
Mbeya. Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale, amelitaka Jeshi la Polisi kueleza iwapo linamshikilia mwanaharakati Mdude Nyagali na kutaja kosa wanalomtuhumu, pia amesimulia namna alivyokamatwa.
Kwa mujibu wa Mbeyale, baada ya kufika nyumbani kwa Mdude, majirani walieleza kuwa watu waliovunja mlango, kumshambulia kwa kipigo na baadaye kuondoka naye, walijitambulisha kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema hana taarifa ya tukio hilo na kuhitaji kupewa muda wa kulifuatilia na kufanya uchunguzi.
“Unajua mtu anaandika kwenye mitandao, sio rahisi kujibu haraka bila kufanya uchunguzi na inaposemwa Polisi wameenda ni polisi wa wapi? tunahitaji kupata ushirikiano wa taarifa sahihi,” amesema Kuzaga.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Mei 2, 2025, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale, amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kuomba apewe muda wa kulifuatilia kwa kina.
“Tunaendelea kufuatilia na baadaye kama Chama tutatoa tamko kuhusiana na tukio hilo,”amesema.
Simulizi ya kukamatwa Mdude
Kwa mujibu wa Mbeyale, baada ya kufika nyumbani kwa Mdude, majirani walidai kuwa watu waliovunja mlango, kumshambulia kwa kipigo na baadaye kuondoka naye, walijitambulisha kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi.
“Ukamataji wake haukufuata taratibu, kulikuwa na purukushani kubwa na damu ilimwagika. Zaidi ya hayo, hawakutoa taarifa yoyote kwa viongozi wa serikali ya mtaa ambako alikuwa akiishi,” alidai.
“Tulifika nyumbani kwa Mdude Nyagali, eneo la Iwambi, na kushuhudia hali halisi, mlango umevunjwa na mazingira ya tukio yanatia mashaka kutokana na kiasi kikubwa cha damu kilichokuwa kimemwagika eneo hilo,” ameongeza.
Imedaiwa kuwa baada ya kufanikisha walichokusudia, watu hao walimpakia kwenye gari na kuondoka kupitia vichochoro vinavyounganisha barabara zinazoelekea Mamlaka ya Mji wa Mbalizi au jijini Dar es Salaam.
Madai ya kuhusika polisi
Mbeyale alidai kuwa, kwa mujibu wa madai ya mke wa Mdude (jina limehifadhiwa), watu hao walipofika nyumbani waligonga mlango na walipojibiwa, walijitambulisha kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi.
Amedai baada ya hapo walivunja mlango, wakaingia ndani na kuanza kumshambulia kwa kipigo.
“Taarifa hizo zinatupa mwanga kuhusu watu waliomhusisha katika tukio hili. Kwa maelezo haya, ni wazi sasa tunapata picha ya waliohusika, na tunasisitiza tena msimamo wetu kwa Jeshi la Polisi kutoa ufafanuzi wa kina, amedai.”
Kauli ya Wakili Mwabukusi
Awali, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, kupitia akaunti yake ya mitandao ya kijamii, alieleza kuwa amepokea taarifa usiku huu kwamba Jeshi la Polisi limefika nyumbani kwa mwanaharakati Mdude Mpaluka Nyagali.
Kwa mujibu wa maelezo yake, askari hao walivunja mlango, wakaingia ndani, wakampiga kwa kutumia vitu mbalimbali na kumsababishia majeraha kabla ya kuondoka naye.
“Hili ni tukio jingine linaloendeleza mfululizo wa vitendo vinavyolenga kuwadhulumu na kuwaumiza wale wanaoonekana kuwa wakosoaji wa Serikali, kinyume na sheria na misingi ya haki za binadamu.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuhakikisha usalama wa Mdude Mpaluka Nyagali na kuhakikisha anapatiwa matibabu stahiki mara moja,” amesema.