Dar es Salaam. Je, umewahi kusikia kijiji chenye mtu mmoja tu? Leo nitakupa stori ya kijiji hicho na historia yake.
Huko Marekani kwa Joe Biden, kuna kijiji kimoja kinaiwa Monowi (kinatamkwa Monoayi). Kijiji hicho kinapatikana katika kaunti ya Boyd, kaskazini mwa Marekani
Kaunti ya Boyd ina jumla ya wakazi 2,000 na miji mitatu katika kaunti hiyo, ina chini ya watu 10, huku Kijiji cha Monowi kikiwa na mkazi mmoja pekee.
Mtu anayeishi kwenye kijiji hicho ni kikongwe mwenye umri wa miaka 87, Elsie Eiler. Mwanamke huyo amekuwa anaishi peke yake tangu mwaka 2004 baada ya mume wake, Rudy kufariki dunia.

Basi bwana, unaambiwa bibi huyo amekuwa akikomaa na maisha peke yake kwa biashara yake ya kuuza mgahawa (baga na bia) kwa madereva na wafanyakazi wengine wanaopita kwenye barabara inayokatisha katika kijiji hicho.
Serikali ya Marekani inaitambua Monowi kama kijiji na kwa mujibu wa sensa ya Marekani ya mwaka 2022, kijiji hicho kilirekodiwa kuwa na mkazi mmoja pekee ambaye ni Elsie.
Kibongobongo unaweza kusema yeye ndio mwananchi, yeye ndio mwenyekiti wa kijiji, yeye ndio mjumbe na ndiyekila kitu.
Na kwenye kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa (kama zinazokuja), sijui anapigaje kampeni na kujipigia kura.
Duru zinaeleza kwamba kijiji hicho kilianzishwa mwaka 1902 na idadi kubwa ya watu iliyowahi kufikiwa katika kijiji hicho ni 123, na hiyo ilikuwa mwaka 1930.
Mwaka 1978, watu wengi walianza kukihama kijiji hicho kilichokuwa kikitegemea zaidi kilimo na kwenda kutafuta kazi katika maeneo mengine ya mijini.
Elsie na mumewe waliendelea kuishi hapo hadi walipojikuta wako peke yao na mwaka 2004, Elsie akajikuta yuko pekee baada ya mume wake kufariki dunia.
Mgahawa wa Elsie ndiyo biashara pekee inayofanyika katika Kijiji cha Manowi na hivi karibuni amekuwa kivutio kwa kuwa anatembelewa na watu tofauti hasa vyombo vya habari vinavyotaka kufanya naye mahojiano.
Kama ilivyo kwenye vijiji vingine, Monowi ina kanisa, barabara na hata gereza ambalo sasa limechakaa. Ibada ya mwisho ya mazishi iliyofanyika katika kanisa hilo ilikuwa mwaka 1960.
Nikifikiria maisha ya Elsie, namuona kama mtu mpweke zaidi duniani. Hata hivyo, watu wengine kutoka miji ya jirani wanamjali, huwa wanamtembelea baada ya muda fulani, wanakusanyika kwake, wanapiga ‘vyombo’ huku wakicheza gemu pamoja naye.
Amekuwa akitembelewa mara kwa mara na askari polisi na wafanyakazi wa ujenzi ambao wamekuwa wakifika nyumbani kwake kumjulia hali.
Maisha ya Elsie yamenikumbusha “Operesheni Sogea” iliyofanyika mwaka 1974 kama utekelezaji wa sera ya uanzishaji wa vijiji. Watu waliokuwa wakiishi mashambani kama Elsie walilazimishwa kuhama na kusogea kwa wengine ili kuanzisha kijiji vya ujamaa na kupatiwa huduma za jamii.
Watoto wa mwaka 2000 ambao wakiona muvi za mazombi hawalali peke yao kwenye nyumba, wataweza kuishi peke yao kwenye kijiji kama Elsie?