Simulizi ya kijana aliyeacha ujambazi na kumrudia Mungu, apewa spika

Njombe. Shukuru Mwalongo (37), mkazi wa Kijiji cha Lugawala, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, ameamua kuachana na maisha ya ujambazi wa pikipiki na uhalifu mwingine na kuamua kuzunguka kutoa ushuhuda wa mabadiliko yake ya kiroho.

Akielezea safari yake ya kutoka katika giza la uhalifu na kuingia katika huduma ya kuhubiri neno la Mungu, Mwalongo amesema amejizatiti kumsaidia kila mtu kubadilika na kujitokeza kutoka katika njia mbaya ili kumrudia Mungu.

Mwalongo amesema kuwa, kupitia ushuhuda wake ana matumaini ya kuhamasisha jamii ya Kijiji cha Lugawala na maeneo jirani kuacha matukio maovu na kujenga maisha bora.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga akimkabidhi spika Shukuru Mwalongo (37) mkazi wa Lugarawa Wilayani Ludewa baada ya kuacha uhalifu na kumrudia Mungu baada ya kifungo cha miaka mitano jela.

Ametoa ushuhuda huo  jana, Machi 27, 2025, mbele ya waandishi wa habari wakati akikabidhiwa msaada wa kipaza sauti na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, ikiwa ni sehemu ya msaada kutoka kwa Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga.

Kipaza sauti hicho kitamuwezesha Mwalongo kutangaza neno la Mungu kwa njia ya mafundisho na kuhamasisha mabadiliko kwa jamii. Makabidhiano hayo yalifanyika Kituo cha Polisi Njombe.

Akitoa ushuhuda wa uhalifu, Mwalongo ameelezea mbinu alizotumia katika kufanya wizi wa pikipiki, akieleza jinsi alivyokuwa akiziiba kwa kuvizia pikipiki za watu pindi wamiliki wanapoziegesha bila kuchukua tahadhari.

Mwalongo amesema katika kutekeleza wizi wake huo, alikuwa anakata waya za pikipiki ili ziweze kuwashwa bila ya kutumia funguo, kisha kuondoka nazo.

Amesema alifanya uhalifu huo kwa lengo la kupata kipato, lakini amejiwekea lengo la kubadili maisha yake kwa kuhubiri neno la Mungu, huku akitoa ushuhuda wake kama njia ya kuwahamasisha wengine kuepuka maovu.

                                                                                    

Historia ya uhalifu

Akizungumzia namna alivyokuwa akifanya uhalifu, Mwalongo ameelezea jinsi alivyoshirikiana na wenzake wawili katika kufanya matukio ya uhalifu mkoani Njombe, ambapo mmoja wa wenzake alikufa kwa kukatwa mapanga, na mwingine aliuawa kwa kumwagiwa petroli huko Halmashauri ya Mji wa Makambako.

Shukuru Mwalongo (37) mkazi wa Lugarawa Wilayani Ludewa aliyeamua kuachana na uhalifu na kuanza kuhubiri neno la Mung baada ya kifungo cha miaka mitano jela.

Mwalongo alikiri kuwa, licha ya kuendelea na matukio ya ujambazi kama kuiba pikipiki na kuwapiga nondo watu, hakupata mafanikio wala amani katika maisha yake ya kihalifu.

Amesema alibaki peke yake baada ya vifo vya wenzake na alijikuta akiendelea na vitendo vya uhalifu, lakini akashindwa kupata matokeo bora kutoka kwa matukio hayo.

Mwalongo ameongeza kuwa, hatua ya kuachana na uhalifu na kujiingiza katika huduma ya kuhubiri neno la Mungu ni njia pekee ya kupata amani ya kweli na maisha yenye manufaa.

Amesema kipindi cha nyuma zaidi ya miaka 15 alikuwa mhalifu ambaye alifanya matukio ya kijambazi maeneo tofauti mkoani Njombe kwa muda mrefu, lakini amesema hakuna faida aliyoipata katika maisha yake zaidi ya kunusurika kuuawa.

Mwalongo amesema kuna wakati alijikuta akijiuliza kuhusu mwisho wa njia aliyoichagua, hasa baada ya kupoteza wenzake wengi katika matukio ya kijambazi.

Akizungumza kuhusu mabadiliko makubwa aliyopitia, Mwalongo amesema: “Nilikuwa najiuliza, nitafika wapi kwa njia hii ya uhalifu? Wenzangu wengi walikufa, na nilibaki peke yangu. Nilijaribu kufanya tukio la mwisho la wizi wa pikipiki huko Ludewa, lakini polisi walinifuatilia na kunikamata.”

Mwalongo ameelezea jinsi alivyokamatwa baada ya kuiba pikipiki na kuikimbiza hadi Makambako, ambapo alikamatwa na kisha kupelekwa kituo cha polisi wilayani Ludewa.

Amesema baada ya kufikishwa mahakamani, alikutwa na hatia ya kumiliki pikipiki hiyo kinyume cha sheria, na alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.

“Nashukuru kwa Mungu na kwa msaada wa watu, niliweza kutoka gerezani na sasa naomba kuwa chombo cha mabadiliko kwa vijana, ili waache uhalifu na kumrudia Mungu.”

Mwalongo pia ameelezea jinsi alivyoomba msaada wa kipaza sauti kutoka kwa Jeshi la Polisi, kwani kutokana na matendo mabaya aliyokuwa akiyafanya kwa wananchi lakini bado anaona wana mchango katika kuokoa hai wake hadi leo, kutokana na tabia zisizofaa zilizokuwa zimemtawala.

 “Nilioomba msaada huu kwa Jeshi la Polisi, kwa sababu nilipojikuta mikononi mwa polisi kwa tabia zangu mwenywe hatarishi kabla sijabadilika, nikagundua Mungu ana makusudi na maisha yangu,  kama ilivyokawaida jeshi la polisi kulinda mali na raia wote,” amesema Mwalongo.

Kauli ya polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema alimpokea Shukuru Mwalongo baada ya kumuelezea jinsi alivyohusika katika matukio mbalimbali ya uhalifu, ikiwemo wizi wa pikipiki, jambo lililomsababisha kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Banga amefafanua kuwa Shukuru alikamilisha kifungo chake Februari 2024, lakini akiwa gerezani alipata maono ya Mungu, akamwamini Yesu, na baadaye akaokoka akiwa na lengo la kumtumikia Mungu.

“Alijitokeza kwetu kama Jeshi la Polisi akiomba msaada wa kipaza sauti, ambacho kingemsaidia katika kueneza neno la Mungu na vilevile kusaidia jeshi letu kutoa elimu kwa jamii na kuwasaidia watu waliopo kwenye uhalifu kurudi kwa Mungu,” amesema Kamanda Banga.

Kamanda Banga ameelezea kuwa, kwa kushirikiana na wadau akiwamo Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga, walikubali na kuahidi upatikanaji wa kipaza sauti hicho kilichogharimu Sh350,000.

Amemshukuru Mbunge Kamonga kwa mchango wake, akieleza kuwa kifaa hicho kitasaidia kutoa elimu kwa jamii na kutangaza neno la Mungu.

Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga, alimtaja Kamanda Banga kuwa ni kiongozi mwenye msukumo wa kipekee katika kuhamasisha mabadiliko katika jamii.

“Ninachoamini mimi ni kwamba adhabu kali pekee haitoshi kuwabadilisha wahalifu kuwa watu wema. Lakini, ushauri na saikolojia inapotekelezwa vizuri, inaweza kuwabadilisha wahalifu na kuwa watu wema,” alisema Kamonga, akisisitiza umuhimu wa njia mbadala za kuhamasisha mabadiliko ya tabia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *