
Unguja. Wakati Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, ikiomba Baraza la wawakilishi kuidhinisha Sh120.89 bilioni mwaka 2025/26, Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mahususi kudhibiti mfumuko wa bei kwa bidhaa na huduma mbalimbali.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuendelea kutoa bei elekezi na kusimamia bidhaa zinazoingia nchini zikiwemo za chakula na vifaa vya ujenzi.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleima Abdulla wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi katika mkutano wa 19 wa baraza la wawakilishi leo Mei 7, 2025 Chukwani Zanzibar.
Amesema matumizi ya ofisi yake ni Sh80 bilioni na ofisi ya baraza la wawakilishi Sh34.7 bilioni huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiombewa Sh6 bilioni.
“Kuimarisha programu za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha ufanisi wa Bandari ya Malindi kwa ununuzi wa vifaa vya kisasa na kuanza kutumika kwa bandari nyingine za Fumba na Mkoani ili kupunguza muda wa kutoa mizigo bandarini,” amesema
Amesema pia Serikali inaimarisha maghala na mifumo ya uhifadhi wa chakula ili kuwa na uhakika wa chakula nchini.
Hemed amesema Serikali itaendelea kuchukua kila aina ya jitihada kuhakikisha mienendo ya biashara inakuwa na unafuu wa bei kwa wananchi ili kupata huduma na bidhaa kwa urahisi na kwa bei nafuu, huku wafanyabiashara na wazalishaji wakipata faida stahiki.
Kutokana na mafanikio ambayo yameonekana kupitia sekta ya uchumi wa buluu, Serikali itaendelea kuipa nguvu sekta hiyo ili kuongeza uzalishaji na kuongeza kipato kwa wananchi na Taifa kwa jumla.
“Tutaimarisha upatikanaji wa huduma na vifaa vya kisasa sambamba na miundombinu inayoendana na sekta hii ikiwemo masoko na viwanda,” amesema.
Kwa mujibu wa Hemed, uchumi wa buluu umekuwa na wanatarajia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa samaki kutoka tani 80,000 mwaka huu na kufikia tani 115,000.
Hata hivyo, amesema licha ya jitihada zinazofanyika kuimarisha kilimo, kinakabiliwa na changamoto ikiwamo nzi waharibifu wa matunda ambao wamekuwa wakiyaharibu tangu yakiwa machanga na yanapopevuka.
Serikali inaendelea na kampeni za kudhibiti nzi hao kwa kutumia mitego na dawa za kuwanasa, ambapo hadi sasa jumla ya mitego 9,203 imesambazwa kwa wakulima. Akizungumzia kuhusu uchaguzi, Hemed amesema Serikali itahakikisha itachukua kila tahadhari na hatua stahiki ili kuwepo na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi
Kwa mujibu wa Hemed, Tume ya Uchaguzi tayari imeweka miundombinu madhubuti itakayowezesha kuendesha uchaguzi huo kwa ufanisi na uwazi zaidi.
“Tayari imepatiwa magari ya kisasa 15 maalumu kwa ajili ya shughuli za uchaguzi sambamba na kuwa na jengo jipya la kisasa lililojengwa kwa kuzingatia mahitaji ya shughuli za uchaguzi kabla, wakati na baada ya kufanyika,” amesema
Ametaja sababu za kukua kwa uchumi wa Zanzibar kwa asilimia 7.4 kuwa ni kuimarika kwa sekta ya kilimo, ambapo kwa mwaka 2024 imekua kwa wastani wa asilimia 3.3 kutoka wastani wa asilimia 2.3 mwaka 2023, na ukuaji huo umetokana na ukuaji sekta ndogo ya uvuvi kwa asilimia 14.2 kutoka asilimia 8.1 mwaka 2023 na sekta ndogo ya mazao kufikia asilimia 6.4.
Pia, kuongezeka kwa uingiaji wa watalii nchini kufikia watalii 736, 755 mwaka 2024 kutoka watalii 638, 498 waliotembelea Zanzibar mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 5.4
Sababu nyingine ni kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa kwa asilimia 13. kufikia miradi 131 yenye thamani ya Sh1.8 trilioni mwaka 2024 kutoka miradi 114 iliyosajiliwa mwaka 2023.
Amesema pato halisi la Taifa limeongezeka kufikia thamani ya Sh4.02 trilioni kutoka Sh3.7 trilioni.
Kuongezeka kwa Pato la Taifa Zanzibar kumesababisha kuongezeka kwa pato la mwananchi kufika Sh3.2 milioni kutoka Sh3.1 milioni mwaka uliopita.
Hemed amesema katika kuboresha maisha ya Wananchi, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) umeendelea kuboresha maisha ya wananchi kwani wengi wamesaidiwa kupitia mfuko huo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa, Othman Machano Said ameshauri Serikali kufanya kila jitihada kuhakikisha mfuko huo unaendelea kwani umewasaidia wananchi wengi kisiwani hapo.
Naye Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Tasaf, Godwin Mkisi ambao walikuwa miongoni mwa waalikwa katika baraza hilo, amesema wanajivunia usimamizi na uratibu wa mfuko huo kwa upande wa Zanzibar na kwamba zaidi ya vikundi 2200 vya ujasiriamali kwa Zanzibar vimenufaika.
“Kaya 260,000 zimehitimu kwenye mfuko na kati ya hizo 22, 000 zilipata ruzuku kwa ajili ya uzalishaji na wanaweza kusimama wenyewe licha ya kuondoka kwenye mpango, tunashukuru uratibu unaofanywa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,” amesema.