
Dar es Salaam. Unaweza kusema ni mauaji yaliyoacha kitendawili cha sababu hasa ya aliyeyatekeleza kuchukua uamuzi huo. Inaelezwa Richard Yakobo, alinunua lita tatu za petroli na kulipua nyumba ya mke wake wa zamani na kumuua pamoja na watu wengine watano.
Hii ni baada ya kutengana na mkewe huyo, Regina Mavondo Kamari mwaka 2020 kwa kile alichoeleza Yakobo katika utetezi wake kuwa mkewe huyo alikuwa hazai, hivyo aliamua kuachana naye ili aweze kuoa mwanamke mwingine anayezaa.
Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam chini ya Jaji Butamo Phillip, imemuhukumu Yakobo kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuchoma nyumba hiyo na kusababisha vifo vya wanafamilia sita akiwamo mkewe huyo wa zamani.
Waliouawa katika tukio hilo baya la nyumba kuchomwa moto lililotokea usiku wa Februari 8, 2020 kijiji cha Uponda Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani ni Kamari, Agnes Brash, Regina Ng’oda, Frida Mario, Nuru Kipengee na Maimuna Brash.
Miongoni mwa waliouawa ni watu wazima wanne na watoto wawili huku upande wa mashitaka ukiegemea ushahidi wa mashahidi watano na vielelezo saba yakiwamo maelezo ya onyo ya mshtakiwa, ambayo alikiri kuhusika na mauaji hayo.
Katika hukumu yake aliyoitoa Aprili 29, 2025 kisha kuwekwa mtandaoni usiku wa Aprili 30, 2025, Jaji Phillip alisema ingawa hakuna shahidi aliyeshuhudia mshtakiwa akilipua nyumba hiyo, ushahidi wa mazingira umethibitisha ni yeye.
Ushahidi wa Jamhuri ulivyokuwa
Shahidi wa kwanza, Saimon Kabisera ambaye ni mtoto wa Regina Kamari, aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa ni baba yake wa kambo na mama yake alimweleza kuwa aliachana naye mwaka 2020.
Alieleza kuwa Februari 8, 2020, majirani walimpigia simu na kumjulisha kuwa nyumba ya mama yake imechomwa moto, alienda eneo la tukio na polisi walipofika pamoja na daktari, waliingia wote ndani ya nyumba iliyoungua.
Shahidi huyo aliweza kuwatambua marehemu ambao walikuwa wameunguzwa na moto na kufa kutokana na wajihi wao kwa sababu alifahamu nani na nani walilala katika nyumba hiyo, kwani jana yake usiku alikuwa amemtembelea mama yake.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni pamoja na mama yake mzazi, Regina Kamari na watu wengine watano, wakiwamo watoto wadogo wawili na watu wazima watatu na kufanya idadi ya waliokufa kufikia sita.
Kulingana na ushahidi wake, siku moja kabla ya tukio hilo alikuwa amemtembelea mama yake ambaye alimweleza kuwa wametengana na baba yake wa kambo na hawaishi pamoja.
Hata hivyo, mama yake alimwambia kuwa mshtakiwa alikuwa amemwambia atamfanyia kitu kibaya ambacho hatakaa akisahau katika maisha yake, na usiku huo akamwacha mama yake akiwa na Agnes, Regina, Frida, Nuru na Maimuna.
Shahidi wa pili, Sadock Bandiko ambaye alikuwa ni daktari aliyefanya uchunguzi wa miili ya marehemu hao katika eneo la tukio, alisema alibaini kuwa chanzo cha vifo vyao ni kukosa hewa na maumivu mabaya ya moto.
Shahidi wa tatu, Zuwena Mawala ambaye anajishughulisha na uuzaji wa mafuta kwa kiwango kidogo, alieleza kuwa Februari 7,2020, mshtakiwa alifika eneo lake la biashara akiwa na bobo (dumu) la kununuliwa petroli lita tano.
Hata hivyo, hakuwa na kiasi hicho cha petroli kwani alikuwa amebakiwa na lita tatu tu, ambapo mshtakiwa aliyekuwa amevalia mgolole wa Kimasai alikubali kununua lita hizo tatu ambazo alimjazia katika bobo hilo la lita tano.
Shahidi huyo alipoulizwa kama anaweza kumtambua mshtakiwa huyo hapo mahakamani, alisema ndio na aliweza kumtambua akiwa kizimbani na kueleza kuwa hafahamu mshtakiwa alienda eneo gani baada ya kumuuzia petroli.
Askari Polisi Koplo Victor aliyekuwa shahidi wa nne, alisema yeye ni miongoni mwa watu waliofika eneo la tukio na baadaye alipata taarifa fiche kuwa mshtakiwa ameonekana katika kijiji cha Njopeka Wilaya ya Mkuranga.
Walikwenda hadi kijiji hicho baada ya msiri wao kuwaeleza alivyovaa na mwonekano wake na kufanikiwa kumkamata na katika mahojiano aliwaambia hawana haja ya kupoteza muda wao kwa kuwa yeye ndio amechoma nyumba.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, mshtakiwa aliahidi kuwapa ushirikiano ili ukweli wa tukio hilo uweze kujulikana na walirudi naye hadi kituo cha Polisi Kibiti, ambapo alipewa wajibu wa kuandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo.
Shahidi wa tano, Koplo Emmanuel alieleza namna yeye na maofisa wengine akiwamo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Kanuni walivyokwenda eneo la tukio na kushuhudia namna nyumba ilivyochomwa moto.
