
Dar es Salaam. Kupata au kutopata vyeti kwa wanafunzi 54 wa Tanzania waliomaliza masomo yao nchini Sudan mwaka 2022, imebaki kuwa sintofahamu.
Wanafunzi hao ni wale waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo vikisababisha mauaji, watu kukimbia makazi yao, magonjwa na njaa.
Wakizungumza na gazeti dada la The Citizen jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti wiki hii, wanafunzi hao wameeleza kuwa vyeti hivyo si tu karatasi za kawaida, bali vinawakilisha miaka ya kazi ngumu, kujitolea na matumaini ya maisha bora ya baadaye.
Semili Pazi, mwanafunzi Mtanzania aliyesomea Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika nchini Sudan, ameelezea jinsi matumaini yake yaliyofifia.
Amesema ni jambo la kusikitisha kwamba wengi wao wamekaa miaka saba wakisoma katika nchi ya kigeni, lakini wamerejea nyumbani bila vyeti.
Walitumia miaka mitano kusomea udaktari, mwaka mmoja kujifunza lugha na mwaka mwingine wakiwa mapumzikoni, wakati dunia ilipokuwa ikipambana na janga la COVID-19.
“Nilipomaliza mitihani yangu, nilibaki nchini Sudan kufanya uhakiki na kusubiri vyeti vyangu. Kwa bahati mbaya, kutokana na vita vilivyozuka Aprili 2023, tulilazimika kurejea nyumbani pamoja na wengine bila kupokea vyeti vyetu,” amesema.
Pazi, aliyesomea shahada ya kwanza ya udaktari, alimaliza masomo yake Februari 2023, lakini bado hajapokea hati za matokeo wala cheti chake, ambavyo ni muhimu kwa mchakato wa ajira.
Wanafunzi hao wameanza kufuatilia suala hilo wakiwa nyumbani kupitia Wizara ya Elimu.
Kwa mujibu wa Pazi, wamekuwa wakifuatilia suala hilo kupitia wizara husika, lakini waliambiwa wawasiliane na Wizara ya Mambo ya Nje kwa msaada, juhudi ambazo hazijazaa matunda.
Ameendelea kusema kuwa Novemba mwaka jana walifahamishwa kwamba chuo kilianza kufanya kazi mtandaoni, na wakaanza kufuatilia, lakini juhudi zao hazijazaa matunda kwa sababu kampasi kuu iliyopo Khartoum haifanyi kazi tena.
Chuo hicho kilianzisha tawi Port Sudan na wanafunzi wengi walifanya malipo mtandaoni wakitarajia kupokea vyeti vyao. Hata hivyo, hadi sasa hakuna kilichofanikiwa.
“Tunaomba Serikali yetu izingatie kutusaidia kupata uthibitisho au cheti kinachothibitisha kuwa tulisoma Sudan na kumaliza masomo yetu.”
“Hii itaturuhusu kufanya mafunzo kwa vitendo na kutekeleza taaluma zetu mahali pengine. Kwa mfano, nilisomea udaktari na imekuwa changamoto kwangu kutafuta kazi kwa sababu bado sijafanya mafunzo ya vitendo,” ameeleza.
Pia amependekeza Serikali kutoa barua ya uthibitisho inayoonyesha kuwa wanafunzi walihudhuria na kuhitimu vyuo vya Sudan.
Ikiwa hilo lingefanyika, wanafunzi wengi wangekuwa wameshakamilisha mafunzo ya vitendo na wengine tayari wangekuwa wameanza kazi au shughuli nyingine.
Kiongozi wa wanafunzi waliokuwa wakisoma Sudan, Sulfian Mbalazi, alihitimu shahada ya kwanza ya kemia ya viwanda Novemba 2021.
Baadaye alijiunga tena mwaka 2022 kusomea shahada ya pili katika kozi hiyohiyo. Amesema vyeti vyake vyote vya shahada ya kwanza na elimu ya sekondari vipo huko.
“Tulifuatilia suala hili kwa Wizara ya Elimu, wakatuambia tuende Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Tumekuwa tukiandika barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje tangu mwaka jana, lakini hadi sasa hakuna majibu,” amesema.
Mbalazi anaamini kuwa kama angepewa vyeti vyake, angefanya mambo mengi, lakini sasa hawezi kufanya chochote.
Amesema, “Uzuri wa Sudan ni kwamba baada ya kumaliza shahada ya kwanza, unapojiunga na programu ya shahada ya pili, wanakushirikisha kufundisha katika chuo kama kujitolea. Nilikuwa nimepewa nafasi ya kufundisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza, lakini kwa bahati mbaya vita vilizuka.”
Amebainisha kuwa wanafunzi kutoka nchi nyingine waliokuwa wakisoma Sudan na kumaliza masomo yao tayari wameanza kupokea vyeti vyao, lakini hakuna Mtanzania yeyote aliyepokea vyeti.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki bado haijatoa majibu kuhusu suala hilo.
Lakini gazeti dada la The Citizen limeona barua kutoka Wizara ya Elimu kwenda Wizara ya Mambo ya Nje, ikiomba msaada kwa wanafunzi hao.
Mwanafunzi mwingine, Ibrahimu Kajanja, aliyemaliza shahada ya sayansi katika jiolojia Desemba 2022, alikuwa na simulizi kama hiyo.
Alieleza kuwa chuo kilianza kutoa vyeti mwaka 2023, lakini vita vilizuka na kusimamisha mchakato huo.
“Nilikuwa katika mchakato wa kukusanya vyeti vyangu, lakini havikutolewa. Tulirejea nyumbani Aprili 27, 2023, kwa msaada wa Serikali. Ikiwa tuliweza kurejea kupitia msaada wa Air Tanzania, kwa nini sasa hatuwezi kusaidiwa?” amehoji.
Wanafunzi wa Sudan
walivyokuja Tanzania
Juni 19, 2023, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliwapokea wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Sayansi, na Teknolojia (UMST), Khartoum, Sudan.
Wanafunzi hao walihamishiwa Tanzania ili kukamilisha mwaka wao wa mwisho wa masomo kutokana na kuzuka kwa vita nchini Sudan.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuwapokea wanafunzi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohamed Janabi alisema hospitali hiyo itatoa fursa kwa wataalamu hao kujifunza kama ambavyo inatoa kwa wataalamu wengine wa ndani na nje ya nchi, na hata baada ya kumaliza masomo kama watapenda kufanya mafunzo tarajali MNH itawapa nafasi hiyo.
Chanzo cha vita Sudan
Desemba 2018, Omar al-Bashir aliyeitawala nchi hiyo tangu mwaka 1986 alikabiliwa na maandamano ya wananchi waliopinga utawala wake wa kidikteta.
Mgogoro huo ulidumu kwa miezi minane hadi Aprili 2019, ambapo jeshi (pamoja na Kikosi cha Usaidizi wa Haraka – RSF) walimwondoa al-Bashir kupitia mapinduzi ya kijeshi na hivyo kumaliza utawala wake wa miongo mitatu.
Jeshi lilianzisha Baraza la Mpito la Kijeshi (TMC), ambalo lilikuwa utawala wa kijeshi. Bashir alifungwa katika gereza la Khartoum lakini hakukabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambayo ilikuwa imetoa hati za kukamatwa kwake kwa mashitaka ya uhalifu wa kivita.
Maandamano ya kudai utawala wa kiraia yaliendelea na ilipofika Juni 2019 vikosi vya usalama vya TMC, vilivyohusisha RSF na Jeshi la Sudan (SAF), viliua zaidi ya waandamanaji 100 jijini Khartoum na wengine walibakwa.
Mnamo Agosti 2019, kutokana na shinikizo la kimataifa na upatanishi wa Umoja wa Afrika na Ethiopia, jeshi lilikubali kushiriki madaraka na serikali ya mpito ya umoja wa kiraia na kijeshi (Baraza la Uongozi la Mpito), lililoongozwa na Waziri Mkuu wa kiraia, Abdalla Hamdok. Uchaguzi ulipangwa kufanyika mwaka 2023.
Hata hivyo, mnamo Oktoba 2021, jeshi lilitwaa mamlaka kupitia mapinduzi yaliyosimamiwa na kiongozi wa Jeshi la Sudan (SAF), Abdel Fattah al-Burhan, pamoja na Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu Hemedti.
Lakini kama wanavyosema, mafahali wawili hawaishi zizi moja, sasa Burhan na Hemedti wameanzisha vita wao kwa wao.
Athari za vita
Zaidi ya watu milioni 11.4 sasa wamehama makazi yao ndani ya nchi, huku zaidi ya milioni tatu hasa wanawake na watoto wakikimbilia nchi jirani.
Hali hii imezidi kuwa mbaya kutokana na mvua kubwa na mafuriko vilivyotokea kati ya Juni na Septemba, ambayo yameathiri karibu watu 600,000, kuwalazimisha zaidi ya 172,500 kuhama na kusababisha uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu.
Pia yamesababisha kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu. Maeneo yaliyoathirika vibaya zaidi kama Bahari Nyekundu na Darfur Kaskazini, yanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa, hali inayozidisha changamoto kwa wakazi waliokuwa tayari wanahangaika na mizozo na ukosefu wa utulivu.