Singida Black Stars ifanye jambo Shirikisho Afrika

KIJIWENI hapa tuliuangalia kwa utulivu wa hali ya juu kutokana na mpira uliochezwa katika mechi baina ya Simba na Singida Black Stars katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwenye Uwanja wa Tan-zanite Kwaraa, mjini Babati mkoani Manyara.

Singida BS ilimaliza kibabe mechi kwa ushindi wa mabao 3-1, lakini haikuishia kupata ushindi tu bali waliupiga mpira mwingi siku hiyo.

Japo tunaweza kuitetea Simba kwamba wachezaji wao wengi walikuwa wamechoka na ukweli ni huo, lakini Singida BS ilikuwa na ubora maana kukonda kwa tembo hakuwezi kumfanya awe na mwili kama sungura.

Tumeshuhudia mechi nyingi Simba inakuwa na wachezaji waliochoka, lakini bado iliweza kupata ushindi lakini kwa juzi ikashindwa kwa sababu Singida walikuwa na wachezaji wazuri ambao walitumia vizuri udhaifu huo wa Simba kupata ushindi mnono.

Aina ile ya mechi ndio watu tunataka kuona mfululizo hapa nchini kwetu pindi timu tofauti zinapokuta-na badala ya mambo kuwa rahisi kwa timu kubwa kila siku jambo ambalo linaweza kuzifanya zisiwe imara.

Sasa Singida BS isiishie kucheza vile dhidi ya Simba tu bali inatakiwa ihamishie nguvu katika Kombe la Shirikisho Afrika ambalo itashiriki msimu ujao ikiwa na Azam FC kwa vile haiwezi kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi.

Kikosi walichonacho kinaweza kabisa kupambana kimataifa na ikafanikiwa na haitakiwi kujiona kwamba haitaweza kwa vile klabu ndogo au ndio inashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza.

Siku hizi timu inaweza kufanikiwa kimataifa hata kama ndio inashiriki kwa mara ya kwanza na mifano iko mingi ya hilo hivyo inaweza kuwa chachu ya Singida BS kufanya vyema.

Kama hapa nchini Namungo iliwahi kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, basi Singida Black Stars ikijipanga inaweza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *