Spika wa Bunge la Iran ataka Umoja wa Mabunge dunia ulaani mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza, Lebanon

Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf anasema nchi wanachama wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) zinapaswa kuwa na misimamo ya wazi kuhusu mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na Lebanon na kulaani ukatili wa utawala huo dhidi ya raia.

Qalibaf aliyasema hayo katika mkutano wake wa Jumapili na Rais wa IPU Tulia Ackson kando ya Mkutano wa 149 wa IPU unaofanyika Geneva, Uswisi.

Amesema watu wa dunia wanatarajia Umoja wa Mabunge Duniani utaongeza mashinikizo ya  kisiasa kwa Israel ili kukomesha jinai zake huko Palestina na Lebanon.

Ameongeza kuwa eneo la Asia Magharibi  sasa liko katika hali ngumu kutokana na mambo yanayoendelea ikiwemo vita kati ya Russia na Ukraine na hujuma za Israel dhidi ya Palestina na Lebanon.

Spika wa  Bunge la Iran amesisitiza kuwa, pale utawala wa Israel kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani unapokiuka sheria zote za kimataifa na za kibinadamu, hakuna anayeweza kutarajia kuwepo amani na usalama.

Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf na Rais wa IPU Tulia Ackson

Qalibaf amesisitiza umuhimu wa kushughulikia suala la Palestina na kusema washiriki katika mkutano wa kilele wa IPU wanapaswa kuchukua hatua kuelekea kupitishwa azimio kwa kuzingatia uratibu chanya kati ya nchi za Kiarabu, Kiislamu na Asia.

Kwa upande wake, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani  Tulia Ackson, ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema IPU inapinga vita na imeunda kamati ambayo ina jukumu kubwa la kuweka amani katika eneo hilo.

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani  ameongeza kuwa pande zote lazima ziendelee kujitolea na kujitahidi kuleta amani na utulivu.