SIO ZENGWE: Sakata la Yanga, Simba ni la kimfumo zaidi

Mara nyingi maamuzi ya kisiasa huwa ni ya kuangaliana usoni na si kuangalia suala la msingi linalotakiwa litafutiwe ufumbuzi.

Mara nyingi maamuzi ya kisiasa ama hutolewa kwa ajili ya kufurahisha pande zote, kuokoa hali inayoonekana kuwa mbaya hata kama mmoja ataumizwa na maamuzi hayo au kwa lengo la kufurahisha kikundi cha watu au genge la watu fulani.

Lakini uwezekano mkubwa ni maamuzi hayo kuwa na athari kubwa kwa kile kinachoshughulikiwa. Yaani kama ni kuwaondoa watu kwenye makazi ya asili, basi waathirika wakubwa wa maamuzi ya kisiasa watakuwa wananchi na kama ni huku kwenye mpira wa miguu, mchezo wenyewe ndiyo utaathirika sana.

Mwaka 1995 wakati mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Bara akiwa Safari Lager, utata ulizuka mwishoni mwa msimu wa matokeo ya timu kadhaa, zikiwemo zilizohusu maeneo ambayo wanatoka wanasiasa waliokuwa na nyadhifa.

Wakati huo timu za Ligi Kuu zilikuwa 12. Ili kufurahisha wanasiasa hao, iliamuliwa timu mbili zilizotakiwa zishuke daraja zisishuke, halafu timu nyingine mbili zilizofuzu kucheza Ligi Kuu ziongezwe ili ligi hiyo iwe na timu 14.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambayo ndio mzalishaji wa Safari Lager, haikupendezwa na uamuzi huo hivyo ikaamua kufuta udhamini wake kwa kuwa bajeti katika mkataba wa wakati huo ilihusu timu 12 tu na hivyo kuongeza ghafla timu mbili ilikuwa nje ya kampuni hiyo.

Wanasiasa hawakuumizwa kwa sababu lengo lao la kisiasa kuona timu kutoka maeneo yao zikicheza daraja la juu lilitimia, lakini hali ya uchumi kwenye klabu ikawa mbaya hadi kampuni ya mawasiliano ya Vodacom ilipokuja kuchukua ligi hiyo.

Wiki hii tumeshuhudia waendeshaji wa mchezo wa mpira wakifanya tena maamuzi yanayoumiza uchumi wa wadhamini, na hasa kampuni ya Azam Media ambayo imenunua matangazo ya kurusha moja kwa moja mechi za Ligi Kuu.

Ikiwa imeshatumia fedha zake nyingi kuitangaza mechi hiyo kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni, imeshaweka mkakati madhubuti wa kuongeza mauzo ya ving’amuzi vyake kwa kuweka timu mbalimbali za mauzo kwenye vituo tofauti, ikiwa imeshapeleka gari lake la kurushia matangazo uwanjani, ikiwa imeshasafirisha watangazaji wake na watumishi wake kwenda uwanjani, watu wanaojiita Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, inatangaza kuahirisha mechi bila ya kuzingatia mazingira yoyote yaliyowekwa kwenye kanuni.

Hakukuwepo na dharura yoyote, janga au hali mbaya ya hewa ambayo ingeweza kulazimisha mechi ya Ligi Kuu baina ya Simba na Yanga iahirishwe. Bali ilikuwepo barua ya Simba tu! Barua ambayo haikutumia kifungu chochote cha kanuni kufikia uamuzi wa kugomea mechi.

Haikutumia kifungu chochote wala sheria kuweka msimamo itacheza mechi hiyo baada ya waliohusika kuzuia timu yao ifanye mazoezi muda wa mechi, siku moja kwa kabla mechi kwenye uwanja utakaotumika, wachukuliwe hatua.

Kila ukisikiliza hali ilivyokuwa Machi 7 jioni wakati Simba ilipokwenda usiku kujaribu kufanya mazoezi ya mwisho, huwezi kuelewa ni sababu zipi ziliwafanya wafikie uamuzi wa kugomea mechi. Kwenda uwanja na mabasi matatu, walinzi wasingeweza kuwaruhusu; kwenda uwanjani nje ya muda wa mechi tarajiwa (yaani zaidi ya saa 1:00 usiku) wenyeji wasingeruhusu; kwenda uwanjani bila ya taarifa yoyote kwa msimamizi wa mechi hiyo, pia ingekuwa ngumu.

Kwa klabu ya kisasa, ni aibu kwa kiongozi kujitokeza hadharani kutetea mambo hayo. Yaani mengi yamegubikwa na imani za kishirikina.

