Sowah, Bwenzi wawatisha Mzize, Dube

Dar es Salaam. Clement Mzize, Prince Dube na Charles Ahoua wanaongoza chati ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu msimu huu kila mmoja akiwa amefunga mabao 10.

Mbio za kufika kileleni kwenye chati hiyo walianza tangu msimu huu ulipoanza na baadhi ya mabao walifunga katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Hata hivyo maingizo mawili ya wachezaji katika dirisha dogo la usajili yanaonekana kuanza kutishia uwezekano wa Dube, Ahoua au Mzize kuibuka mfungaji/wafungaji bora katika Ligi msimu huu.

Tangu Sowah ajiunge na Singida Black Stars katika dirisha dogo la usajili lililoanza Desemba na kumalizika Januaria kama ilivyo kwa Bwenzi aliyejiunga na KenGold katika kipindi hicho, wameonyesha muendelezo mzuri wa kufumania nyavu katika mechi walizozitumikia timu zao.

Katika mechi sita ambazo Sowah ameitumikia Singida Black Stars kwenye Ligi Kuu msimu huu, mshambuliaji huyo raia wa Ghana amefunga mabao sita ikiwa ni wastani wa bao moja kwa mchezo.

Nyota njema kwa Sowah ilianza kuonekana katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 ambapo alifunga moja huku lingine likifungwa na Marouf Tchakei na kisha akafunga dhidi ya JKT Tanzania.

Baada ya hapo akapachika bao moja katika mechi waliyopoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga na akafunga bao moja katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Pamba Jiji FC ambapo lingine moja lilipachikwa na Sergie Pokou.

Mshambuliaji huyo alifikisha mabao sita kwa kufunga mabao mawili katika mchezo uliopita ambao timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mashujaa FC ambapo lingine moja lilifungwa na Elvis Rupia.

Kwa upande wa Bwenzi yeye amefunga mabao matano katika mechi sita zilizopita za KenGold.

Alianza kwa kupachika bao moja katika kichapo cha mabao 6-1 walichokipata kutoka kwa Yanga kisha akafunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate.

Bwenzi alipachika bao lingine katika sare ya bao 1-1 na Tabora United na akafunga bao pekee la KenGold katika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC.

Mchezaji huyo amepachika bao lake la tano katika mechi ambayo KenGold imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania Alhamisi, Februari 27, 2025.

Akizungumzia kasi yake ya kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu tangu alipojiunga na KenGold, Bwenzi alisema inachangiwa na kufanyia kazi kile ambacho anaelekezwa na benchi la ufundi la timu yake.

“Walimu wamekuwa wakinielekeza nini cha kufanya katika mechi na pia mazoezini tumekuwa tukifanyia kazi mapungufu ambayo tumeyaonyesha na namshukuru Mungu nimekuwa nafanya vizuri.

“Kuhusu ufungaji bora ni ndoto zangu. Jukumu langu la kwanza ni kuisaidia timu yangu ya KenGold kubaki kwenye ligi na kama ikitokea nimemaliza nikiwa mfungaji bora litakuwa jambo jema zaidi,” alisema Bwenzi.