Sowah kiatu anakitaka Bara

MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah ameanza maisha yake vyema katika kikosi hicho tangu ajiunge nacho dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya, hivyo kuanza kutishia upya vita ya ufungaji bora akionyesha anakitaka kiatu cha dhahabu.

Sowah tangu ajiunge na Singida amecheza michezo sita ya Ligi Kuu na kufunga mabao sita ikiwa ni wastani wa bao moja kila mchezo, akizidiwa manne na vinara, Prince Dube, Clement Mzize (Yanga) na Jean Charles Ahoua wa Simba wenye 10.

Akizungumzia kiwango cha nyota huyo, kaimu kocha mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma alisema usajili huo kwa kiasi kikubwa umeamsha morali ya upambanaji kwa washambuliaji wengine, jambo linalowaweka nafasi nzuri ya ushindani msimu huu.

“Malengo yetu ni kumaliza nafasi nne za juu, sasa kama ni hivyo ni lazima kila mmoja wao aonyeshe ushindani kwa sababu hiyo ndio siri ya kufanikisha hilo, Sowah ni mchezaji mzuri na hahitaji kumzungumzia sana kutokana na kile anachofanya.”

Ouma aliyekaimu nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Miloud Hamdi aliyejiunga na Yanga, alisema uwezo unaoonyeshwa na nyota huyo sio faida tu kwa timu, isipokuwa hata mchezaji mmoja mmoja inawaongezea morali ya kupambana kila wanapopewa nafasi.

Nyota huyo raia wa Ghana, ameendeleza kiwango bora kwani hata alivyokuwa na Al-Nasr Benghazi FC aliyoichezea kwa miezi sita, alihusika na mabao saba na kikosi hicho, baada ya kufunga matano na kuchangia mawili ‘Assisti’ kwenye mechi tisa.

Sowah alijiunga na Al-Nasr Benghazi Januari 27, 2024, akitokea Medeama ya kwao Ghana ambapo pia alionyesha kiwango bora na kuzivutia klabu mbalimbali ikiwemo Yanga baada ya kuwasumbua kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi.

Akiwa na Medeama aliyojiunga nayo Januari 11, 2023, akitokea Danbort FC, alicheza michezo 20 ya Ligi Kuu ya Ghana na alifunga mabao 16, huku katika Ligi ya Mabingwa Afrika, alifunga matatu kwenye mechi zake saba alizochezea kikosi hicho.

Katika michuano ya FA ya Ghana alifunga mabao matatu katika michezo saba na Medeama na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka, huku akijumuishwa kikosi cha mwisho cha Ghana kwenye fainali za Mataifa Afrika (AFCON) 2023, zilizofanyika Ivory Coast.