CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinatathmini uendeshaji wa viwanja vyake vya michezo ili kuangalia uwezekano wa kuuboresha na ikiwezekana kwa kushirikiana na wawekezaji watakaokuwa tayari kufikia makubaliano nao.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Amosi Makala alisema hayo wakati alipozungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki na gharama za uendeshaji na mfumo wa malipo uliowekwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinakuwa ni kubwa kulinganisha na kile kinachopatikana milangoni.
Kwa kawaida viwanja huchukua kuanzia asilimia 15 ya mapato ya mlangoni ya mechi za Ligi za soka, lakini ni mechi chache zinazoweza kuingiza mapato ya kutosheleza mmiliki wa uwanja kulipia gharama za masuala mbalimbali ya uendeshaji.
Matokeo yake huandikwa madeni ambayo hugeuka chechefu, huku viwanja vikikosa huduma muhimu za matengenezo na ukarabati hadi wamiliki waingilie kati na kugharimia. Hii imesababisha Bodi ya Ligi (TPLB) kufungia baadhi ya viwanja mara kwa mara na hivyo kusababisha usumbufu kwa timu zinazotumia viwanja vya CCM kama makao yake makuu.

CCM inamiliki viwanja vya michezo vya hadhi ya Olimpiki karibu kila mkoa wa Tanzania Bara, hasa ile ya zamani. CCM ilijenga viwanja hivyo wakati nchi ikiwa kwenye mfumo wa chama kimoja na ilitumia nguvu za wananchi kuvijenga.
Serikali za Mikoa zilihamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa viwanja hivyo kwa njia tofauti, kama kushiriki katika ujenzi, kulipia bidhaa muhimu kama petroli kwa bei ya ziada na mambo mengine, jambo lililosababisha kelele wakati nchi ikihamia kwenye mfumo wa vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya 90.
Vyama vya upinzani vilidai viwanja hivyo ni mali ya wananchi kwa sababu walishiriki kwa njia mbalimbali kuvijenga, hivyo CCM haina budi kuvirejesha serikalini ili vimilikiwe na wananchi wote bila ya kujali itikadi za vyama.
Hata hivyo, CCM imeendelea kuvishikilia na kuvitumia kwa shughuli zake za kisiasa, huku vyama vya michezo vikiruhusiwa kuvitumia katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Kumekuwepo na wazo viwanja hivyo virudishwe kwa serikali na serikali iunde ofisi ya wakala wa viwanja vya michezo ili ivisimamie kwa ufanisi zaidi tofauti na sasa. Katika siku za karibuni, serikali ilivifanyia ukarabati baadhi ya viwanja na hivyo kuamsha tena kelele za wananchi waliohoji sababu za serikali kutumia kodi za wananchi kukarabati viwanja vya chama cha siasa.
Kwa hiyo, kauli hiyo inaweza kuwa imekuja wakati sahihi kwa mashabiki wa michezo, hasa wa soka ambao hutumia viwanja hivyo karibu kila wiki kutokana na TFF na vyama vya mikoa kuwa na mashindano tofauti kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa.
Mahitaji ya mashirikisho ya kimataifa ya soka kuhusu viwango na ubora wa viwanja vinavyotumiwa kwa ajili ya mashindano yake yanazidi kukua. Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limekuwa likizuia nchi kadhaa kutumia viwanja vyake kwa mashindano kama ya Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho na michuano ya awali ya Mataifa ya Afrika.

Hii imesababisha Tanzania kutumika kama uwanja wa nyumbani wa mataifa kadhaa ambayo viwanja vyake havijafikia viwango vya CAF. Ubora wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao unamilikiwa na serikali, umevutia nchi nyingi kuamua kuutumia kwa mechi zao za nyumbani.
Ubora huo wa Uwanja wa Mkapa ndio unaotakiwa—basi angalau nusu yake—kwenye viwanja vingine vilivyosambaa karibu kila mkoa. Lakini hadi serikali kuweza kuulinda ubora wa Uwanja wa Mkapa, maana yake zimetumika bilioni nyingi kwa ukarabati na matengenezo mengine kadhaa, hali ambayo inaiweka CCM katika mazingira magumu kuweza kukarabati viwanja vyake ili vifikie hata robo ya viwango vya Uwanja wa Mkapa.
Viwanja vingi, kama sio vyote, vya CCM vina nyasi za kawaida ambazo ni ngumu kuzitunza kama hakujawekwa nguvu kubwa. Vingi vimejaa au kuzungukwa na maduka au ofisi na hivyo kuwa na maeneo machache kwa ajili ya huduma za kimichezo kama vyumba vya kutosha vya kubadilishia nguo na vyumba vya kutosha kwa ajili ya mikutano na waandishi wa habari.

Pia uwepo wa vyumba kwa ajili ya vipimo vya dawa za kusisimua misuli, mfumo mzuri wa mawasiliano na watazamaji kwa ajili ya dharura na matangazo mengine, mifumo mizuri ya tahadhari kwa ajili ya usalama wa watu wanaoingia viwanjani, n ahata mifumo mizuri ya uingiaji viwanjani.
Sehemu ya kuchezea, hasa mpira wa miguu ndio tatizo jingine kubwa kutokana na aina za nyasi zinazotumiwa na hali kadhalika matunzo.
Yote hayo yanahitaji chombo madhubuti au mmiliki mwenye uwezo wa kifedha, mbunifu na mwenye watu wenye taaluma ya kuvisimamia na kuviendesha. Si kwamba CCM haiwezi kuwa na vitu hivyo, lakini usimamizi na uendeshaji wake umeshakuwa changamoto na hivyo ni jambo sahihi ni itathmini suala hilo na ikiwezekana watafutwe wawekezaji wa kuvisimamia na kuviendesha kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Mchezo kama mpira wa miguu unazidi kuwa biashara yenye faida kubwa na hivyo unahitaji mazingira mazuri ya kucheza ili uvutie zaidi wagtu na wawekezaji waone thamani na kutumbukiza zaidi fedha ambazo zitaweza kusaidia kulipia gharama za uendeshaji.
Viwanja kama Camp Noun na Santiago Bernabeu sasa vinatumika kibiashara zaidi, tofauti na hapo mwanzo vilipokuwa vikitumika kwa ajili ya michezo. Real Madrid wamefikia kuondoa hata neno Santiago na kubakiza ‘Bernabeu’ peke yake kwa sababu za kibiashara, huku ikiufanyia uwanja huo marekebisho makubwa yanaoufanya uwe mmoja wa viwanja vya kisasa zaidi duniani.

Barcelona wameingia mkataba na Sportify ambao unaongeza matumizi ya Uwanja wa Camp Nou kutoka yale ya kawaida ya michezo pekee. Matamasha ya muziki, sherehe za harusi na masuala mengine ya burudani, sasa yanaweza kufanyika vizuri zaidi kwenye uwanja huo.
Huu ni ubunifu unaiotakiwa kwa wamiliki wa viwanja. Na ili kuwe na ufanisi kunahitajika chombo maalum kwa ajili ya kushughulikia viwanja tu. Na hilo likifanyika tutakuwa na Camp Nou na Bernabeu zetu hapa Tanzania.
Kunahitajika ujasiri kwa CCM kuliona hilo na kulichukulia hatua. Ujasiri wa kwanza ndio huo wa kutathmini na wa pili ni wa kuchukua hatua baada ya kuona tatizo liko wapi.