
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) Mohammad Baqer Qalibaf amesema uwezo wa Iran wa kutetea maslahi yake hautaathiriwa na kuchaguliwa au kuondolewa madarakani marais wa nchi nyingine.
Qalibaf ameyasema hayo leo Jumapili katika kikao cha wazi cha bunge, siku chache baada ya Donald Trump kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Marekani.
Amesema marais wa Marekani hutumia mbinu zinazotofautiana kuonyesha uadui wao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa, suala lililo muhimu ni nguvu za kitaifa za Iran.
Qalibaf aidha amesisitiza kuwa, uwezo wa ndani wa Iran unaotokana na uwezo wa taifa na azma yake imara, jambo ambalo linayalazimisha madola makubwa duniani kuzingatia maslahi ya taifa hili katika maamuzi yao.
Vile vile amewataka viongozi wa Iran kuongeza nguvu za kiulinzi za Iran na kutatua matatizo ya kiuchumi ili kuzidisha nguvu ya kuzuia hujuma ya adui ya nchi mbele ya vitisho na mashinikizo. ya maadui
Hivi karibuni pia, Rais wa Iran alisema: ‘Hakuna tofauti kwa Jamhuri ya Kiislamu ni nani ameshinda uchaguzi wa rais nchini Marekani.’ Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni taifa lenye heshima na adhimu linaloegemea kwenye nguvu zake za ndani.
Wakati huo huo, Gavana wa Benki Kuu ya Iran (CBI), Mohammad-Reza Farzin amesema kuchaguliwa tena Donald Trump kuwa rais wa Marekani hakuna mfungamano wowote na ustawi wa uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu.
Farzin alisema katika mahojiano ya televisheni Jumamosi usiku kuwa, “Trump kama rais hana athari za moja kwa moja kwa uchumi wa Iran kwa sababu hatuna ushirikiano wowote wa moja kwa moja wa kibiashara, kimuamala na kifedha na Marekani au hata Ulaya.”