
Dar es Salaam. Yapo mengi yanayoweza kuandikwa ama kusimuliwa kumhusu Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Kipenka Mussa hususani katika utumishi wake wa umma.
Jaji Kipenka ambaye alizaliwa Desemba 28, 1954 amefariki dunia Jumamosi Novemba 2, 2024, katika Hospitali ya Mloganzila jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwili wake umeagwa leo Jumanne, Novemba 5, 2024 nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, na baadaye jioni utasafirishwa kwenda kijijini kwao Kinampanda, Singida, utakapopumzishwa kaburini kesho Jumatano.
Wakati wa uhai wake alilitumikia Taifa katika maeneo mbalimbali katika mihimili yote mitatu ya dola, yaani Serikali alikohudumu kama Wakili wa Serikali, Bunge, alikohudumu katika nafasi ya Katibu wa Bunge na Mahakama alikotumika katika nafasi ya Jaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Hivyo, wakati anaondoka duniani nyuma yake anaacha simulizi ya kusisimua kuhusiana na utumishi wake ulioacha alama za kukumbukwa kutokana na umahiri, uvumilivu na ujasiri wake wa kufanya mambo ambayo kwa nafasi yake kama mtumishi haikutarajiwa kuyafanya kwa urahisi.
Moja ya simulizi hizo ni kuhusiana na ujasiri wa pekee aliokuwa nao katika kufanya au kuamua mambo ambayo katika hali ya kawaida kwa mtumishi wa umma yanaweza kuonekana kuwa si rahisi au ya kustua.
Ni kawaida na haki ya mdaiwa (pande husika katika kesi) kumkataa hakimu au jaji na kumuomba ajiondoe katika kusikiliza kesi yake.
Lakini fikiria Wakili wa Serikali kula kiapo cha kumuomba Jaji ajiondoe katika kesi, au kuibua hoja dhidi ya hakimu au jaji kuwa amebadilisha mwenendo wa kesi, kwamba kile kilichozungumzwa si kile kilichoandikwa.
Bila shaka haya si mambo rahisi na ni nadra kufanyika, lakini Jaji Kipenka aliweza kuyafanya, mpaka akaifanya Mahakama ikachukua hatua ambayo haikuwa na haijawahi kusikika tena ikichukua baada ya hapo katika mazingira ya kawaida.
Pamoja na sifa nyingine, ujasiri huo wa Jaji Kipenka unaweza kuwa somo la namna ya utendaji na utumishi wa umma umethibitishwa na baadhi ya mawakili, ambao wamewahi kufanya naye kazi katika namna tofautitofauti.
Wakili Mwandamizi Richard Rweyongeza, amesema alimfahamu Jaji Kipenka akiwa Wakili Mfawidhi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Dodoma na kwamba alifanya naye kazi wakati yeye akiwa wakili wa kujitegemea mkoani Dodoma.
Amesema Jaji Kipenka alikuwa anapenda haki na alikuwa na akili sana na uwezo wa kugundua vitu vidogo vinavyojificha ambavyo mwanasheria wa kawaida asingeweza kuvibaini kwa urahisi, kwani alikuwa anasoma sana na kufanya utafiti.
Akizungumzia ujasiri wa Jaji Kipenka, Wakili Rweyongeza anasema katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambayo yeye Rweyongeza alikuwa wakili wa mdai na Kipenka akiwa Wakili wa Serikali, alimkataa jaji asiisikilize kesi hiyo.
Kesi hiyo ya mwaka 1993 pamoja na mambo mengine Mtikila alikuwa anapigania kuruhusiwa kwa mgombea huru katika urais, ubunge na udiwani, awali ilikuwa imepangwa kusikilizwa na Jaji James Lewis Mwalusanya.
Lakini Jaji Kipenka, akiwa Wakili Mwandamizi wa Serikali aliyehusika kwenye kesi hiyo, alimuomba Jaji Mwalusanya ajiondoe kwa madai kuwa alikuwa ameshaonesha mtizamo wa kupendelea upande wa mdai.
Kutokana na pingamizi hilo Jaji Mwalusanya alilazimika kujiondoa badala yake Jaji Mkuu akamteua Jaji Kahwa Lugakingira kutoka Mwanza akaenda kusikiliza kesi hiyo, ambaye katika hukumu yake mwaka 1995 aliruhusu kuwepo mgombea huru.
“Hiyo ni sifa ya pekee na huo ni ujasiri ambao si wa kawaida,” amesema Wakili Rweyongeza.
Rweyongeza anasema jambo lingine linaloonesha ujasiri wa kipekee wa Jaji Kipenka aliuonesha katika kesi ya Shirika la Nyumba (NHC).
Wakili Rweyongeza anasema wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya kesi hiyo katika Mahakama ya Rufani, Jaji Kipenka (wakili wakati huo) aliibua hoja kuwa jaji aliyekuwa ameiamua alikuwa amebadilisha kumbukumbu (mwenendo), kwamba kile kilichokuwa kimezungumzwa si kile alichokuwa amekirekodi.
“Hii ilisababisha hata Mahakama ya Rufani ikakaa kuendesha ushahidi kutazama kama kweli Jaji alikuwa amebadilisha kumbukumbu. Hivyo, mawakili wa pande zote waliitwa kutoa ushahidi kwamba kweli kilichozungumzwa kwenye ushahidi ndicho hiki au sicho chenyewe,” amesema Wakili Rweyongeza na kuongeza:
“Nakumbuka tulikuwa Dodoma mahakamani, ikaitisha ushahidi watu wakatoa ushahidi. It was interesting (lilikuwa jambo la kuvutia sana), nadhani watu wengine hawajawahi kuisikia hilo.”
Kwa kawaida Mahakama ya Rufani haina mamlaka ya asili (original jurisdiction) yaani haina mamlaka ya kusikiliza kesi kwa mara ya kwanza (trial) ama kupokea ushahidi kutoka kwa mashahidi, bali husikiliza rufaa au mapitio.
Lakini kutokana na hoja hiyo Mahakama ya Rufani ikachukua hatua ambayo ama ilikuwa haijawahi kuichukua katika hali ya kawaida.
“Mahakama baada ya kukaa na kusikiliza ushahidi ilikubaliana na hoja yake kwamba kweli jaji alikuwa amebadilisha mwenendo. Hivyo Mahakama ya Rufani ilibatilisha hukumu na mwenendo wake. Kwa hiyo utaona ni namna gani alivyokuwa jasiri, ni ujasiri usio wa kawaida,” anasema Rweyongeza.
Anasema kuwa, mawakili wengi hawana ujasiri wa kuibua hoja kama hiyo dhidi ya jaji na kwamba pengine ni jambo ambalo sasa hivi likiibuliwa kwamba jaji amebadilisha mwenendo pengine watu hawataweza kuamini.
Hata hivyo, anasema kuwa hiyo ilionesha kwamba jambo hilo linawezekana kwa sababu hata majaji ni binadamu, inawezekana akabadilisha mwenendo.
Wakili Rweyongeza anasema kuwa pia Jaji Kipenka ndiye aliyesababisha Sheria ya Utekelezaji Wajibu na Haki za Msingi – Bradea) ilipotungwa taratibu zake kesi zinazofunguliwa chini ya Sheria hiyo ziwe zinasikilizwa na majaji watatu.
“Mwanzoni kwanza kesi hizi mtu alikuwa anaweza kufungua kesi popote, mfano tukio limetokea Dodoma kesi anafungua Mwanza. Halafu Jaji mmoja anachukua kesi anaisikiliza,” anasema Wakili Rweyongeza.
Anasema wakati huo kulikuwa na kesi nyingi za namna hiyo zilizokuwa zinakwenda kufunguliwa Dodoma kwa kuwa walivutiwa na kwamba wakati ule majaji wengine walikuwa wanaogopa kesi hizo.
Hivyo, anasema Jaji Kipenka alitoa pendekezo na alisukuma mpaka ikapita na utaratibu ukabadilishwa kutoka jaji mmoja na kuwa watatu.
Rweyongeza anasema kuwa pia Jaji Kipenga alikuwa mvumilivu sana, huku akitoa mfano wa kauli moja aliyowahi kutolewa na wakili wa Serikali, wakati huo yeye Kipenka akiwa Jaji.
“Nakumbuka kuna wakili mmoja wa Serikali tukiwa mahakamani alimjibu Jaji Kipenka kuwa yeye (wakili) anajua sheria baada ya jaji kumrekebisha. Jaji Kipenka alisema tu kuwa haya bwana. Sasa utaona uvumilivu aliokuwa nao si wa kawaida. Ni majaji wachache wangeweza kuvumilia kauli kama hiyo.”
Hoja za Wakili Rweyongeza zinaungwa mkono na Wakili mwingine mwandamizi na rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Lugemeleza Nshala, ambaye anasema kuwa Jaji Kipenka alikuwa anafahamu sana sheria, hasa za haki za binadamu.
“Kwa hiyo alikuwa anafahamu sana masuala ya haki za binadamu akiwa kama Wakili wa Serikali na wakati akiwa jaji”, amesema Dk Nshala.
Dk Nshala pia anarejea pingamizi alilomwekea Jaji Mwalusanya akimtaka ajiondoe kusikiliza kesi ya Mtikala dhidi ya AG ambayo ni maarufu kama kesi ya mgombea binafsi (huru).
“Katika kesi hiyo (Mtikila) alikula kiapo kumkataa jaji Mwalusanya akimtaka ajitoe akidai kuwa atakuwa na upendeleo kwa sababu alikuwa ameshaandika vitabu vingi vya haki za binadamu vilikuwa vinafanana na kesi kama hivyo, hivyo akasema hapana, huyu hafai kusikiliza kesi hiyo,” anasema Dk Nshala.
Dk Shala anasema kesi nyingine ni rufaa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Wakili Jeremiah Mtobesya, iliyobatilisha kifungu cha 148 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Kifungu hicho kilikuwa kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na ofisa wa polisi kuzuia dhamana ya mshitakiwa/mtuhumiwa kwa madai ya masilahi ya umma.
“Yeye ndiye aliyeandika hukumu hiyo (kwa niaba ya jopo la majaji watano walioisikiliza), aliandika vizuri sana hukumu hiyo,” anasema Dk Nshala.
Naye wakili mwandamizi Fulgence Massawe anasema Jaji Kipenka alikuwa mpole na mkimya na kwamba alikuwa anaongea pale tu ilipokuwa inalazimu.
“Lakini Kipenka tunamfahamu zaidi kwa umahiri wake kwenye ripoti ya mauaji ya wafabyabiashara wa madini wa Morogoro, kwenye kesi ya Zombe na ya mauaji ya aliyekuwa mkurugenzi mstaafu wa Usalama wa Taifa, LutenI Jenerali Imran Kombe,”anasema.
“Ni mtu ambaye alisimamia haki na kwa mazingira yaliyokuwepo kuwatuhumu maafisa wakubwa wa polisi kama wale na ripoti ikafanyiwa kazi maana iliweza kuonesha uozo ulioko ndani ya Jeshi la Polisi.”