
MSHAMBULIAJI machachari wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah mwenye mabao saba kwenye michezo saba ya ligi, anaamini kuwa msimu huu anaweza kuvunja rekodi yake ya mabao aliyoiweka miaka miwili iliyopita.
Msimu wa 2022/2023, Sowah alifanya makubwa nchini Ghana alipokuwa akiichezea Medeama, ambapo aliibuka mfungaji bora wa timu yake. Ilikuwa ni msimu wake wa mafanikio zaidi kwa kufunga mabao 12, lakini sasa, akiwa Singida BS, anaona nafasi ya kuandika historia mpya.
Licha ya kwamba amejiunga na Singida BS katika dirisha dogo la usajili, Sowah ameonyesha uwezo mkubwa kwa kuwa na wastani wa kufunga kwenye kila mchezo wa Ligi Kuu Bara. Hii ni ishara kwamba anaweza kufikia na hata kupita rekodi yake ya awali.
“Tangu nimewasili hapa, nimepokewa vizuri na wachezaji wenzangu na benchi la ufundi. Hilo limenisaidia kuzoea haraka mfumo wa timu na kufunga mabao,” amesema Sowah.
“Kwa mshambuliaji huyu, mabao saba si mwisho wa safari, bali ni hatua ya kwanza kuelekea malengo makubwa. “Najua ninaweza kufanya zaidi. Niko katika kiwango kizuri na kama nitaendelea hivi, basi hakuna kinachonizuia kufunga mabao mengi zaidi msimu huu.”
Kile kinachomvutia zaidi ni kwamba tayari amefikia idadi ya mabao aliyofunga msimu uliopita alipokuwa akiichezea Al Nasr ya Libya. Msimu huo haukuwa mzuri sana kwake, lakini sasa anaiona Singida BS kama mahali sahihi pa kung’ara.
Makocha wake na mashabiki wanavutiwa na namna anavyocheza. Ana kasi nzuri, anajua kujipanga ndani ya eneo la hatari, na ni mbabe wa mabeki wachovu.
“Najua kazi yangu ni kufunga, na nitaendelea kupambana ili niwe na msimu bora zaidi,” amesema.
Singida BS, ambayo inawania nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi, inafaidika sana na uwepo wa Sowah. Mabao yake yamekuwa chachu ya ushindi kwa timu, na kila mchezo anaingia uwanjani na njaa ya kuongeza idadi yake ya mabao.
Singida BS imesaliwa na michezo saba mbele yao ambayo ni dhidi ya Fountain Gate, Azam, Coastal Union,Tabora United, Simba, Dodoma Jiji na Prisons.