Spika wa Bunge Kenya asema: Wabunge mtasafiri kwa treni, si kwa ndege, tunabana matumizi

Spika wa Bunge la Kenya amesema wabunge watakaoshiriki katika michezo baina ya wabunge wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), watasafiri kwenda Mombasa kwa gari moshi sio kwa ndege kama ilivyozoeleka.

Akieleza kuwa yeye mwenyewe pia atasafiri kwa gari moshi, Moses Wetang’ula amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya taasisi hiyo kupunguza gharama ili kuelekeza pesa kwa mipango inayofaidi raia moja kwa moja.

“Nawaalika Mombasa kwa michezo baina ya mabunge ya EALA ambapo wabunge kutoka mataifa manane wanachama watashiriki. Nyie, pamoja na Spika, mtasafiri kwa SGR”, alisema jana Bwana Wetang’ula katika taarifa kwa Bunge la Kenya.

Michezo hiyo, inayoshirikisha fani mbalimbali, imepangwa kuanza Desemba 6 hadi 18 mwaka huu 2024.

Bw. Wetang’ula aliongeza kuwa uamuzi wa kutumia SGR utaisaidia Bunge kulipia gharama za wabunge wengi watakaoshiriki katika michezo hiyo ya EALA.

Uamuzi huo umeungwa mkono na Kiongozi wa Wengi, Bw. Kimani Ichung’wah, japokuwa umepingwa na baadhi ya wabunge. 

Mwezi Julai mwaka huu serikali ya Kenya ililazimika kupunguza mgao wa bajeti kwa matawi yote matatu ya serikali baada ya kukataliwa kwa Muswada wa Fedha wa 2024 uliotarajiwa kuiwezesha serikali kukusanya Shilingi bilioni 346 zaidi.