Spika Qalibaf: Uwekaji wa mashinepewa za kisasa ni jibu kwa ufanyaji mambo kisiasa wa IAEA

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuanza kutumiwa mashinepewa (centrifuges) mpya na za kisasa ni jibu la Jamhuri ya Kiislamu kwa hatua ya baadhi ya nchi ya kuitumia kisiasa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Mohammad Baqer Qalibaf, ameyasema hayo leo katika kikao cha wazi cha Bunge na akabainisha kuwa: muelekeo usioendana na uhalisia, wa kisiasa na haribifu wa nchi tatu za Ulaya na Marekani umepelekea kupitishwa katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki azimio lisilo halalishika na lisiloafikiwa na wote kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.

Qalibaf ameongeza kuwa: Serikali za nchi tatu za Ulaya na Marekani zinazitumia shughuli za nyuklia za amani za Iran kama kisingizio cha kuhalalishia vitendo vyao visivyo vya kisheria na kuitia doa itibari na utendaji huru wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa kuufanya uonekane si mkweli na usio na muamana, na kuchafua mazingira ya ujengaji yaliyoandaliwa ili kuimarisha maelewano kati ya Iran wakala huo.

Spika wa Bunge la Iran amebainsha kuwa, jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuitumia vibaya na kisiasa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki limetekelezwa bila kupoteza muda kwa kuwekea sentrifuji mpya na za kisasa.

Itakumbukwa kuwa tarehe 21 Novemba azimio lililopendekezwa na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Marekani dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran liliidhinishwa na Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Katika azimio hili, bila kuashiriwa chochote kuhusu mashirikiano inayotoa Iran kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Tehran imetakiwa ichukue kile kilichoitwa “hatua za lazima na za haraka” kutatua masuala yanayodaiwa ya usimamizi…/