Siri mauzo ya korosho ya Tanzania kupaa masoko ya nje

Dar es Salaam. Uongezaji wa thamani na kuongezeka kwa korosho zinazozalishwa kumetajwa kuwa sababu ya kupaa kwa mauzo ya zao hilo katika masoko ya nje.

Mauzo ya korosho yalifikia Sh1.544 trilioni katika mwaka ulioishia Januari mwaka huu, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh585.77 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia, kwa mujibu wa ripoti ya hali ya uchumi ya kila mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Februari mwaka huu.

Mauzo yanafikia hapo wakati uzalishaji ukifikia tani 500,000 katika msimu wa mwaka 2024/2025 kutoka tani 240,158 zilizokuwapo mwaka 2022.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Machi 24, 2025, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wiki moja ya wataalamu wa sekta ya korosho 75 kutoka nchi tisa za Afrika, ili kuboresha utendaji wao na namna wanavyoweza kuongeza ufanisi katika mnyororo mzima wa zao hilo.

Washiriki hao wametoka katika nchi za Burundi, Kenya, Malawi, Tanzania, Msumbiji, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda na Zambia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Rashid Tamatamah, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (TCB), amesema kuuza nje korosho iliyoongezwa thamani ndiyo sababu ya kupaa kwa mauzo hayo, tofauti na awali ilipokuwa ikipelekwa ghafi.

“Lakini katika eneo hili bado hatujafanya vizuri pia, kwani katika ile korosho tuliyozalisha tani 500,000, ni asilimia 10 pekee ndiyo iliongezewa thamani. Kwa sasa, kuna mikakati ya kuhakikisha tunaongeza thamani ya korosho yetu yote,” amesema.

Amesema kwa kutambua faida ya uongezaji thamani, Serikali iliweka lengo la kuhakikisha korosho yote inaongezwa thamani hapa nchini kwa kutenga eneo kwa ajili ya kujenga kongani ya viwanda mkoani Mtwara likiwa na ekari 1,518.

Kati ya ekari hizo, 354 ziko katika uendelezaji, ikijumuisha maghala mawili ambayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 kila moja.

“Lengo ni kuhakikisha asilimia 100 ya korosho inayozalishwa nchini inabanguliwa kabla ya kupelekwa katika masoko ya nje,” amesema Tamatamah.

Hili linafanyika wakati ambapo pia Serikali imeweka wazi matarajio yake ya kuzalisha tani 700,000 katika msimu wa mwaka 2025/2026 na kufikia tani milioni moja mwaka 2030/31.

Matarajio hayo yanawekwa wakati ambao ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania inaonyesha kuwa mauzo ya korosho yameendelea kuimarika mwaka hadi mwaka kutoka Sh478.81 bilioni mwaka 2022, Sh563.01 bilioni mwaka 2023, Sh585.77 bilioni mwaka 2024, huku yakitarajiwa kuongezeka hadi kufikia Sh1.63 trilioni mwaka 2025.

Katika kuongeza ushiriki wa wakulima, Tamatamah amesema wamekuwa wakiwaweka karibu na bodi kwa kuhakikisha uwakilishi wao unapewa kipaumbele ndani ya bodi.

“Pia, mwaka uliopita, vijana 500 walipewa mafunzo ya kilimo cha korosho na kupelekwa vijijini ili waweze kusaidia wakulima pale inapohitajika, na hii itasaidia kuongeza uzalishaji,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa African Cashew Alliance (ACA), Ernest Mintah, amesema uzalishaji wa korosho ghafi kwa Afrika umeongezeka takribani mara mbili kutoka asilimia 30 mwaka 2006 hadi takribani asilimia 60 sasa.

Ukuaji huo umesukumwa na ongezeko la uzalishaji katika ukanda wa Afrika Magharibi, hasa nchi ya Ivory Coast, huku Afrika Mashariki ikionyesha ukuaji mkubwa zaidi kwa upande wa Tanzania.

“Licha ya ukuaji mkubwa wa uzalishaji wa korosho ghafi barani Afrika, ni huzuni kuona kuwa tunayoiongezea thamani ni chini ya asilimia 20 ya uzalishaji wote barani Afrika, hali inayosababisha sehemu kubwa ya shughuli hii kufanyika kwenye nchi kama Vietnam na India, hivyo kupoteza ajira,” amesema Mintah.

Mintah amesema ili kuimarisha uzalishaji na kuharakisha usindikaji wa korosho ghafi barani Afrika, uwekezaji katika mafunzo ya kina na ufanisi mkubwa unahitajika kwa wafanyakazi.

Akizungumzia mafunzo yanayotolewa kwa wataalamu wa sekta hiyo, Profesa Edda Lwoga, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa sababu kilimo cha leo si tu kupanda mazao na kuvuna, bali kimekuwa sekta yenye mabadiliko makubwa.

“Sekta hii sasa inahitaji ujuzi mpya, mbinu za ubunifu na ushirikiano madhubuti kati ya wakulima, wasindikaji na wadau wote wanaohusika katika minyororo ya thamani,” amesema Profesa Lwoga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *