeleka baadhi ya taasisi za umma, ikiwemo ofisi ya ardhi pamoja na ofisi ya Nida, huku viongozi wa Manispaa hiyo, wakiwemo madiwani wakiamini kuwa inaweza kuwa sababu ya kuwepo kwa daladala zitakazopeleka abiria kupata huduma hizo.

Hata hivyo, baadhi ya madereva wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro kutokea kituo hicho cha Mafiga wamelalamikia kuwepo kwa vituo visivyo rasmi (stendi bubu) katika maeneo mbalimbali ya mji huo, hali inayowafanya madereva wachache waliokubali kubaki Mafiga kukosa abiria.

Jeremiah Francis, mmoja wa madereva wa mabasi yanayokwenda wilayani amesema vituo hivyo visivyo rasmi vimekuwa zikipakia abiria wengi, huku wao waliotii amri ya kwenda Mafiga wakikosa abiria na kutumia muda mrefu kujaza abiria kwenye mabasi hayo.

“Mwanzoni kituo hiki cha Mafiga kilijengwa kwa ajili ya daladala, lakini baada ya daladala kugoma kuingia hapa sisi madereva wa mabasi ya wilayani tukaamrishwa na Serikali tuje hapa ili kuvutia abiria na kupafanya pachangamke, lakini bado daladala hazitaki kuja, matokeo yake na sisi baadhi ya madereva wenzetu, hasa wa mabasi ya Turiani, Gairo na Kilosa wameamua kwenda kuanzisha vituo bubu jirani na maeneo ya Msamvu,” alisema Francis.

Aliongeza: “Mfano mtu katoka mkoani kashuka Msamvu anataka kwenda Kilosa, Gairo au Turiani na hakuna daladala za kuja Mafiga, hawezi kupoteza tena shilingi elfu mbili kupanda bodaboda aje huku Mafiga, atakachofanya atapanda daladala Sh500 atakwenda kwenye kituo bubu cha Kwa Mkomola au Kwa Chambo, atapanda coaster atakwenda zake, sisi tuliokubali kubaki huku Mafiga tunakosa abiria.

“Tunachoomba hao viongozi wenye mamlaka warekebishe hili suala, mabasi yanayotakiwa kuja huku Mafiga yaje, ili tubadilishane abiria, daladala zituletee abiria na sisi mabasi ya wilaya tuwape wenzetu wa daladala abiria kutoka wilayani, hii itasaidia hata kituo kuwa na mzunguko wa biashara, lakini kwa sasa tunapitia wakati mgumu wa kazi,” alisema Francis.

Katibu msaidizi wa umoja wa madereva na makondakta wa mabasi yanayokwenda Kilosa, Maurus Dihindila, anasema licha ya wao kufuata utaratibu, kuwepo kwa mabasi yanayopakia abiria kiholela barabarani ni jambo linalowafanya na wao waliopo Mafiga wakose abiria.

Dihindila alisema ujenzi wa kituo hicho umegharimu fedha nyingi, lakini kwa muda mrefu utendaji kazi wake umekuwa wa kusuasua, hivyo amewashauri viongozi wa Manispaa, hasa Mkurugenzi na madiwani kuchukua hatua kali dhidi ya daladala zinazogoma kwenda Mafiga, lakini pia mabasi ya wilayani yanayopakia abiria kwenye maeneo yasiyokuwa rasmi.

“Cha kusikitisha kwa sasa daladala hasa za Kihonda, Mkundi, Mazimbu, Lukobe hazina kituo maalumu, zinaingia mjini kati na kupakia abiria kwenye maegesho yaliyopo kando ya barabara, madereva hawana njia maalumu ya kupita wakiingia mjini au kutoka mahala popote, wakiona abiria wanapakia na akitaka kushusha anashusha, hali hii ni upotevu wa mapato, maana hizi daladala hakuna mahali maalumu ambapo Manispaa inaweza kuchukua mapato,” alisema Dihindila.

Dihindila alisema mpango wa Manispaa ulilenga kuhakikisha kituo cha Mafiga kinatumika kikamilifu kama sehemu rasmi ya daladala, ili kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia ushuru wa getini, hata hivyo, kutokana na mgomo wa daladala na uwepo wa vituo visivyo rasmi, fedha za mapato zilizotarajiwa kukusanywa haziwezi kupatikana kwa sababu zipo fedha zinapotea.