Aliieleza Mahakama kuwa Februari 9,2020, alimchukua mshtakiwa na kumpeleleka hadi eneo la biashara la shahidi wa tatu, ambapo shahidi huyo alimtambua mshtakiwa kuwa ndiye alikuwa amemuuzia lita tatu za petroli.
Kulingana na ushahidi wake, siku iliyofuata walimpeleka mshtakiwa kwa mlinzi wa amani kuandika maelezo yake na kukiri ndiye aliyeilipua nyumba ya Kamari.
Huu ndio utetezi wake
Katika utetezi wake, alieleza kuwa uhusiano wake na Regina Kamari ulianza mwaka 2014 wakati huo akiishi eneo la Buza Kanisani jijini Dar es Salaam na baadaye mwaka 2015 wakaamua kuishi kama mume na mke na marehemu huko kijiji cha Upondo.
Alieleza kuwa walitengana na mkewe mwaka 2019 kwa sababu alikuwa hazai na alimweleza kuwa alihitaji kuoa mwanamke mwingine atakayemzalia watoto, hivyo baada ya kuachana, yeye alirudi kuishi Buza jijini Dar es Salaam.
Siku ya tukio Februari 8,2020 alikuwa eneo la Kigando Jaribu akiuza vyombo vya kupikia ambayo ndio ilikuwa biashara yake na alikuwa hapo hadi saa 4:00 asubuhi, kwa lengo la kuendelea na biashara yake ya kuuza vyombo.
Baada ya kumaliza alichokuwa akikifanya, alianza kurudi Jaribu ambapo njiani alikutana na gari lililosheheni mihogo likiwa limeegeshwa pembeni halina mafuta, ambapo dereva alimuomba amsaidie kwenda kumnunulia petroli lita tano.
Pembeni ya barabara aliona watu wanauza mafuta ambapo alifanikiwa kununua lita tatu tu na hivyo kumrudishia dereva chenji ya Sh2,500 kutoka katika Sh10,000 aliyokuwa amempa, na kwamba alikamatwa akiwa kijiji cha Njopeka.
Alisema kuwa baada ya kukamatwa, alipelekwa kituo cha Polisi Kibiti ambako huko aliingizwa katika chumba alichodai ni cha wapelelezi ambao walimtesa na kumtaka akiri kumuua Regina Kamari na ili kujiokoa na kifo, ilibidi asaini maelezo hayo.
Hukumu ya Jaji
Katika hukumu yake, Jaji Phillip alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri amebaini kuwa hakuna shahidi hata mmoja aliyemshuhudia mshtakiwa akiichoma nyumba hiyo, bali ushahidi uliopo ni wa mazingira.
Hata hivyo, Jaji alisema mnyororo wa matukio waliyoyaeleza mashahidi wa Jamhuri unamuunganisha moja kwa moja mshtakiwa na tukio hilo, licha ya kwamba hakuna shahidi hata mmoja aliyemshuhudia akiichoma nyumba.
Akitolea mfano, Jaji alisema shahidi wa tatu alimtambua mshtakiwa kuwa ndiye aliyenunua petroli kutoka kwake Februari 7,2020 na asubuhi ya siku iliyofuata akapata taarifa kuna nyumba imechomwa moto kijiji cha Uponda.
“Mshtakiwa mwenyewe naye alikiri kuwa siku hiyo alinunua petroli kutoka kwa shahidi huyo wa tatu ingawa alijitetea kuwa haikuwa yake bali alitumwa kumnunulia mtu mwingine,”alisema Jaji.
Hata hivyo, Jaji alisema kwa umakini mkubwa amezingatia utetezi huo na kujiridhisha kuwa aliamua kusema hivyo kwa lengo tu la kujinasua na tuhuma zilizokuwa zinamkabili na wala haiwezi kuwa ni tukio lililoingiliana.
“Kwamba mshtakiwa anaombwa akanunue petroli kwa ajili ya mtu mwingine halafu siku inayofuata nyumba ya mke wake wa zamani inachomwa moto. Mnyororo huu wa matukio unaoana na kile mshtakiwa alichokieleza.”
“Ukiacha maelezo hayo ya kukiri kutenda kosa kuna ushahidi wa shahidi wa kwanza kwamba mshtakiwa aliahidi kumfanyia kitu kibaya marehemu ambacho hatakaa akisahau. Kiukweli utetezi wake haujaibua mashaka yoyote ushahidi wa Jamhuri,” alisema.
Ni kutokana na ushahidi huo wa mazingira, Jaji alisema Mahakama inaona upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka hilo pasipokuacha mashaka yoyote kwamba mshtakiwa ndiye aliyesababisha vifo vya marehemu hao sita.
Jaji alisema kifungu cha 200 cha Kanuni ya Adhabu kinaeleza kuwa na nia ovu kunafananaje, na kwamba mtu anayechoma nyumba anakuwa na dhamira ovu ya kutenda kosa hilo kama ambavyo mshtakiwa alifanya kwenye nyumba ya mkewe.
Katika kesi hiyo, Jaji alisema mshtakiwa alidhamiria kutenda kosa hilo na kusababisha majeraha mabaya kwa mke wake wa zamani na wanafamilia, hivyo kwa kosa hilo la kusababisha vifo vya watu hao anahukumiwa adhabu ya kifo.