UHONDO wa Ligi Kuu Bara umerejea tena baada ya kusimama kwa wiki moja ambapo viwanja viwili leo Ijumaa vitawaka moto, kazi kubwa ikiwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya wakati maafande wa Tanzania Prisons na JKT Tanzania watakapoonyeshana kazi, huku jijini Dar kuna dabi nyingine.
Kwenye Uwanja wa KMC Complex, wenyeji KMC timu inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni itaialika Dodoma Jiji inayomilikiwa na Jiji la Dodoma, mechi zote zikipigwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Mechi ya jijini Mbeya, inazikutanisha timu zilizopo katika nafasi tofauti wenyeji wakipambana kujiepusha kushuka daraja, ilihali JKT ikipambana kumaliza ndani ya 6 Bora ya msimu huu, kitu kinachoufanya mchezo huo kuwa mgumu kwa maafande hao.
TZ Prisons iliyopo nafasi ya 14 ikimiliki pointi 24 itakuwa na kazi kubwa mbele ya JKT Tanzania inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 32, huku wenyeji wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi ya kwanza ugenini kwa bao 1-0, mechi iliyopigwa Novemba 24 mwaka jana.
Wenyeji wanatambua matokeo mazuri mbele ya maafande wenzao yatawatoa eneo walilopo na kupanda japo kwa nafasi moja tu kwani itafikisha pointi 27, huku wakiwaombea mabaya KMC itakayokuwa uwanjani kuvaana na Dodoma Jiji inayomiliki pia idadi ya pointi hizo sawa na Pamba Jiji.
Prisons itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi mbili mfululizo zilizopita kwenye uwanja huo dhidi ya Kagera Sugar iliyowalaza bao 1-0 kisha kuizima KenGold kwa 3-1, maafande hao wakicheza kama wageni na kufikisha pointi hizo 24.
Haruna Chanongo, Benno Ngassa na wakongwe waliorejeshwa kikosini baada ya awali kuondolewa Salum Kimenya, Jumanne Elfadhil na Jeremiah Juma wataendelea kutegemewa na Prisons katika mechi hiyo dhidi ya JKT iliyoambulia sare ya 2-2 katika mechi mbili zilizopita mbele ya Dodoma Jiji na Namungo.

Hata hivyo, rekodi nzuri ya JKT kwa mechi za ugenini ikishika nafasi ya saba kati ya timu 16 ikikusanya pointi 12 katika mechi 12 ikiwa na maana kila mechi imevuna alama moja, ilihali Prisons ikishika nafasi ya 14 kwa timu zilizo na matokeo mabaya nyumbani, inaufanya mchezo kuwa mgumu.
Katika mechi 12 zilizokutana kwa timu hizo tangu 2018, JKT imeshinda mechi mbili dhidi ya nne za TZ Prisons na zilizosalia zikiisha kwa sare za aina tofauti na ni mechi mbili tu za Machi 15, 2019 na ile ya Machi 14, 2021 wenyeji wamewahi kushinda nyumbani, huku JKT ikiwa haijawahi kushinda ugenini.
Ikiwategemea Edward Songo, Shiza Kichuya, John Bocco, Ismai,l Aziz Kader na wakali wengine akiwamo kipa Yakoub Suleiman, JKT itakuwa na kazi ya kufuta gundu la kutowahi kuifunga Prisons ikiwa kwao, lakini ikisaka pointi tatu za kuzidi kuwaweka pazuri katika msimamo wa Ligi.
KMC v DODOMA JIJI
Mechi nyingine inayopigwa leo ni Dabi ya Majiji, KMC na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa KMC, huku wenyeji wakiwa na kumbukumbu la kulala 2-1 katika mechi ya duru la kwanza.
KMC ipo nafasi ya 13 kwa sasa ikiwa na pointi 27 kama ilizonazo Pamba Jiji, lakini ikiwa na mwendelezo mbaya kwa mbele ya Dodoma Jiji kwani misimu miwili mfululizo ilipoteza mechi za nyumbani dhidi ya wapinzani wao hao, lakini hata matokeo ya jumla baina yao yanawaangusha.

Katika mechi tisa zilizopigwa katika Ligi baina yao tangu 2020, Dodoma imeitambia KMC mara saba, huku yenyewe ikipoteza mechi mbili zote za ugenini misimu miwili ya mwanzo, kitu kinachoifanya mchezo wa leo kuwa ni wa kisasi kwa wenyeji dhidi ya wageni wao hao.
Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya sita ikiwa na pointi 34 itaendelea kumtegemea kinara wao wa mabao, Paul Peter aliyefunga mabao manane, mbali na wakali wengine ili kuwabana KMC inayopambana kuepuka kushuka daraja.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha wa TZ Prisons, Amani Josiah alisema anatarajia dakika 90 ngumu na muhimu ni kuhakikisha anaendelea alipoishia ili kuipambania timu hiyo kongwe isishuke daraja.
“Hautakuwa mchezo rahisi tuna kutana na timu ngumu kufungika na bora, lakini hilo halitunyimi sisi kuvuja jasho kupambania pointi tatu tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani na kuendeleza ushindi tulioupata mfululizo,” alisema Josiah, huku kocha wa JKT TZ, Ahmed Ally alisema: “Ni mchezo muhimu na tunacheza na timu ambayo inapambania kujikwamua kushuka daraja hivyo hatutarajii urahisi tunatakiwa kupambana.”
Kwa upande wa kocha wa KMC, Kally Ongala alisema timu yake inahitaji pointi tatu muhimu ili kurudi kwenye morali ya ushindani na pia inataka nafasi ya kucheza ligi msimu ujao.
“Tunakutana na wapinzani wagumu na wazuri lakini hilo haliondoi sisi kufanya kilicho bora ili tupate pointi tatu muhimu tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani tukiwa tumetoka kupoteza ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya Namungo.”