Kwa upande wao, wamiliki wa mabasi yanayokwenda wilayani wanaeleza namna wanavyopata hasara kutokana na kuwepo kwa vituo bubu ambavyo havina mchango wowote kwenye mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Wanachosema watumiaji

Mmoja wa wamiliki wa mabasi hayo, Mubarak Al Saedy aliiomba Manispaa ya Morogoro na viongozi wa mkoa kurudisha mabasi ya wilayani kwenye kituo cha mabasi cha Msamvu ili kuondoa vituo bubu vya mitaani na barabarani.

“Hawa madereva wanaopakia kwenye vituo bubu ni kwa sababu tu Mafiga hakuna abiria, sasa na sisi wengine tukiamua kutoa mabasi hapa Mafiga na kutafuta kituo vyetu bubu si itakuwa vurugu, haiwezekani wenzetu wapakie huko sisi tushinde kutwa nzima bila kupata abiria, Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kwenye hili,” alisema Al Saedy.

Musa Ramadhani, ambaye ni dereva wa daladala inayofanya safari kati ya Kihonda na Mjini anasema kituo cha Mafiga kimejengwa kwa ubora, lakini sababu inayowafanya washindwe kupeleka daladala ni umbali wa kutoka katikati ya mji hadi kwenye kituo hicho, lakini pia kutokuwepo kwa abiria wanaokwenda katika kituo hicho.

“Kujenga kituo kule Mafiga Manispaa imeharibu hela tu, huwezi kujenga kituo kwenye maeneo ambayo hayana shughuli za kijamii au za kuvutia watu, eneo walilochagua kuweka kituo siyo rafiki kwa abiria, ofisi zote muhimu za Serikali zipo katikati ya mji, halafu wao Manispaa wanakwenda kujenga kituo kule pembezoni mwa mji, nani atakwenda,” alihoji.

Amesema kama Serikali inataka kupata mapato wawarudishe kwenye kituo cha zamani cha mjini kati vinginevyo wataendelea kuzunguka mjini na kupakia abiria kule hakuna atakayekwenda.

Halmashauri

Meya wa Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga, amesema jitihada za kukifanya kituo hicho kuwa na mzunguko wa kibiashara na kuweza kuingizia mapato Manispaa haziwezi kufikiwa iwapo vituo visivyo rasmi vitaendelea kuwepo ndani ya mji huo, huku akisisitiza kuwa hali hiyo inaathiri pia mipango yao ya kuwa Jiji.

“Hatuwezi kuwa na mabasi yanapaki kila mahala, baraza (la madiwani) tumeshatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro pamoja na kwa Mkuu wa Wilaya kwamba hatuhitaji kuona mabasi yanapaki hovyo, tunataka ile stendi ya Mafiga iwe inafanya kazi,” anasema Kihanga.

Kuhusu kupotea kwa mapato, Kihanga amekiri kwa kusema sababu ni daladala kutotoa ushuru wa getini, hasa baada ya kugomea kupeleka daladala kwenye kituo cha Mafiga, hata hivyo anasema Manispaa hiyo imejipanga kuja na sheria zitakazolazimisha daladala kwenda kwenye kituo hicho.

“Mapato yanapotea, fedha zinapotea, maana mradi wowote unaojengwa lazima uwe na faida, tulipoona watu wa daladala wamegoma kuja Mafiga tukaona ni vema tupeleke mabasi ya wilayani tukiamini daladala zitakwenda, lakini bado hawa watu wa daladala wanaendelea kuegesha hovyo hovyo mjini na kupakia abiria,” amesema Kiahanga.

Meya huyo alitoa ombi kwa mamlaka nyingine kusaidia kuzuia jambo hilo, akitolea mfano jeshi la polisi ambalo muda mwingi linakuwa barabarani.

Ofisa mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Andrew Mlacha, anasema jukumu la taasisi hiyo ni kutoa vibali vya njia na kuhakikisha kila daladala inakwenda kwenye njia iliyoombwa kwenye vibali.

“Suala la wapi kijengwe kituo na kusimamia daladala zinaingia kituoni ni jukumu la Halmashauri ya Manispaa pamoja na jeshi la polisi, sisi tukiona dereva wa Kihonda anapita njia ya Mazimbu au Kichangani au mtu anapeleka daladala mahali bila ya leseni hapo ndiyo tunachukua sheria,” anasema Mlacha.