Unguja. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff amesema Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogowadogo kutokana na kutokuwepo kwa uhakika wa marejesho.
Hivyo, ili kuhakikisha wakulima hao wanapata fursa ya mikopo yenye masharti nafuu, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kwa kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea), imeanzisha mpango wa kuwapatia wakulima vijana ujuzi wa kilimo cha kisasa.
Pamoja na maeneo ya kilimo na masoko ya uhakika ndani ya Zanzibar kupitia sekta ya utalii na nje ya nchi kupitia soko la Afrika Kusini kwa kushirikiana na Taasisi ya EARN, ambayo ina uzoefu mkubwa wa sekta hiyo.
Waziri Shariff amesema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir leo Alhamisi Februari 27, 2025 katika mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.

Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad akizungumza katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja
Ameir alihoji ugumu wa kupata mikopo kutokana na kutokuwepo kwa uhakika wa marejesho kunawakwaza wakulima wadogo wadogo kujiendeleza vyema, hivyo Serikali inafikiria kwa wakulima hao ili kunufaika na mikopo nafuu.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Shariff amesema kupitia mpango huo wakulima watapata fursa ya kuuza mazao yao kwa uhakika, jambo ambalo litawasaidia kuwa na mtiririko mzuri wa mapato na hivyo kuwawezesha kurejesha mikopo kwa wakati.
“Mpango huu utapunguza hatari ya ucheleweshaji wa marejesho na kuwajengea uwezo wakulima wadogowadogo sifa ya kuaminika kwa taasisi za kifedha na tayari mazungumzo ya pande zote mbili yameshafanyika,” amesema Shariff.
Amesema hatua hizo zote ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha vijana na wakulima wadogo wanajengewa uwezo wa kifedha na kiteknolojia ili kuchochea maendeleo ya kilimo na uchumi wa Zanzibar.