
Wadau mbalimbali wa soka nchini wamegawanyika kuhusu makosa yanayojirudia ya waamuzi wanaocheza Ligi Kuu Bara, baadhi wakitaka iundwe kampuni itakayowasimamia, huku bodi ikisema kuna makosa saba kila baada ya dakika tisini.
Wadau hao walitoa maoni yao kupitia mjadala wa njia ya mtandao wa Mwananchi X Space, uliokuwa na mada isemayo; ‘Makosa ya Waamuzi Ligi Kuu Bara, nini kifanyike’, ambapo viongozi wa sasa na wale wa zamani wa soka nchini, sambamba na wadau wengine walitoa maoni yao juu ya tatizo hilo.
Mdau wa michezo na mmoja wa viongozi wa zamani wa Njombe Mji, Hassan Macho, alisema ni wakati wa kutenga eneo la waamuzi kuwa chini ya kampuni, ili pale watakapofanya makosa basi kampuni ndio ichukuliwe hatua.
“Badala ya kamati zilizopo ambazo zina ushawishi wa michezo husika ni bora kuwa na kampuni husika ambayo itachukuliwa hatua tofauti na ilivyo sasa,” alisema Macho na kuongeza;
“Ukiona mwanafunzi kafanya vizuri maana yake kaelewa lakini akienda kwenye vitendo anaenda akiwa na ushawishi ukiangalia mechi za madaraja ya kati kuanzia la kwanza, la pili, ligi ya mabingwa mkoa waamuzi wanafanya kazi yao vizuri ukiangalia unaridhika na hata wakikosea hayawi makosa makubwa.
“Eneo la ushawishi kwa waamuzi huwa haliangaliwi zaidi na wadau zaidi ya mijadala ya kaiwa ya juu kwa juu hili eneo mara nyingi sana inaonekana ni maamuzi yake au ya msukumo na kama ni hivyo lazima makosa yake yaonekane.”
Macho alisema kamati ya uamuzi inafanya kazi yake kwa usahihi, lakini waamuzi wanaopangiwa mechi siku tatu kabla ya mchezo ndio wanatengeneza mwamuzi kuwa na ushawishi na hapo ndio unaona anakuwa na maamuzi mabaya ya upande mmoja.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo amesema kuna wanaoamini kutegemea kamati ya waamuzi bado ni tatizo tofauti na mataifa mengine yaliyoendelea ambayo yameunda kampuni zinazosimamia waamuzi, lakini hata huko bado kuna matatizo.
“Hiyo kampuni ndio inalipa gharama nyingi kwa kushughulikia gharama zote za waamuzi inalipa fedha nyingi kule Ulaya, lakini bado kuna mijadala mingi hususani msimu huu hadi Real Madrid wao wanaamini wanafanya jitihada za makusudi ili wasifanikiwe msimu huu,” alisema Kasongo na kuongeza;
“Kuna mabadiliko makubwa ya upatikanaji wa waamuzi, lakini kwetu bado tuna mifumo ya awali kwa kutegemea vyama vya waamuzi na kamati za waamuzi wenzetu hawapo, lakini changamoto ya tatu ni upatikanaji wa waamuzi ambaye ana mafunzo ya siku tano hadi saba tu ya kumtambua kuwa mwamuzi.”
Kasongo alisema hivyo inamfanya mwamuzi aanzie madaraja ya chini na baadae kuja kufundisha Ligi Kuu, changamoto katika upatikanaji huo hakuna maandalizi ya kuwaandaa hao waamuzi wanaokuja kuchezesha soka.
MAKOSA SABA KILA DK 90
Kasongo pia alisema tafiti zinaonyesha katika kila mchezo wa dakika 90 kuna makosa yasiyopungua saba ambayo yanaweza kunufaisha timu A na kuiumiza timu B.
“Uamuzi unazungumzwa sana duniani kote katika kuzungumza huko ndio maana wenzetu uamuzi wa kutegemea ubinadamu wa waamuzi wakaamua kuachana nao na kuingia kwenye teknolojia,” alisema Kasongo na kuongeza;
“Yanaweza kunusaisha timu A au timu B pamoja na wenzetu walioendelea na kufanikiwa kwenda kwenye teknolojia hiyo bado kuna mapungufu kama kawaida, ni ukweli usio pingika kwamba zimeleta tija kubwa.”
Kasongo aliongeza tafiti zinaonyesha kuwa teknolojia hiyo kwa asilimia kubwa imepunguza makosa kumeongezeka ufanisi, lakini kwa Tanzania tunategemea ubinadamu wa uamuzi imekuwa ni changamoto kubwa.
“Waamuzi wakikosea imekuwa changamoto kubwa hatuna visaidizi vya kuwasaidia waamuzi wetu lakini duniani katika masuala ya mabadiliko ya uamuzi lakini kwetu bado tunategemea mwamuzi kutoka chama cha uamuzi wenzetu wametoka huko wana kampuni ya waamuzi,” alisema Kasongo.
Makatibu wa zamani watia neno
Katika mjadala huo, Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa alisema wakati mwingine tatizo linachangiwa na mashabiki wenyewe na kutaka wapewe sapoti na mafunzo endelevu.
“Tunapoongelea mchezo wa soka tunaongelea sheria zake, kwetu tumekuwa na changamoto ya waamuzi, nilikuwa najaribu kuangalia uwezo mdogo kwa waamuzi, ufanisi mdogo na kiwango na yale yanayoleta makosa ya kinidhamu inaweza kutokana na matatizo ya makusudi,” alisem Mwesigwa na kuongeza;
“Tatizo la waamuzi ni ishu za kibinadamu kama ilivyo mahakamani, lipo sehemu nyingi kama unakuwa na tafsiri tofauti za kisheria, watendaji wako wanapata elimu ya kutosha, kila mtu anapangiwa kazi au majukumu kulingana na elimu yake kwanza kwa mafunzo aliyoyapata wakati anachezesha baadhi ya michezo.”
Katibu huyo wa zamani wa Yanga kabla ya kula shavu TFF aliongeza; “Ligi nyingine ukichezesha vibaya wanakushusha ligi ya chini ili kujifunza kupunguza makosa kwa waamuzi, haya mafunzo yana ugumu wake na mpira wa mguiu sio kitu cha kuamka na kuchezesha mpira wa miguu, lazima tuwe na watu wanaouelewa na uzoefu wa kuchezesha.
“Tuwape sapoti na mafunzo endelevu waendelee kupata motisha watakuwa vizuri zaidi, tunapaswa kuwa na taratibu za kinidhamu matatizo ya kawaida ama makusudi mwamuzi achukuliwe hatua kabisa nadhani hayo yakizingatiwa yatapunguza ingawa hayatamaliza yote.
“Teknolojia inaweza kusaidia lakini inaweza kuleta presha kwetu hapa, tunataka lakini hatuna wazoefu kwenye teknolojia hiyo, wakati mwingine tatizo tunalileta sisi kwa sababu unaangalia mpira kwenye TV marudio unabishana kwenye mitandano tunatengeneza presha.”
Mwesigwa alifafanua zaidi kwa kusema; “Wakati mwingine tunaweza kuzidisha tatizo kubwa na kuweka presha linapokuja suala la hizi timu mbili, hata marefa wakitoka nje wakaletwa hapa nchini bado kuna makosa yatatokea, ni muhimu kuangalia taaluma na kimaadili na haya yakifanyika tunaweza kwenda mbele ingawa sio jambo la siku moja.”
Kwa upande wa Katibu Mkuu mwingine wa zamani wa TFF, Angetile Osiah enzi za Rais Leodegar Tenga, alisema tatizo ni uongozi mbovu uliopo nchini kwa kushindwa kutoa uhuru kwa vyombo mbalimbali vinavyohusika na soka kama waamuzi huru huku akiwataka wadau wabishane kwa maamuzi ya kunufaisha mipira.
“Hakuna viongozi au chombo ya kusimamia uamuzi hakuna mtu ambaye anasimama kuzungumzia suala hilo hili ni tatizo, mpira ni biashara kubwa sana watu wanaohusika na mpira wanatakiwa kujitokeza na kuzungumza,’’ alisema Angetile.
Angetile alisema kila mmoja awajibike kutokana na makosa yanayotokea mpira ni mchezo ambao ni biashara kubwa hakuna vyombo huru wamejaa machawa na katiba imeruhusu kuwepo kwa watu hao.
