Ssali alivyoacha alama na mahojiano ya vigogo

Dar es Salaam.  Sauti ya Shaka Ssali (71), aliyekuwa mtangazaji maarufu wa Kituo cha Televisheni cha Sauti ya Marekani (VOA), ambaye amefariki dunia nchini Marekani, itaendelea kuishi katika kumbukumbu za Watanzania.

Mkongwe huyo wa habari na mzaliwa wa Uganda, Ssali ameaga dunia juzi akiwa na umri wa miaka 71, wiki mbili kabla ya kufikisha miaka 72 huko Virginia, nchini Marekani.

Watanzania wengi walimsikia na kumuona Ssali kupitia televeshini na redio za Tanzania katika kipindi chake cha Straight Talk Africa kupitia Idhaa ya Sauti ya Amerika (VOA).

Miongoni mwa mambo yatakayomfanya Ssali kuendelea kubaki kwenye kumbukumbu za Watanzania ni msukumo wake katika suala la ‘Haki ya Uhuru wa Kujieleza’, nchini Tanzania akihusisha na tukio la Septemba 7, 2017 pale Tundu Lissu alipopigwa risasi zaidi ya 30 akiwa ndani ya gari lake nje ya nyumba yake eneo la Area D, Site 3 mjini Dodoma.

Kumbukumbu nyingine za Ssali zitakazoendelea kuwepo kwa Watanzania ni mahojiano yake mengine na Tundu Lissu yaliyokuwa na mada iliyoitwa ‘Urithi wa Rais John Magufuli’, hii ni baada ya kifo cha Rais Magufuli na Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania wa kwanza mwanamke.

Mahojiano hayo yalifanyika kwa njia ya mtandao, wakati huo Lissu akiwa nchini Ubelgiji na Ssali akiwa Marekani.

Pia, kumbukumbu nyingine kwa Watanzania ni mahojiano kati ya Ssali na Bernard Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa wakati huo yaliyohusu miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.

Membe kwenye mahojiano hayo alimwambia Ssali anawapeleka viongozi wa dunia Butiama mkoani Mara kwenye eneo alilozaliwa na kuzikwa Mwalimu Nyerere na kuwafikisha kwenye vivutio vya Tanzania, zikiwamo mbuga za wanyama.

Pia, Ssali ataendelea kuwa kwenye kumbukumbu za Watanzania alipofanya mahojiano na mwanasiasa na Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa huko Zanzibar, kuhusiana na Mahakama ya juu nchini Kenya kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais.

Tume ya Uchaguzi ilikuwa imemtangaza Rais Uhuru Kenyatta mshindi akiwa na kura 8,203,290 (asilimia 54.27), huku kura za Raila Odinga zikiwa 6,762,224 (asilimia 44.74).

Ssali kwenye mahojianio hayo alimtambulisha Lowassa kama ‘mwanasiasa mvumilivu zaidi’.

Ilivyokuwa mjadala wa Ssali, Lissu, Masilingi

Mjadala huo uliongozwa na mtangazaji Ssali ukiwa na mada ya mada ya ‘Haki ya Uhuru wa kujieleza’, mbali na Lissu aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) kwa wakati huo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi, wanajopo wengine walikuwa Jon Temin kutoka taasisi ya Freedom House na mwanasiasa wa upinzani wa Uganda, Robert Chagulani maarufu kama Bobi Wine.

Mjadala huo uliendeshwa kupitia kipindi cha Straight Talk Africa kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Sauti ya Marekani (VOA), huku kila mmoja akipangua hoja za mwenzake.

Masilingi alikuwa balozi wa pili kumjibu Lissu, baada ya siku tano kupita Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi kumjibu Lissu kutokana na mbunge huyo kueleza madai mbalimbali kuhusu Serikali na jinsi alivyoshambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, 2017.

Akijibu maswali ya mtangazaji Ssali kuhusu uhuru wa kujieleza na sababu ya Lissu kushambuliwa kwa risasi, Balozi Masilingi alisema licha ya eneo aliloshambuliwa kuwa ni la nyumba za Serikali, halina uhusiano na kubanwa kwa uhuru wa kujieleza.

“Huwezi kuhusisha hilo moja kwa moja na uhuru wa kujieleza bila kuweka uthibitisho. Ndugu yangu alishambuliwa, lakini Rais (John Magufuli- enzi za uhai wake) alitoa tamko la kulaani tukio hilo na kutaka vyombo vya dola kuchunguza tukio hilo. Kila mtu aliguswa na tuko hilo.”

“Uchunguzi bado unaendelea, wanamsubiri arudi (Tanzania) atoe ushirikiano, dereva wake anasubiriwa kutoa ushirikiano. Sasa utakuwaje jaji kuhukumu hilo?” alihoji Masilingi.

Katika majibu yake Lissu alinukuliwa akisema: “Nilishambuliwa kwenye nyumba za Serikali, na nimefanyiwa operesheni 22. Swali la kujiuliza, nani aliyetoa agizo la kuondoa ulinzi katika nyumba za Serikali?

“Pili, hilo eneo linalindwa na CCTV (kamera) ziliondolewa siku moja kabla ya tukio. Hakuna anayejua zilikopelekwa kwa sababu polisi hawasemi walizipeleka wapi. Ninazungumza na watu, hakuna mtu aliyehojiwa.”

Lissu alikuwa nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu alikokwenda Januari 6, 2018 akitokea hospitalini Nairobi, Kenya.

Mnadhimu mkuu huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni nchini alipelekwa Nairobi akitokea Hospitali ya Rufaa ya Dodoma baada ya kushambuliwa kwa risasi mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya bunge.

Ssali ni nani?

Shaka Ssali, maarufu kama ‘Kabale Kid’, alizaliwa katika Wilaya ya Kabale, Uganda, ambapo maisha yake ya awali yalikuwa na changamoto nyingi.

Katika utoto wake, Ssali alihudumu jeshini kabla ya kuhamia Marekani, ambapo alisoma na kupata Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Utamaduni kutoka Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA).

Mei 2021, Ssali alistaafu kutoka Idhaa ya Sauti ya Amerika (VOA) baada ya huduma ya miaka 29, akiwa amehudumu zaidi ya miongo miwili kama mwanzilishi, mtangazaji, na mhariri mkuu wa kipindi cha Straight Talk Africa.

Kipindi hicho kilikuwa ni jukwaa muhimu kwa viongozi wa Afrika, wachambuzi, na wananchi kujadili masuala muhimu ya demokrasia, utawala bora, na maendeleo ya bara la Afrika.

Katika utendaji wake wa kitaaluma, Ssali alifanya mahojiano na viongozi wakuu wa Afrika, wakiwemo marais na mawaziri wakuu, huku akihakikisha sauti za wananchi wa kawaida pia zinapata nafasi katika mijadala kuhusu uongozi na maendeleo.

Aprili 2024, taarifa za kifo chake zilienea kwenye mitandao ya kijamii, lakini Ssali alikanusha habari hizo kwa video aliyoitoa akitania, “Taarifa kuhusu kifo changu zimepotoshwa kwa kiwango kikubwa.”

Shaka Ssali atakumbukwa kama mchoraji wa habari mwenye mafanikio. Aliheshimiwa na kupokea tuzo nyingi kutokana na mchango wake mkubwa katika taaluma ya uandishi wa habari.

Alikuwa gwiji wa uandishi wa habari na urithi wake utaendelea kuwa chanzo cha motisha kwa waandishi wa habari na watangazaji wa kizazi kijacho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *