Dar es Salaam. Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Yanga, Ally Kamwe ameitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kujieleza baada ya kutoa matamshi kuhusu kasoro za uamuzi ambazo sasa zimegeuka kuwa ndiyo maudhui ya vyombo vingi vya habari kila wakati mechi za raundi moja ya Ligi Kuu zinapoisha.
Hakuna raundi ya Ligi Kuu inayoisha bila ya matatizo ya uamuzi kujitokeza na kutawala mijadala ya vyombo vya habari badala ya kujikita kujadili ushindani wa mechi na ustadi wa wachezaji na mbinu za makocha.
Matatizo hayo ya uamuzi sasa yamekuwa tatizo pia kwa wadau wengine wa Ligi Kuu, hasa makocha, viongozi na watendaji katika ngazi ya klabu wanaokerwa na kasoro hizo kiasi kwamba uvumilivu unawashinda na kuamua kuzungumza waziwazi.
Wa kwanza katika siku za karibuni ni kocha wa Fountain Gate, Robert Matano ambaye amepigwa faini ya Sh500,000 kwa kuzungumzia uamuzi mbovu wa waamuzi katika mechi yao dhidi ya Simba wiki iliyopita.
Kocha huyo alikosoa uamuzi wa mechi hiyo akidai kuwa haukuwa mzuri kwa timu yake na kwa kiwango fulani maamuzi yaliiinufaisha Simba. Hajaitwa Kamati ya Maadili kuthibitisha tuhuma zake na moja kwa moja amepigwa faini ya fedha hizo.

Hivi sasa anga za soka zinasubiri uamuzi wa Kamati ya Maadili kuhusu kauli za Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe kuhusu tatizo hilohilo la uamuzi ambalo linarembwa kwa kupewa jina la “Makosa ya kibinadamu” bila ya wahusika kuchukua hatua za wazi kukabiliana nalo, hatua ambazo zingeweza kutisha waamuzi na kujirekebisha.
Kamwe, mmoja wa wasemaji wenye hoja na makini, alinukuliwa akitaka mamlaka za soka zifanye uchunguzi dhidi ya “makosa ya kibinadamu” yanayoendelea kutawala soka la Tanzania, akituhumu, makosa hayo yamekuwa yakiinufaisha klabu moja, hivyo kunahitajika uchunguzi kubaini tatizo.
Msemji huyo wa Yanga aliorodhesha hoja kadhaa zinazoonyesha kuna tatizo la uamuzi katika mechi za ligi na hivyo kutaka uchunguzi ufanyike ili kubaini tatizo. Lakini Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) imemshtaki kwamba kimaadili hatakiwi kuzungumzia kasoro za uamuzi wakati ana jukwaa la kuwasilisha maoni yake.

Hakuwa peke yake, bali pia Ofisa Habari wa Kagera Sugar, Hamisi Masanzara. Kamati ya Usimamizi wa Ligi imeeleza katika mashtaka yake kuwa viongozi na maofisa wa klabu wanazuiliwa kwa mujibu wa kanuni kutoa matamshi chonganishi au yanayoweza kuchafua taswira ya soka.
Ukiangalia mashtaka hayo na kile kilichoandikwa na Kamwe katika ukurasa wa Instagram, unajiuliza kama kweli alikuwa na nia hiyo ya kuchafua taswira ya soka au kulisafisha.
Mtu anayeomba mamlaka zifanye uchunguzi kubaini kweli wa tatizo linalozidi kuwa kubwa, anauchafua mchezo au anataka hatua zichukuliwe kuusafisha?

Labda kama tunataka kuwatisha wadau wa soka wasizungumzie matatizo yanayozidi kujitokeza katika uendeshaji na usimamizi wa mechi za mashindano makubwa.
Kama Bodi ya Ligi, iliyowashtaki hao wawili, inaona kuzungumzia kasoro za uamuzi wa mechi za Simba na Yanga ndiyo uhalifu pekee, basi ndio inakosea zaidi na ndio inayopaswa kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili.
Uamuzi mbovu umetapakaa katika mechi nyingi za Ligi Kuu na hata Ligi ya Championship, ambayo ni ligi ya pili kwa ukubwa nchini.

