SMZ yapokea vifaa vya Sh1.9 bilioni vya kuhifadhia taka

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepokea vifaa vya kuhifadhi na kusafirishia taka ngumu vyenye thamani ya Sh1.9billioni kupitia mradi wa Ukuzaji Uchumi Jumuishi (BIG Z) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Vifaa ambavyo vimekabidhiwa ni gari za kubebea taka, vikapu na makontena ya kuhifadhia, ambapo hizo ni juhudi za kuimarisha usafi kisiwani hapa. 

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo leo, Jumatano Aprili 30, 2025 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu SMZ, Massoud Ali Mohammed amesema vifaa hivyo vitakuwa ni msaada kwao katika kuondoa changamoto ya mrundikano wa taka hali ambayo inalalamikiwa na wananchi wengi.

“Tumepewa vifaa hivi ili kuhakikisha miji yetu inakuwa safi, usafi ni jukumu la kila mmoja na vifaa hivi vitasaidia kupunguza mrundikano wa taka katika maeneo yetu,” amesema Massoud.

Waziri Massoud ameongezea kuwa, pamoja na kupokea msaada huo changamoto ya uchafu bado ipo hivyo magari hayo ya kubebea taka na vifaa vingine vitakabidhiwa kwa watendaji ili kushughulikia tatizo hilo sugu.

Pia, amewataka watendaji wa mabaraza ya Manispaa kutotanguliza muhali kwa wanaochafua mazingira badala yake kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria ili kufika lengo husika.

Kaimu Mratibu wa Mradi wa BIG Z, Hamad Bakar Said amesema mradi huo umejikita katika kuboresha huduma za usafi wa miji ili kuwa na haiba nzuri.

Amesema, magari hayo yaliyokabidhiwa yamenunuliwa na vipuri vya akiba ili vifaa hivyo viweze kuendelea kufanya kazi bila usumbufu.

“Ni matarajio yetu kuwa vifaa hivi vitatumika katika Manispaa kwa lengo lililokusudiwa na tunashauri watumiaji wapatiwe mafunzo ya mara kwa mara ili kuvitumia kwa weledi,” amesema Bakari. 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango, Aboud Hassan Mwinyi amesema vifaa vilivyokabidhiwa katika awamu ya kwanza kupitia mradi huo ulio chini ya wizara ya fedha ni pamoja na magari mawili ya kubebea taka, vikapu 20 vya kuhifadhi taka na makontena kumi.

Amesema kwa awamu ya pili itahusisha ununuzi wa magari mengine 26, yakiwemo ya aina ya kompacta, tipa, na gari la kufagia barabarani.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud alifahamisha kuwa ili miundombinu ifanye kazi vizuri ni lazima kuwepo kwa vitendea kazi vinavyohitajika.

Pia, Ayoub ameeleza kuwa kupokea vifaa hivyo ni kieleelezo cha utayari wao katika kuhakikisha Zanzibar inakuwa safi na kuahidi kushirikiana na Serikali za mitaa katika kuvusimamia vifaa hivyo vitumike kama ilivyokusudiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *