Ule mjadala wa kampuni moja kudhamini timu zaidi ya moja umeibuka tena, ukizungumzwa zaidi na baadhi ya wachambuzi, lakini mashabiki wa suala hilowa kijadili kwa ukubwa.
Kama kawaida mjadala huu huibuka wakati Yanga inapoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na klabu hiyo kudhaminiwa na kampuni ya GSM katika masuala ya jezi.
Mamlaka husika hazijawahi kutoa ufafanuzi kuhusu hilo; yaani si Shirikisho la Soka (TFF) au Bodi ya Ligi (TPLB) wala kampuni ya GSM yenyewe, ambayo kwa sasa inadhamini karibu klabu sita.
Wanaolizungumzia hilo ni wale mashabiki wa Simba wanaodai kuwa, Yanga huwa inajihakikishia pointi za timu hizo sita wakati Ligi Kuu inapoanza na hivyo kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kutetea ubingwa.
Cha ajabu hakuna kiongozi wa Simba anayetoa madai hayo, pengine ni kwa kujua kinachozungumzwa hakiendani na masuala ya udhamini yalivyo katika soka duniani.

Coastal Union
Wengi wanauliza ni nchi gani duniani ambayo mdhamini mmoja hujihusisha na zaidi ya klabu mbili, lakini hakuna anayesema kama kuna sheria au kanuni katika nchi fulani inayozuia kampuni moja kudhamini klabu zaidi ya moja.
Wanapotoa mifano wanatoa ile ya Leseni za Klabu inayozuia mtu au taasisi kumiliki klabu zaidi ya moja zilizo katika daraja moja au shindano moja na si udhamini.
Hivyo suala hilo limekuwa likiachwa lijiibue na kujifia pale mambo yanapokwenda sawa.
Lakini nadhani kuliacha hilo lijiendeshe, kwa maana ya kuibuka na kupotea, si jambo sahihi. Ni muhimu sana kwa taasisi zinazohusika na uendeshaji na usimamizi wa soka zijitokeze na kuzungumzia suala hilo kwa mapana na marefu ili mashabiki, na hata wachambuzi walielewe na kulizungumzia vizuri katika vyombo vya habari.

Kazi za Idara za mahusiano na habari kwenye taasisi ni pamoja na kutoa ufafanuzi wa masuala tata ama kwa kupendekeza kwa viongozi wao wajitokeze kulizungumzia au kuita wataalamu wa masuala ya masoko na udhamini waeleze kama kuna sheria zozote zinazoruhusu au kuzuia kampuni moja kudhamini zaidi ya klabu moja kwenye shindano moja.
Kazi za idara hizo za habari na mawasiliano si kusubiri tukio litokee ndipo zitoe taarifa, bali pia ni kujenga taswira nzuri ya taasisi na shughuli kwa kutoa ufafanuzi wa masuala tata yanayoweza kuchafua mchezo au taasisi yenyewe.
Ninavyofahamu ni kwamba GSM si mdhamini mkuu wa Yanga na wala si mmiliki wa klabu hiyo yenye makao makuu katika makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani.

Singida Black Stars
Ndio maana GSM haweki nembo yake kifuani ambako klabu ziliachiwa kwa ajili ya mdhamini mkuu, kama ilivyo Simba kwa M-Bet. GSM ni mdhamini wa jezi, kama ilivyo kampuni ya Adidas kwa klabu kadhaa zinazoshiriki Ligi Kuu ya England, zikiwemo Arsenal, Chelsea na Manchester United.
Mbali na Yanga, timu nyingine zinazodhaminiwa na GSM ni Mashujaa Kigoma, Coastal Union (Tanga), Namungo (Lindi), Pamba Jiji (Mwanza) na Singida Big Stars. Kifuani mwa jezi za
Singida BS kuna nembo ya Sportspesa kama mdhamini mkuu, Namungo ipoa Azam Max, wakati kifuani mwa jezi za Coastal na Pamba yupo GSM. Mdhamini mkuu wa Mashujaa ni G-Boost.
Hivyo ni timu mbili tu, ambazo GSM ni mdhamini mkuu yaani Coastal na Pamba, huko kwingine ni mdhamini mwenza, akijihusisha zaidi na vifaa. Ndivyo ilivyo kwa Adidas, Umbro, Puma, Nike, Macron, Sudu na Castore ambazo ndio pekee zinadhamini timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu ya England.

Yaani Adidas anazidhamini Arsenal, Aston Villa, Manchester United, Newcastle United na Nottingham Forest, huku Umbro ikizidhamini Bournemouth, Brentford, Ipswich Town na West Ham United wakati Nike inazidhamini Brighton & Holves, Chelsea, Liverpool na Tottenham.
Puma inazidhamini Manchester City na Southmpton, wakati Macron ni wadhamini wa Crystal Palace na Sudu ni wadhamini wa Wolverhampton.
Kwa upande wa mdhamini mkuu kudhamini zaidi ya timu moja, hilo si jambo geni. Simba na Yanga walikuwa wakidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager na baadaye kuhamia kwa Sportspesa kabla ya Simba kumpata M-Bet na kuamua kuachana na Sportspesa. Hakuna sheria iliilazimisha Simba kuachana na SportPesaa zaidi ya masharti ya mkataba.
Kwingineko barani Ulaya, uwezekano wa kampuni moja kudhamini zaidi ya timu moja ni mdogo sana kutokana na uchumi wao kuwa mkubwa, hivyo ni rahisi kwa kampuni kuwa na ukiritimba katika klabu moja tu. Benki kama Standard Chartered inaidhamini Liverpool tu duniani kote.

Namungo
Hata hivyo, tofauti na huku, mdhamini mkuu wa Bayern Munich ni Allianz lakini logo yake imewekwa begani wakati ile ya kampuni ya simu ya T-Mobile imewekwa kifuani kutokana na makubaliano ya kimkataba.
Hivyo, mjadala huu wa udhamini wa GSM ungetumika kusaidia mamlaka kufikiri zaidi kuhusu udhamini na kikubwa kwanza zingejitokeza kuzungumzia sheria na kanuni zinasemaje kuhusu hali ya sasa na kama zimeona tatizo ambalo linaweza kurekebishwa.
Kilicho kikubwa ni kwamba mpira wetu bado unahitaji fedha zaidi na hivyo kunahitajika umakini mkubwa kushughulikia suala hilo kwa sababu kwa jicho fulani wanaolalamika wana hoja, lakini wakati huo huo fedha nazo ni muhimu kwa klabu husika.