Mwanza. Wataalamu wa afya, lishe na mazingira wametaja ulaji wa chakula kinachofaa, kudhibiti msongo wa mawazo, kufanya uchunguzi wa afya ya mwili mara kwa mara, mazoezi na kutunza mazingira, ni miongoni mwa siri za mtu kuishi maisha marefu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Makadirio ya Taifa ya Idadi ya Watu nchini iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), makadirio yaa ukomo wa umri wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka kutoka miaka 67 na miezi mitatu mwaka 2022 hadi kufikia miaka 74 ifikapo 2035.
Hilo ni ongezeko la miaka saba na miezi miwili ndani ya miaka 12 ijayo kwa mujibu wa makadirio hayo.
Hata hivyo, umri mrefu unaandaliwa kwa kuzingatia masuala mbalimbali ya kiafya, kiakili, lishe na kimazingira, kama wanavyopendekeza wataalamu.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wataalamu hao wamesema iwapo vitu hivyo vitazingatiwa, watu wataishi maisha marefu kwakuwa wataondokana na maradhi yakiwemo yanayosababishwa na ulaji usiofaa, kutofanya mazoezi na uharibifu wa mazingira.
Ulaji unaofaa
Kwa mujibu wa kitabu cha mtindo wa maisha na magonjwa yasiyoambukiza kilichochapishwa na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), ili kuwa na afya bora mtu anatakiwa kula chakula cha kutosha kwa mahitaji ya mwili, kwa ajili ya makuzi na maendeleo yake na kuwa na uzito wa kawaida kulingana na umri na urefu.
Kinaeleza kuwa ulaji unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko, chenye virutubishi vyote kwa uwiano ikiwemo kula matunda yaliyopo kwenye msimu aina mbili kwa siku na kula mboga mboga kwa milo miwili kwa siku, huku tahadhari ikitolewa kwenye matumizi ya mafuta mengi.
“Sukari isizidi vijiko vitano vya chai kwa siku na chumvi isizidi kijiko kimoja cha chai kwa siku na usinywe pombe kupita kiasi. Chakula mchanganyiko hukuwezesha kupata virutubishi vyote vinavyohitajika mwilini. Kwa mfano, vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto, protini husaidia kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali, vitamini na madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa,”kinaeleza kitabu hicho.

Kinaongeza:”Kila siku jitahidi kula vyakula kutoka kila mojawapo ya makundi ya chakula ambayo ni vyakula vya wanga (nafaka, ndizi za kupika, mahindi, mtama, ngano, ulezi, mchele, uwele, mihogo, viazi vya aina zote, maghimbi) vyakula vya protini (jamii ya mikunde na asili ya wanyama), mbogamboga na matunda ili kupata virutubishi vyote.”
Kitabu hicho kinaelezea vyakula hivyo ni chanzo cha vitamini na madini ambavyo huupatia mwili kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na kuupatia makapi-mlo au nyuzi nyuzi ambazo humfanya mtu ajisikie kushiba na kupunguza kiasi cha chakula anachokula na hivyo kupunguza uwezekano wa kuwa na uzito uliozidi.
“Maji hayahesabiwi kama kundi la chakula lakini ni muhimu kwa kurekebisha joto la mwili na kuondoa mabaki au uchafu mwilini kwa njia ya jasho na mkojo, ambapo kitaalamu mtu anatakiwa atumie maji lita moja na nusu kwa siku…Mwili unahitaji nguvu na nishati, hivyo ni vizuri kula milo kamili mara tatu kwa siku na vitafunwa (asusa) mara mbili kwa siku kati ya kifungua kinywa na chakula cha mchana na kati ya chakula cha mchana na cha jioni,”kinaeleza.
Ofisa lishe wa Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mwamini Mziray anasema ili mtu aweze kuishi muda mrefu, anatakiwa kujali mtindo huo wa ulaji bora kwa sababu kama hatokula vizuri, kinga ya mwili itashuka au kupungua na hivyo kupata magonjwa.
“Muhimu kuzingatia lishe yake kuhakikisha kinga ya mwili inanyanyuka, kula mboga za majani na matunda inamsaidia kuimarisha kinga ya mwili. Akila vizuri kunamwepusha asiweze kupata magonjwa ya kuambukiza yanatotokana na ongezeko la uzito. Kwa wanawake wapewe muda wa kutosha wanapotoka kujifungua, wale vizuri kwakuwa muda huo wanakuwa wanarejesha afya yako,”anasema.
Mtaalamu huyo anashauri watu kuepuka vyakula vilivyokaangwa au kupikwa kwa mafuta mengi, badala yake vichemshwe, kuokwa au kuchomwa.
Punguza mafuta kwenye nyama iliyonona ikibidi ngozi ya kuku hasa wa kisasa iondolewe kabla ya kupika, kula tunda zima badala ya juisi, matumizi ya unga wa nafaka zisizokobolewa, kutoongeza chumvi ya ziada mezani wakati wa kula na kupunguza sukari, ni miongoni mwa vitu vinavyochangia kuongeza maisha marefu.
Mazoezi, uchunguzi wa afya
Daktari wa magonjwa ya binadamu Hospitali ya Nzega Mji, Dk Sarah Boniphace, anasema kufanya mazoezi zaidi ya nusu saa angalau mara nne kwa wiki, kunasaidia kupunguza uzito, kinga ya magonjwa ambayo yamekuwa yakifupisha maisha ya watu wengi
Miongoni mwa faida za mazoezi ni kudhibiti unene, sukari na mafuta yaliyozidi mwilini na kuepusha shinikizo kubwa la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani, kujenga misuli ambayo husaidia kutumia nishati ya ziada na hivyo kuepuka unene.
Faida nyingine ni kupunguza msongo wa mawazo na uchovu, kuwezesha usingizi mnono, kuongeza kinga ya mwili, kuimarisha hisia na kuongeza ufanisi wa akili.
“Pia kupunguza msongo wa mawazo kwa sababu unaweza kusababisha kupunguza kinga ya mwili na inapopungua, inasababisha kunyemelewa na magonjwa mara kwa mara yanayoweza kuchangia kupunguza umri wa kuishi,”anasema Dk Sarah.

Anasema kufanya uchunguzi wa mara kwa mara japo mara mbili au tatu kwa mwaka, kunasaidia kugundua magonjwa kwa haraka kama yapo na kupata tiba mapema, akitolea mfano maradhi ya saratani hasa ya shingo ya kizazi ambayo inashauriwa kupimwa japo mara moja ndani ya miaka mitatu.
“Kutolala kiasi cha kutosha huongeza uwezekano wa kupata magojwa kama vile kisukari, shinikizo la damu, unene na sonona na udhibiti wa hayo magonjwa unakuwa mgumu zaidi,”wanaeleza wataalamu.
Kutunza mazingira
Ofisa Mazingira Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene pamoja na kuzingatia kanuni za afya, kingine kinachoweza kuchangia mtu kuishi maisha marefu, ni kuishi kwenye mazingira safi na salama.
“Ni lazima uhakikishe unaishi kwenye mazingira safi na salama, unakuwa na miti mingi inayoleta hewa nzuri ya oksijeni kwa kuzingatia upandaji miti wa kutosha,”anasema.
Anasema pia ni muhimu kupunguza matumizi ya vitu vinavyosababisha uchafuzi wa hewa, ikiwemo matumizi ya mkaa na kuni yanayosababisha moshi ambao unaweza kuchangia magonjwa ya kupumua na matatizo ya moyo.
“Kupumua hewa safi kuna faida kubwa kwa afya ya mapafu na mfumo wa moyo, lazima upate hewa ya asili inayopatikana baada ya miti kupandwa na pia tunatakiwa kutumia usafiri wa umma kupunguza hewa ukaa inayotokana na moshi wa magari au tungeweza kutumia hata baiskeli kama usafiri…ukienda kwa wenzetu wanatumia sana baiskeli au magari ya umeme ili kupunguza hewa ukaa,”anaeleza.
Anasema hata sehemu za utalii wa mazingira zikiwemo fukwe, bustani, kutembelea maliasili za misitu, wanyama na vivutio vingine, ni sehemu ya mazingira ya kujifurahisha na kupumzisha akili, yanayochangia kupunguza msongo wa mawazo ambao ukizidi unahatarisha maisha.