Spurs, Man United kwenye mechi za kibabe

London, England. Baada ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kupigwa juzi na jana, leo Europa League itaendelea katika hatua ya nusu fainali ambapo Manchester United itakuwa Hispania kuvaana na Athletic Bilbao, huku Bodo/Glimt ikisafiri kutoka Norway hadi London kuumana na Tottenham.

Achana na rekodi, Spurs imepata matumaini mengine ya kushinda mechi hii ya nyumbani baada ya kutoka kwa taarifa kwamba baadhi ya wachezaji muhimu wa wapinzani wao watakosekana kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Jumla ya wachezaji watatu wa Glimt watakosekana ikiwa ni pamoja na Both Berg na Evjen ambao walionyeshwa kadi zao za tatu mfululizo katika kipindi cha pili cha mechi ya robo fainali dhidi ya Lazio.

Mbali ya mastaa hao ambao walicheza karibia mechi zote za michuano hiyo hadi kufikia sasa, pia Glimt itamkosa straika wake Andreas Helmersen, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika muda wa dakika 30 za ziada katika mechi ya Lazio.

Hakuna historia iliyopo kati ya Spurs na timu hii kwa sababu hazijawahi kukutana ingawa Wanorway hawa wanaonekana kuwa tishio baada ya kuitoa Lazio katika robo fainali.

Mashetani Wekundu, Man United wao watakuwa na kibarua cha kubadilisha rekodi mbaya ambayo wamekuwa nayo dhidi ya Bilbao ambayo haijawahi kuifunga katika mechi tatu ilizokutana nayo ambapo ilichapika mbili na moja ikamalizika kwa sare.

Man United pia iliwahi kufungwa mchezo wa fainali ya michuano hii dhidi ya Villarreal mwaka 2021 kwa penalti 10-11.

Mashetani Wekundu walitolewa na Sevilla katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa, msimu wa 2017/18, pia mwaka 2020 walitolewa katika hatua hiyo hiyo dhidi ya Sevilla ambao pia waliwatoa mwaka juzi.

Hata hivyo, huenda mashabiki wakapata matumaini zaidi baada ya taarifa za kurejea kwa baadhi ya mastaa kama Matthijs de Ligt na Amad Diallo ambao wameshaanza mazoezi na timu baada ya kuwa nje kwa muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *