Mshambuliaji wa JKT Tanzania, Edward Songo amesema yeye na wenzake katika eneo la ushambuliaji wameshajua tatizo lililopo la ufungaji wa mabao ambalo benchi la ufundi limelifanyia kazi na sasa litapatiwa tiba.
JKT Tanzania inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na alama 27 katika michezo 22, ikishinda sita, sare tisa na kupoteza saba, huku ikifunga mabao 16 na kuruhusu 16.

Ukitoa Simba (8), Yanga (9) na Azam FC (12) JKT Tanzania ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache (16) huku ikiwa na wastani mdogo wa kufunga mabao (16) hivyo haina faida yoyote ya mabao (0).
Kwa kufunga mabao 16, JKT inakuwa kati ya timu zenye mabao machache zaidi kati ya zinazoshika nafasi 10 bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ambapo inazizidi Tanzania Prisons (12), Pamba Jiji (13) na KMC (15) tu.

Songo ametoa kauli hiyo leo Machi 6, 2025 jijini Mwanza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mchezo wa kesho Ijumaa dhidi ya Tabora United utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni.
“Ni kweli kumekuwa na udhaifu katika eneo letu la ushambuliaji lakini ni suala ambalo tunalifanyia kazi kwenye kiwanja cha mazoezi na benchi la ufundi limeshaliona hilo na tunapambana kukabiliana nalo. Lakini kufunga siyo suala la mastraika peke yao, mtu yeyote kwenye timu anaweza kufunga, muhimu ni timu ipate alama tatu,” amesema Songo.
Akizungumzia mchezo wa kesho dhidi ya Tabora United, Kocha Msaidizi wa JKT Tanzania, Raymond Dotto amesema mabadiliko ya uwanja hayajaathiri maandalizi yao kwani kikosi hicho kilijiandaa kukabiliana na mazingira yoyote ambayo yangejitokeza mbele yao.

“Tunacheza na mtu ambaye yuko juu yetu na tunajua ubora wao wana wachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu mkubwa lakini tumejiandaa vizuri namna ya kukabiliana nao, tunasubiri tu kesho ifike tutekeleze mipango yetu,” amesema Dotto.