Sintofahamu kifo cha mtoto Elvis, askari watuhumiwa kuhusika

Songwe. Wakati familia ya Jack Pemba ikilituhumu Jeshi la Polisi kuhusika na mauaji ya mtoto wao, Elivis Pemba, Jeshi la Polisi mkoani Songwe limeeleza sababu ya kifo cha kijana huyo huku likiahidi kuendelea na uchunguzi kubaini ukweli.

Elvis (18) alidaiwa kufariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili, Februari 9, 2025 huko Mji wa Tunduma mkoani humo ikiwa ni siku mbili kupotea nyumbani kwao.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Februari 12, 2025 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Agustino Senga amesema amepokea taarifa za kifo hicho akieleza ripoti za awali zimeeleza marehemu huyo kuuawa na watu kwa tuhuma za wizi wa simu.

Amesema baada ya kufanya tukio hilo, mwenye simu aliomba msaada kwa watu ambao walimshambulia hadi kupelekwa hospitali ambapo wakati akiendelea na matibabu alifariki dunia.

“Taarifa za awali ni kwamba aliiba simu, japokuwa yapo maneno yanayosemwa hivyo RCO (Ofisa upelelezi Mkoa) yupo huko anafuatilia tujue ukweli wake,” amesema.

“Hatujamshikilia yeyote kwakuwa tukio lilitokea usiku wa saa 7 hadi saa 8 usiku na faili lilifunguliwa hivyo tusubiri uchunguzi zaidi tutaeleza,” amesema Kamanda huyo.

Familia yasimulia

Veronica Mwang’onde, mzazi wa marehemu, Elvis amesema mtoto wake alimuacha nyumbani kwao akiwa na mjomba wake kwenda hospitali ambapo Ijumaa mtoto huyo alikwenda kununua maji na hakurudi.

Amesema kwa muda wote tangu amalize shule hakuwahi kuripoti kuwapo mgogoro baina yake na mtu yeyote hata uhusiano wa kimapenzi na kwamba alikuwa mtu wa kukaa zaidi ndani.

“Mwezi ujao Machi tulikuwa katika maandalizi ya kumpeleka chuo, ndio Ijumaa alienda kununua maji na hakurudi kwa siku mbili mfululizo,” amesema.

“Baadaye alionekana akiwa ameshikiliwa na askari anaumwa akapelekwa hospitali, ghafla tunaambiwa amekufa, tunachoomba ni hatua stahiki kuchukuliwa kwa askari hao waseme ilikuaje,” amesema Veronica.

Kwa upande wake ndugu wa marehemu, amesema katika uchunguzi wa kitaalamu ilibainika marehemu kupigwa na kuumizwa na vitu vyenye ncha kali hadi kusababisha kifo chake.

“Kutokana na kipigo kizito hadi kutokwa damu nyingi maeneo mbalimbali ya mwili ilisababisha Elvis kufariki na nimewasilisha maelezo yangu kwa Polisi,” amesema

Amesema pamoja na taarifa za kwamba taarifa za Polisi kuwa marehemu alipigwa kwa wizi hazina ushahidi wowote ikiwamo mlalamikaji wala tuhuma zake na hakuna faili linaloonesha usahihi.

“Mkuu wa kituo anasema kuna mtu alimleta huyo mtoto kumshitaki lakini faili na taarifa zake hazipo, inaeleza alikutwa barabarani akaletwa tunaomba kupata ukweli na undani zaidi,” amesema.