Spurs, Man United sio kinyonge EPL

London, England. Tottenham Hotspur na Manchester United haziko pazuri kwenye msimamo wa ligi lakini hilo haliondoi ugumu wa mechi baina yao leo kwenye Uwanja wa Tottenham London.

Utofauti wa pointi mbili uliopo baina ya timu hizo mbili, unalazimisha kila moja kupata ushindi leo ili iweke vyema hesabu zake katika mbio za kusaka nafasi za kucheza mashindano

 ya Ulaya msimu ujao.

Manchester United iko nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) ikiwa na pointi 29 na nyuma yake ipo Spurs yenye pointi 27.

Hii inamaanisha kwamba ushindi leo utaifanya Manchester United kuipiku Spurs kwa tofauti ya pointi tano lakini kama itapoteza, Tottenham itapanda juu yao kwa pointi moja zaidi.

Mchezo uliopita baina yao ambao ulichezwa katika Uwanja wa Old Trafford, Spurs iliondoka kibabe kwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Manchester United kwa mabao yaliyofungwa na Brennan Johnson, Dejan Kulusevski na Dominic Solanke.

Man United inaingia katika mechi hiyo ikiwa imetoka kupata ushindi katika mechi nne kati ya tano zilizopita za mashindano tofauti huku ikipoteza moja wakati Tottenham yenyewe katika mechi tano zilizopita imepata ushindi mara mbili tu huku ikipoteza mechi tatu.

Mchezo huo itachezeshwa na refa Peter Bankes akisaidiwa na Eddie Smart na Nick Greenhalgh huku refa wa akiba akipangwa kuwa Michael Salisbury.

Mchezo mwingine leo utakuwa baina ya Liverpool itakayoikaribisha Wolves katika Uwanja wa Anfield kuanzia saa 11:00 jioni.

Baada ya kuangusha pointi mbili katika mechi iliyopita dhidi ya Everton iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2, hapana shaka leo ni mchezo ambao Liverpool inahitaji pointi tatu ili iweze kujiweka katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu.

Refa Simon Hooper ndio atachezesha mechi hiyo akisaidiwa na Adrian Holmes na Simon Long na mwamuzi wa nne atakuwa ni Sam Barrott.