Ni vile tu wachambuzi na wadau wengine wanakodolea macho mechi za Simba na Yanga tu kutokana na kudhani ndizo zinazosababisha watazamwe sana na kufuatiliwa na wengi.
Lakini ukweli, kasoro hizo ni nyingi hata katika mechi zisizohusu klabu hizo mbili, haufichiki.
Ukisema uanze kuorodhesha, unaweza kujaza kurasa nyingi kuonyesha kuna tatizo kubwa katika uamuzi. Lakini Ally Kamwe anahisi huenda kukaa na tatizo kubwa zaidi nyuma ya uamuzi mbovu unaoitwa “makosa ya kibinadamu”.
Anasema kama ni uamuzi mbovu pekee, iweje uonekane kunufaisha klabu moja? Iweje penalti zenye utata ziwe za upande mmoja tu. Anaona cha muhimu ni kufanya uchunguzi kujua ukweli wa tatizo hilo.
Na uchunguzi unaweza kuja na majibu, kuna tatizo la tafsiri za sheria za soka, au kuna tatizo la utimamu wa waamuzi na hawawezi kwenda na kasi ya mchezo au ni kweli kuna njama zinazoinufaisha timu moja na hapo suluhisho likatafutwa kwa njia nzuri zaidi.
Ally Kamwe alikosea nini hapo kutaka uchunguzi ufanyike? Bodi ya Ligi au TFF wanaogopa kufanya uchunguzi wa matatizo yaliyokithiri ya uamuzi?

Kama tatizo limekithiri na ndiyo kiini cha mijadala kila raundi moja ya mechi inapoisha, viongozi washtuliwe kwa kutumia jukwaa gani? Kufuatwa kisirisiri ofisini na kuambiwa kuna tatizo?
Kama katika kila mechi, TFF inapeleka maofisa wake kwa ajili ya kusimamia mechi, kutathmini waamuzi na masuala mengine, imekuwaje taasisi ishindwe kutoa taarifa au ripoti ya kina kuhusu hiki kinachozungumzwa kila wiki kuhusu uamuzi mbovu?
Hawa maofisa wanaoenda kusimamia mechi na kutathmini waamuzi, wanaenda kufanya kazi gani hasa? Au ni njia ya kupooza machawa wenye ‘kamdomo?’
Badala ya kufikiria kumshtaki Ally Kamwe, Masanzara na wengine, ni muhimu Kamati ya Usimamizi wa Ligi na TFF wakaahirisha hayo yote na kujikita katika kile alichopendekeza Kamwe uchunguzi ufanyike na baada ya hapo ndipo irudi kwa Kamwe na majibu sahihi ya uamuzi mbovu unaoendelea nchini kama ni wa kusukwa au “ni makosa ya kibinadamu”.
Na kama ni makosa ya kibinadamu, basi mamlaka zitakuwa zimechelewa mno kuyashughulikia kwa sababu sasa ni zaidi ya miaka mitatu makosa hayo yanalalamikiwa na hatujawahi kusikia tamko lolote kutoka kwa viongozi wa juu wa shirikisho wakilaani kasoro hizo au kutangaza mikakati ya kulirekebisha.
Kinachotokea ni kuwaadhibu wanaolizungumzia tatizo hilo kwa ujasiri.
Inawezekana kuna ‘kamstari” ambako kanamtia hatiani Ally Kamwe kulingana na hizo kanuni zinazotumiwa na Kamati ya Uendeshaji wa Ligi, lakini katika mazingira kama haya ya kushamiri kwa makossa ya kibinadamu, nguvu ingeelekezwa katika uchunguzi anaouhitaji msemaji huyo wa Yanga.