Dar es Salaam. Baada ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeendeleza historia yake ya kufuzu mashindano haya kwa namna moja ambapo katika awamu zote imekuwa ikisubili hadi mechi za mwisho ili kufuzu.
Afcon ya mwaka 1980 iliyofanyika Nigeria, Stars ilifuzu baada ya kupata sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Zambia ambapo mchezo wa kwanza Stars ilishinda bao 1-0.
Mwaka 2018 Stars ilipangwa kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho ambapo Stars ilisubili mpaka mechi ya mwisho ili kujihakikishia kufuzu Afcon ilipoifunga Uganda mabao 3-0 kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambapo fainali hizo zilifanyika Misri mwaka 2019.
Mwaka 2021 Stars ilipangwa kundi F pamoja na Algeria, Uganda na Niger ambapo ilifanikiwa kufuzu mashindano ya Afcon baada ya kupata sare ugenini kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Algeria ambapo fainali hizo zilifanyika Ivory Coast mwaka 2022.
Mwaka huu 2024 umeonekana kujirudia kwa mtindo uleule wa kufuzu kwenda Afcon ambapo Stars imelazimika kusubili mechi ya mwisho ili kufuzu mashindano haya ambapo mwaka huu ilipangwa kundi H pamoja na DR Congo, Guinea, na Ethiopia.

Kwenye hatua hii ya makundi Stars imefuzu kwenda Afcon baada ya kuifunga Guinea bao 1-0 kwenye mechi ya mwisho iliyopigwa uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Baada ya kuifunga Guinea, Stars imeweka rekodi ya kushinda mechi mbili dhidi ya timu moja kwenye hatua ya makundi ambapo imeifunga Guinea nyumbani na ugenini lakini ni mara ya kwanza Stars inakubali vipigo viwili dhidi ya timu moja ambapo ilifungwa na DR Congo nyumbani na ugenini.
Pia kwa mara ya kwanza Stars imefanikiwa kufuzu mashindano ya Afcon ikifikisha jumla ya pointi 10 kwenye kundi H ikiwa haijawahi kufikisha idadi hiyo ya pointi za kufuzu Afcon. Stars inafuzu Afcon mara ya pili mfululizo ikiwa haijawahi kufanya hivyo kabla.
Kocha Hemed Morocco amekuwa Mtanzania wa kwanza kuiongoza Stars kufuzu kwenye michuano ya Afcon. Tofauti na michezo mingine ya kufuzu Afcon, mchezo dhidi ya Guinea ulikuwa na mashabiki wengi waliyojitokeza uwanjani kuliko michezo mingine ya Stars.

Stars imemaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi H ikikusanya alama 10 nyuma ya vinara DR Congo iliyomaliza nafasi ya kwanza ikikusanya alama 12 wakati Guinea ikimaliza nafasi ya tatu ikiwa na alama tisa huku Ethiopia ikiwa ya mwisho na alama nne.