Afrika Kusini. Staa wa Afrika Kusini, Tyla, (23) ameweka rekodi kama msanii wa kwanza solo Afrika kwa wimbo wake (Water) kusikilizwa zaidi ya mara bilioni 1 katika mtandao wa Spotify, rekodi ambayo imethibitishwa wiki hii.
Kufuatia rekodi hiyo, Mkuu wa Muziki Spotify barani Afrika, Phiona Okumu amesema hatua hii ni ushuhuda wa talanta kubwa ya Tyla, bidii na nguvu ya muziki kuvuka mipaka, kitu kitachowasukuma na wasanii wengine

Utakumbuka wimbo huo ulitoka Julai 28, 2023 chini ya FAX na Epic Records ndiyo uliobeba jina la albamu yake ya kwanza iliyoachiwa Machi mwaka jana, ulipata mapokezi mazuri na kufikia Jumatano (Feb. 19) ukaweka rekodi hiyo Spotify.
Ni wimbo uliotoa remix rasmi zilizowashirikisha Travis Scott na Marshmello huku ukishika namba 7 kwenye chati ya Billboard Hot 100, na namba 1 kwenye Billboard U.S Afrobeats Songs kwa wiki 43, kwa ujumla ulikaa katika chati hii wiki 55.
Tyla, mzaliwa wa Johannesburg hapo Januari 30, 2002, aliweka rekodi kama msanii mdogo zaidi na wa pili nchini Afrika Kusini kuingia katika chati ya Billboard Hot 100 baada ya miaka 55.

Kutokana na mafaniko ya wimbo huo, Tyla ameshinda tuzo kibao za kimataifa ikiwemo Grammy, tatu za MTV Europe Music Awards (EMAs), mbili za BET, mbili za Billboard na MTV Video Music Awards (VMAs), zote hizi akishinda mwaka uliopita.
“Tunajivunia sana mafanikio ya kihistoria ya Tyla, huu ni msukumo kwa wasanii wanaochipukia barani Afrika na ulimwenguni kote, na tunaheshimika kuwa tumeshiriki katika safari yake,” alisema Phiona Okumu, Mkuu wa Spotify Afrika katika taarifa yake.
Kwa sasa Tyla sio tu anajiunga na klabu ya mabilionea wa Spotify, bali mkali huyo wa kibao, Push 2 Start (2024) anajiunga na kundi la kipekee zaidi la wasanii wachache wa Kiafrika ambao wamefikia hatua hii muhimu.

Mbali na hilo, Spotify imethibitisha kuwa Tems wa Nigeria ndiye msanii wa kwanza wa kike Afrika kwa wimbo wake kusikilizwa zaidi ya mara bilioni, ni kupitia wimbo, Wait For U (2022) alioshirikishwa na Future pamoja na Drake.
Nyimbo nyingine zilizojumuisha wasanii kutoka Afrika na kusikilizwa zaidi ya mara bilioni Spotify, ni One Dance (2016) wake Drake akiwashirikisha Wizkid na Kyla, pia kuna Calm Down (2022) wake Rema akimshirikisha Selena Gomez.
Hivyo, Tyla sio msanii wa kwanza au wa kwanza wa kike Afrika kwa wimbo wake kusikilizwa Spotify zaidi ya mara bilioni 1, bali ni wa kwanza kufikia mafanikio hayo kupitia wimbo alioimba pekee yake, yaani solo.
Utakumbuka mwaka uliopita Tyla alishinda tuzo tatu za MTV EMAs kwa mpigo akiwa ni msanii wa kwanza Afrika, na hatua ya kushinda kipengele cha Best R&B, ilimfanya kuwa mwanamke wa pili duniani asiyetokea Marekani kufanya hivyo baada ya Rihanna.