Stam azitamani pointi za Yanga

KOCHA Msaidizi wa Fountain Gate, Amri Said ‘Stam’ amesema kikosi chao kimeanza kuonyesha matumaini na kutibu madhaifu yaliyokuwepo hivyo wako tayari kuzipambania alama tatu katika mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga.

Stam ambaye kwa sasa anasaidiana na Khalid Adam waliiongoza timu hiyo juzi kupata sare ya bao 1-1 na Pamba Jiji katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza huku Kocha Mkuu, Robert Matano raia wa Kenya akikosekana kwenye benchi.

Alisema mchezo huo umewapa matumaini makubwa kwa namna ambavyo wachezaji wake walipambana na sasa kilichobaki ni kwenda kujiandaa dhidi ya Yanga, mchezo wa raundi ya 27 utakaochezwa katika Uwana wa Tanzanite, Manyara.

“Tunajua mechi ya Yanga ni ngumu lakini tunacheza na timu yoyote inayokuja kwenye ligi kwa sababu wote tuko sawa, kuna Azam bado hatujacheza nao lakini tulicheza na Simba tuliona kwa sababu kila kitu ni mpangilio na mkakati kucheza na ile timu,” amesema Stam na kuongeza:

“Sisi tuna imani katika michezo yetu migumu iliyobakia tutapata pointi nne au tatu kwahiyo tuna imani na tuna muda wa kufanya mazoezi tuna siku kama nane hadi 10 kabla ya kucheza na Yanga kuna kitu nafikiri kitafanyika tutakwenda vizuri katika mchezo huo na wala hatuna amshaka nalo.”

Akizungumzia sare dhidi ya Pamba Jiji ambapo Fountain Gate ilisawazisha dakika ya 60 kupitia kwa Elie Mukono baada ya kutanguliwa dakika ya 21 kwa penalti ya Mathew Tegis ambaye pia alikosa penalti nyingine dakika ya 90, Stam aliwapongeza wachezaji wake kwa kuipigania timu licha ya uchovu.

 “Tunawapongeza wachezaji na tunaondoka hapa tukiwa tuna nguvu tunakwenda kujiandaa kwa mchezo unaofuata dhidi ya Yanga. Tumetoka kupoteza mechi tatu kwa idadi kubwa ya mabao lakini leo tumepata pointi moja tulijipanga na kurekebisha makosa,” amesema Stam

Sare hiyo imewezesha Fountain Gate kufikisha alama 29 na kusalia katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikicheza michezo 26 na kushinda nane, sare tano na kupoteza 13 huku ikifunga mabao 29 na kuruhusu 47.

Tangu ujio wa Robert Matano na msaidizi wake Amri Said ‘Stam’ klabuni hapo Januari 10, 2025 kurithi nafasi ya Mohamed Muya aliyetimuliwa Desemba 29, 2024, timu hiyo imeshinda mbili, sare tatu na kupoteza tano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *