SMZ yafungua fursa mpya kwa diaspora kuwekeza

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imechukua hatua thabiti kutambua na kuthamini mchango wa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi (diaspora) katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kwa kufanya mageuzi yanayolenga kuwawezesha na kuwahusisha katika kupanga na kushiriki mustakabali wa nchi yao.

Miongoni mwa hatua hizo ni ushirikishwaji rasmi wa diaspora katika uandaaji wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, pamoja na ushiriki wao katika kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001.

Hatua hizo zinalenga kujenga mazingira wezeshi na jumuishi yatakayowahamasisha wanadiaspora kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Mei 15, 2025, kwenye Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Ali Suleiman Mrembo, alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdallah Ameir, aliyetaka kufahamu kama kuna mageuzi ya msingi ambayo Taifa linaweza kujivunia yanayowahusisha diaspora.

Akijibu swali hilo, Waziri Mrembo amesema kuwa, pamoja na hatua nyingine zilizochukuliwa, Serikali imeanzisha mfumo rasmi wa usajili wa diaspora wa Zanzibar, unaowawezesha kupata kadi maalumu ya diaspora.

“Kupitia kadi hii, diaspora wanapata fursa mbalimbali zenye manufaa makubwa, ikiwemo msamaha wa ada ya kibali cha kazi kwa wale wanaorudi kufanya kazi nyumbani,” amesema Waziri Mrembo.

Waziri Mrembo amesema fursa nyingine zinazotolewa kwa diaspora ni pamoja na urahisi wa kupata vibali vya ukaazi, uwezo wa kufungua akaunti katika taasisi za kifedha za ndani, pamoja na ukodishaji wa ardhi kwa tozo maalumu kwa ajili ya uwekezaji au matumizi binafsi.

Ameongeza kuwa, diaspora pia wanaruhusiwa kuwekeza moja kwa moja kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa gharama nafuu na katika mazingira wezeshi, ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika sekta ya utalii, hata katika maeneo ambayo kwa kawaida hayaruhusiwi kwa wageni.

Fursa nyingine ni pamoja na punguzo la gharama za usafiri kwa boti na ndege, ambapo diaspora watalipa viwango sawa na wananchi wa kawaida, pamoja na msamaha wa kodi katika uingizaji wa vifaa vya misaada ya kijamii kutoka nje ya nchi.

Aidha, Waziri Mrembo ametaja uwepo wa fursa za kujitolea katika taasisi za Serikali, kushiriki katika kubadilishana ujuzi, utaalamu na uzoefu walioupata nje ya nchi kupitia wizara na taasisi mbalimbali, kama sehemu ya mchango wao kwa maendeleo ya Taifa.

“Mageuzi haya ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutambua, kuimarisha na kuendeleza mchango wa diaspora katika ujenzi wa taifa lenye maendeleo jumuishi.

“Kwa sasa, zaidi ya wakati mwingine wowote, mlango uko wazi kwa diaspora kuungana na nyumbani kwa nia ya kuchangia maendeleo ya Zanzibar,” amesema Waziri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *