Kama wewe ni shabiki wa Yanga au Simba na una tabia ya kununua tiketi siku ya mchezo pindi timu hizo zinapokutana katika Kariakoo Dabi, basi soma hii.
Pale Afrika Kusini, Mei 3, 2025 itapigwa mechi ya watani, mechi kubwa ndani ya Taifa hilo kati ya wenyeji Kaizer Chiefs dhidi ya Orlando Pirates.

Hii ni moja kati ya dabi bora Afrika, ina ushindani mkubwa pengine zaidi ya Kariakoo Dabi kutokana na msisimko mkubwa wakati miamba miwili hii inapokutana.
Hapa zinakutana timu zote ambazo mashabiki wao huwa hawataki kusikia wanaikosa mechi kama hii.
Aprili 8 mwaka huu, wenyeji Kaizer Chiefs walitangaza rasmi kuanza mauzo ya tiketi za mchezo huo na ndani ya siku takribani 13 yaani wiki mbili hazijatimia kwa utimamu tiketi zimekwisha leo Aprili 19.
Kwenye mauzo hayo hakukutumika mkutano wowote wa Afisa Habari wa klabu wala kufanya kampeni za hamasa kwa mashabiki kuujaza uwanja.

Pengine Kaizer Chiefs imetumia matokeo ya mchezo wao wa mwisho wa ushindi mkubwa mbele ya Mamelodi Sundowns wakiichapa mabao 2-1 kwenye mechi ya nusu Fainali ya Kombe la Nedbank kuwavuta mashabiki wao kwa wingi.
Tukumbuke kabla ya matokeo hayo tayari tiketi zilishaanza kuuzwa na Kaizer inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Mtunisia Nasredine Nabi haikuwa na matokeo mazuri.
Achana na matokeo hayo ya Nabi, Kaizer maarufu kwa jina la Amakhosi imepoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Orlando huku ya mwisho ikilala kwa bao 1-0.
Matokeo hayo nayo hayakufanikiwa kuwavunja nguvu mashabiki wao, bado wakazishambulia kwa nguvu tiketi na zikaisha zikiwa zimebaki siku 13 kabla ya mechi kupigwa.
Mashabiki wengi bado wanataka tiketi ikiwezekana hata kwa kuzilangua mara tu baada ya kutangazwa kwamba tiketi zote za mchezo huo zimekuwa ‘sold out’.

Tambua kwamba mchezo huo utapigwa Uwanja wa FNB uliopo Jiji la Johannesburg unaochukua mashabiki 94,736.
Kaizer Chiefs imetumia tangazo moja pekee kwenye ukurasa wake wa Instagram kutangaza mchezo huo na tangazo la mwisho likawa tiketi zimekwisha.
Mechi hiyo kwa kuwa mwenyeji ni Kaizer Chiefs, Orlando Pirates hawajafanya lolote kuitangaza wakiwaacha wapinzani wao pekee kuhusika.
Baada ya mechi ya Mei 3 mwaka huu, jipange kutazama mechi nyingine kama hiyo kwenye Fainali ya Nedbank, miamba hiyo itakapokutana Mei 10, 2025.