Lakini Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji, bila ya kujali wadau wengine kama wadhamini na wamiliki wa haki za matangazo, ikaibuka na uamuzi wa kuridhisha upande mmoja.

Kwanza kwa kutangaza kuahirisha mechi, uamuzi ambao unailinda Simba kuchukuliwa hatua kubwa kama ile ya kushushwa daraja.

Hapa nina maana kwa kuwa kamati hiyo ilishatoa uamuzi wa kuahirisha mechi, Simba ana utetezi, hakwenda uwanjani kwa sababu mamlaka zilishaahirisha mechi.

Pia kwa kutangaza kuahirisha mechi bila ya mazingira yanayotajwa kikanuni yanalazimisha mechi kuahirishwa. Tatu kufanya uamuzi wa kuahirisha mechi hadi siku itakayopangwa ili iweze kutekeleza sharti la Simba la kushughulikia wahusika, kitu ambacho hakimo kwenye kanuni. Mechi huchezwa halafu wahusika kushughulikiwa baadaye.

Yote hayo yamefanywa bila ya kuzingatia wadau wengine kwenye mchezo huo ambao kwa utamaduni wa Tanzania ulipewa takriban siku sita kwa vigogo hao wa Kariakoo  kujiandaa, kitu ambacho ni tofauti kwa klabu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo hiyo.

Wengi wametumia kanuni kuonyesha makosa yaliyofanyika kwenye kushughulikia suala hilo, lakini tatizo halipo hapo. Tatizo lipo kwenye usimamizi wa ligi hiyo.

Hili nalirudia tena na tena ili kuwapa elimu viongozi wa klabu wajue Ligi Kuu ni yao na si ya TFF. Tulipounda Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) tulitaka klabu zijisimamie zenyewe katika maamuzi yote. Ilikuwa ngumu kuiacha Ligi Kuu, lakini hoja ya kuachana nayo ilikuwa nzito kuliko ya kuendelea kuishikilia.

Kwamba ukizipa klabu mamlaka ya kujisimamia unaziambia huku usimamizi wa haki utakuwa kwenu wenyewe. Hapa hakutakuwa na busara za kusema eti Simba na Yanga ni kubwa hivyo zipate muda wa kutosha kujiandaa kwa bechi baina yao kwa kuwa timu zote zinakuwa na haki sawa na jicho la usimamizi linawekwa ili kusiwepo na mbinu zozote za kuinufaisha timu yoyote.

Unapoweka nguvu ya usimamizi kwa klabu zenyewe, hakuna klabu ambayo eti itasusia au kutishia kujitoa kwa sababu itakuwa inapingana na maamuzi yake yewenye, kutokana na ukweli kwa njia moja au nyingine imeshiriki.

Hakutakuwa na chombo kitakachotolewa kafara au kuvishwa lawama au kupewa shinikizo kwamba kifanye mamuzi fulani la sivyo timu inajitoa. Kwa suala la mechi ya Machi 8, lipo Shirikisho la Soka (TFF) la kutupiwa lawama hizo, ipo TPLB ya kutupiwa lawama hizo na hata hiyo Kamati ya saa 72 ipo kutupiwa lawama hizo kwa sababu ni zao la TFF.

Leo, Azam Media wanatoa taarifa ya kusikitika kuhusu mambo yasiyo ya kistaarabu yaliyofanyika hadi mechi kuahirishwa bila ya kujali kiasi ambacho imewekeza, ni hali ya kusikitisha sana.

TPLB ingekuwa ni chombo cha klabu, mara moja mkutano mkuu ungeitishwa na sekretarieti ingeenda kujieleza ilikuwaje hadi sakata hilo likasababisha masilahi yao kiuchumi ‘kama ya mapato ya fedha za haki za matangazo, udhamini wa ligi, udhamini wao binafsi na masuala mengine’ ukawekwa rehani?

Lakini katika mazingira haya huwezi kuiwajibisha sekretarieti. Hili ni zao la TFF la kutaka kuendelea kubeba majukumu yasiyoihusu kabisa kwa kuwa haichangii lolote kwa klabu zaidi ya kuchota fedha za viingilio, udhamini na haki za matangazo.

Kwa wadau makini, TFF ingeitwa na kuulizwa. Je, mnataka kuturudisha kule ambako wadhamini waliamua kususia ligi kama ilivyokuwa mwaka 1995?

Katika jicho pana, si kuvunjwa kwa kanuni wala sheria, bali ni suala la kimfumo zaidi. Tunahitaji kuwaachia wenye klabu waongoze wenyewe Ligi Kuu ili wabanane katika maamuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *