Siri wasanii wengi kutokea Mbeya

Dar es Salaam. Mkoa wa Mbeya umekuwa ukisifika kwa vingi hasa uzalishaji wa mazao kama mchele, maharage na viazi. Lakini hivi sasa unaonekana kuvuka mipaka kwani una mchango mkubwa katika kiwanda cha burudani nchini hasa kwa kuzalisha wachekeshaji wengi. Soma zaidi.

Eliud Samweli (Sukari)

Huyu ni mchekeshaji kutoka Mbeya aliyeibuliwa kwa mara ya kwanza na jukwaa la vichekesho ‘Cheka Tu’.Tangu kuja kwake Dar es Salaam, mchekeshaji huyo amekuwa akitumia lafudhi ya Kinyakyusa katika ucheshi wake jambo linalofanya aendelee kujizolea mashabiki kila kukicha.

Ubunifu na kuibeba asili ya Mbeya pia umegeuka sababu ya Eliud kupata ‘mashavu’ mbalimbali kama lile la kuigiza kwenye tamthilia ya Jua Kali. Na sasa anatambulika kama Mchekeshaji Bora wa Jukwaani  hii ni baada ya kushinda tuzo za wachekeshaji zilizotolewa Februari 22,2025.

Ulimboka Mwalulesa (Senga)
 Huyu ni mwigizaji mkongwe wa vichekesho ambaye naye chimbuko lake ni Mbeya. Mkali huyu hajaanza leo wala jana kuchekesha. Ni mkongwe katika fani tangu enzi zile za kina Mzee Majuto.

Amezipa nyuso nyingi tabasamu na furaha kwa ucheshi wake huku baadhi ya wachekeshaji ambao alianza nao ni marehemu Pemba ambaye alijizolea umaarufu kwa kutembea na rugu begani wakati wote.

Oscar Mwanyanje (Mc Mboneke)

Huyu naye ni kati ya wachekeshaji kutoka Mbeya ambao wanaendelea kuwavunja mbavu mashabiki kutokana na vituko vyake. Utakumbuka Mboneke alianza kufahamika baada ya kutengeneza maudhui ya mtandaoni yaliyokuwa yakimuonesha akikimbia huku akiongea kwa kutumia neno lake “Kama vipi irudiwe”.

Baada ya video yake kufanya vizuri na kupendwa na wengi ilimfanya mchekeshaji huyo ahamie jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendeleza kipaji chake na hadi sasa anawakilisha wachekeshaji wa Mbeya.

Mchekeshaji huyu kutoka Mbeya awali alianzia katika jukwaa la Cheka Tu ambalo limetambulisha wachekeshaji wengi kwenye kiwanda cha burudani. Licha ya kuwa msanii huyu kwa sasa yupo kwenye kundi la Watubaki. Bado anaendelea kufanya vizuri na kuufanya mkoa wa Mbeya kumhesabu kama mmoja wa  wachekeshaji wake.

Hakika Mwapongo (Mwaisa)

Naye ni mchekeshaji ambaye amekuwa akijizolea umaarufu kwa kutumia video fupi mbalimbali za wanyama hasa nyani akiziingizia sauti kwa kutumia lafudhi ya Kinyakyusa.
Kutokana na matumizi ya lafudhi hiyo ameendelea kufanya ajizolee umaarufu na kujinyakulia mashabiki wapya kila kukicha.

Matumaini Marthin
 

Linapotajwa jina la Kiwewe wengi wanamalizia kwa  jina la mchekeshaji kutoka Mbeya Matumaini ambaye ni sababu ya baadhi ya wachekeshaji wengi wa kike kuingia kwenye soko la uchekeshaji.

Akionekana kwenye michezo ya runinga Matumaini hakuficha lafudhi ya Kinyakyusa na kuitumia kama utambulisho wake uliowavutia wengi. Naye anasimama kama kitambulisho cha wachekeshaji kutoka Mbeya. 

Erick Kinyambe

Marehemu Kinyambe naye alikuwa anatokea  Mbeya aliwavutia wengi kutokana na uwezo wake wa kuchekesha kwa kugeuza macho na sauti aliyokuwa akiitumia

Licha ya kufariki mwaka 2016, katika Hospital ya Rufaa ya Mbeya mchekeshaji huyu jina lake halijawahi kufutika katika orodha ya wasanii kutoka Mbeya wanaoitikisa tasnia.

Kutokana na wasanii wengi wa vichekesho kuonekana wanatokea Mbeya. Akizungumza na Mwananchi Mwaisa amesema siri ya mafanikio yao ni malezi katika ngazi ya familia.

“Kitu cha kwanza ni asili yetu ya kuishi kwa ucheshi, kwenye upande huo hata kama mtu siyo mchekeshaji lakini ukikaa naye lazima ucheke. Hata Rayvanny ukikaa naye lazima tu ucheke. Ni utamaduni wetu suala la utani lipo sana tangu katika ngazi ya familia.

“Mfano mimi mama yangu ni mcheshi kuliko hata mimi na kaka yangu, babu yangu wao pia. Kwenye ucheshi watu wa Mbeya ni kawaida. Pia upande wa wasanii wa nyimbo za injili.  Watu wengi wanakulia katika imani. Ndiyo maana kila baada ya nyumba kadhaa kuna kanisa  watoto wanakuwa wanaona hivyo ndiyo maana hata waimbaji ni wengi,”amesema Mwaisa.

Naye Kipotoshi akifichua siri ya wachekeshaji wengi kutokea Mbeya amesema  uhalisia wa maisha yao ndiyo chanzo.

“Sisi kiasili tunaishi uhalisia sana. Ni watu wazuri, hichi ndiyo kitu ambacho kinafanya tuonekane kama tunachekesha. Na maisha halisi ndiyo sababu watu wanacheka,”alisema Kipotoshi.Hata hivyo, kwa upande wake mchekeshaji Matumaini amesema kitu kinachowavutia watu wengi kwa waigizaji wa Mbeya ni lafudhi yao.
 

“Kitu ambacho kimekuwa kikiwavutia wengi ni uhusika ambao tunakuwa tunavaa watu wa Mbeya. Wengi ukiwaangalia lafudhi yetu hatujaitoa, tunapenda kuitumia,  tunapokuja kwenye suala la  vichekesho tunacheza uhalisia wa nyumbani. Hiyo inafanya kuwavutia watu,”alisema

Utakumbuka siyo hao tu hata mchekeshaji Konkala naye anatokea Mbeya. Pia Mbeya imetoa mastaa wengine kama Sugu, Izzo Bizness,  Queen Rocka, Gachi B , Rayvanny, Baddest 47, Amber Lulu na S2kizzy, Bon Mwaitege, na wengine wengi .