“Ligi yetu ni ya nne kwa sababu nchi nyingine zipo hoi na hazina wadhamini, Tanzania haijafika kiwango cha kuwa bora hivyo, waamuzi wanaochezesha mechi za Yanga hawawezi kuchezesha mechi za Simba hapana.”
VAR ITACHELEWESHA
Mfanyabiashara maarufu na mdau mkubwa wa soka nchini, Azim Dewji kwa upande wake alisema hakuna haja ya kutumia gharama kubwa kununua na kutumia vifaa vya VAR, lakini zitumike televisheni kuangalia marudio ya mechi ili kubaini makosa.
“Hakuna haja ya kutafuta VAR, waamuzi wawe wanaangalia marudio ili wajue makosa yao ili kujirekebisha, hakuna haja ya kuingia gharama wakati tv na VAR hakuna tofauti,” alisema Dewji, kauli inayokumbusha tukio la pambano la Simba na Yanga lililopigwa kwa Mkapa enzi hizo Uwanja wa Taifa ambapo bao la Simba lilikataliwa kabla ya marejeo ya televisheni uwanjani hao kumfanya mwamuzi kuweka mpira kati na kuwa bao la kusawazisha.
Tukio hilo lilitokea Machi 5, 2011 katika mechi iliyochezwa mwamuzi Oden Mbaga aliyelikataa bao la MussaHassan Mgosi, lililogonga nguzo ya juu na kudunda chini, kabla ya kurejea uwanjani. Wachezaji wa Simba walimfuata mwamuzi na kumtaka aangalie marudio ya katika runinga na kweli ilionekana mpira ule ilivuka mstari wakati ukidunda chini. Mbaga alibadilisha maamuzi yake na kukubali goli, Mgosi akawa ameisawazishia Simba baada ya Stephano Mwasika kuitanguliza Yanga na mechi kuisha kwa sare.
Kwa upande wa Deo Mruah, mdau wa soka alisema moja la sababu zinazochangia waamuzi kuyumba uwanjani ni ushabiki uliowatawala wadau wengi wa soka kiasi cha kuwapa presha waamuzi hao.
“Watu hawaangalii sana taalumu isipokuwa wanaangalia kinachowanufaisha, ni kweli tuna changamoto ya waamuzi, wachezaji, miundombinu na fedha ila tumechangua eneo moja la kujifichia jambo ambalo linaonyesha wazi tumeendekeza zaidi ushabiki.”
Mdau huyo alisema kumekuwa na ushabiki hasa kwa klabu hizi kubwa kubwa ambazo wanaozishabikia wanaamini hazifungiki, kitu kinachowavuruga na kuwapa presha waingiapo uwanjani.
Mdau mwingine, Cae Jay alisema waamuzi wapewe semina maalumu ya kuweza kutofautisha mapenzi na ujuzi.
“Wewe unaweza ukawa shabiki wa Simba au Yanga ila ukichezesha timu mojawapo kati ya hizo na zingine ni bora kuzingatia weledi, pia tutambue thamani ya ligi yetu kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kupunguza makosa yanayojirudia kila siku,” alisema Cae Jay, huku shabiki wa Simba na mdau wa michezo, Baazi amesema ligi inapaswa kuangaliwa kwa ujumla kwa kila timu shiriki kuwa na haki na sio za Simba na Yanga ambazo zinapewa kipaumbele kikubwa.
“Mpira wetu tunauharibu wenyewe hususani eneo la mashabiki wa Simba na Yanga, watu lazima waheshimu ligi lakini dhana ya kuziona timu mbili hazitakiwi kufungwa au kusemwa ndio inasababisha waamuzi kuwa na hofu,” alisema na kuongeza:
“Shabiki anaongea vitu ambavyo hata kama ningekuwa refa ningeingia na presha, lazima tuangalie ligi kwa ujumla wake na sio Simba au Yanga tu.”
Waandishi wa Habari, Mustapa Mtupa na Devota Kihwelo kwa upande wao wakati wanachangia alisema kuna haja ya waamuzi kupigwa msasa mara kwa mara kujikumbusha sheria, lakini pia kuharakishwa kwa matumizi ya VAR yaliyoelezwa yangeanza kutumika msimu huu bila mafanikio.