
Ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Singida Black Stars dhidi ya Kagera Sugar, kwenye uwanja wa Liti, mkoani Singida katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, umeifanya timu hiyo kukutana na Simba katika hatua ya nusu fainali.
Simba ambayo ilishinda mabao 3-1 jana kwenye uwanja wa KMC, Complex dhidi ya Mbeya City ilifanikiwa kutinga katika hatua ya nusu fainali ambapo ilikuwa ikimsubiri mshindi kati ya Singida Black Stars au Kagera Sugar.
Mabao ya Singida Black Stars yalifungwa na Victorien Adebayor katika dakika ya 11 huku bao la pili likiwekwa kambani na Jonathan Sowah katika dakika ya 66.
Mchezo mwingine ulichezwa katika dimba la Major General Isamuhyo ambapo wenyeji JKT Tanzania wakitinga katika hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Pamba Jiji.
Mabao ya JKT Tanzania yamefungwa na Mohamed Bakari aliyefunga mawili katika dakika ya 70 kabla ya kufunga lingine dakika ya 81 akiunganisha wavuni mpira aliopewa pasi na Karimu Mfaume wakati bao lingine alijifunga beki wa Pamba Jiji, Justine Omary katika dakika ya 37.
Baada ya ushindi huo, JKT Tanzania wametinga katika hatua ya nusu fainali huku wakisubiri kucheza na mshindi kati ya Yanga itakayokuwa nyumbani hapo kesho Aprili 15, 2025 kwenye uwanja wa KMC, Complex kuikaribisha Stand United ya Shinyanga.