Sowah, Sillah kuwachomoa wawili Yanga

KUNA hesabu Kali ambazo Yanga inazipiga kibabe ndani ya kikosi chao cha msimu ujao wakitaka kuingiza silaha za maana ndani ya mziki wao lakini kuna wawili lazima waachie nafasi fasta ili dili hizo zikamilike.

Yanga inataka kumsajili mshambuliaji Jonathan Sowah ambaye yupo pale Singida Black Stars, jamaa huyo licha ya kuingia dirisha dogo msimu huu, lakini ameshaweka wavuni bao zake saba fasta katika mechi saba tu alizocheza kwenye ligi.

Yanga washambuliaji wake wawili Prince Dube na Clement Mzize wako juu kule kwenye msimamo wa ufungaji kila mmoja akifunga mabao 10 nyuma ya kinara wa ufungaji ambaye ni kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua mwenye mabao 12.

Hata hivyo, Yanga bado inataka kumuongeza Sowah ikipiga hesabu kwamba msimu ujao wanaweza kumpoteza Mzize ambaye ana ofa zisizopungua tano mezani za kufanya biashara mwisho wa msimu huu.

Kama Mzize ataondoka, Yanga inataka nafasi yake ichukuliwe na Sowah lakini haitatosha, vigogo hao watalazimika kumpunguza mtu mmoja kwenye wachezaji wake 12 wa kigeni katika kikosi cha sasa.

Hesabu za Yanga haraka zimetua kwa mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuachwa msimu huu ukimalizika akiwa amefunga mabao matatu na asisti moja kwenye ligi.

Habari mbaya zaidi kwa Musonda ni kwamba mwisho wa msimu huu mkataba wake utakuwa umefikia tamati ndani ya Yanga, hatua ambayo itairahisishia timu hiyo kufanya uamuzi wa fasta kwani Dube bado yupo kwenye mkataba mrefu.

Kwenye maboresho hayo pia yupo winga Djibril Sillah wa Azam ambaye Yanga inampigia hesabu za kikubwa kumchomoa kwa matajiri hao wa Chamazi.

Taarifa zinabainisha kwamba, uongozi wa Azam na Sillah ni kama kila mmoja anamtega mwenzake katika dili jipya huku baadhi ya viongozi wakidai hawaridhishwi na uwezo wake vile walivyotarajia.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Yanga imempa ofa ya maana Sillah, huku winga huyo fundi wa mguu wa kushoto akionyesha kuvutiwa nayo.

Yanga inataka kuwa na winga fundi mwenye akili na ubora wa kutumia mguu wa kushoto kwenda kuongeza nguvu huku ikiwa tayari imeshampata Jonathan Ikangalombo ambaye anajua kutumia mguu wa kulia.

Sillah ndio kinara wa mabao mpaka sasa kwenye kikosi cha Azam akiwa ameshaweka wavuni mabao saba kwenye ligi msimu huu akiwa staa muhimu ndani ya kikosi cha matajiri hao.

Hata hivyo, Yanga inafahamu kwamba kama itafanikiwa kuinasa saini ya Sillah, italazimika kumuacha mtu mmoja kwenye wachezaji wake wa kigeni.

Ndani ya kikosi hicho anatajwa Clatous Chama anaweza kupisha nafasi kufuatia mabosi wa timu hiyo bado hawajaridhishwa na ufanisi wake ndani ya kikosi hicho.

Chama amekuwa anakosa muda wa kutosha kwenye kikosi hicho, akifunga mabao matatu pekee kama Mzambia mwenzake, Musonda lakini upande wa asisti anazo mbili.

Jeuri nyingine ambayo wanaipata Yanga ni kwamba eneo ambalo anacheza kiungo huyo wa zamani wa Simba na Zesco ya Zambia, kuna mafundi wengi kama Pacome Zouzoua na Stephanie Aziz KI ambao wanaipa timu hiyo nguvu ya kufanya uamuzi huo mgumu.

Bahati mbaya zaidi kwa Chama ni kwamba mkataba wake wa gharama kubwa aliposaini mwaka mmoja ndani ya Yanga unafikia tamati mwisho wa msimu huu hatua ambayo inaongeza utata wa hatma yake ndani ya klabu hiyo.

SILLAH, SOWAH WANAINGIAJE KIKOSINI?

Kikosi cha Yanga hivi sasa kina nyota wengi wazuri ambao ukikiangalia kwa haraka unaweza kuchanganyikiwa kuwapanga 11 wanaoanza, lakini ukifuatilia kwa umakini zaidi mechi zao zilizochezwa unapata picha halisi.

Yanga sasa kikosi chao kipo hivi; Djigui Diarra, Israel Mwenda, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Prince Dube, Pacome Zouzoua na Clement Mzize.

Kupitia kikosi hicho, Sillah na Sowah wanaweza kuanza kwa kuwatoa Abuya na Dube.

Dube anampisha Sowah kikosini kufuatia Mghana huyo kuonekana kuwa mzuri zaidi katika kutumia nafasi kulinganisha na Dube ambaye licha ya kufunga mabao 10 msimu huu, lakini amekosa nafasi nyingi za wazi.

Kwa Abuya, kuanzia kwake nje inategemea na mfumo wa kocha kwani akiamua kuwa na viungo wengi wachezeshaji, basi Mkenya huyo hana nafasi zaidi ya kutumika Sillah mwenye uwezo wa kushambulia kupitia pembeni, kisha Pacome akisimama kiungo cha kati. Sillah akipewa wingi moja, nyingine anakuwepo Maxi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *