Simulizi ya abiria aliyepoteza mguu ajalini

Dodoma. Jasmini Rajabu ambaye ni miongoni mwa majeruhi 49 wa ajali ya basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Dodoma na Kigoma la AN Classic, amesimulia jinsi alivyopoteza mguu wake katika tukio hilo.

Ajali hiyo ambayo hadi kufikia jana jioni watu wanane walikuwa wamepoteza maisha, ilitokea katika eneo la Chigongwe, mkoani Dodoma, saa 4.00 usiku Machi 3,2025.

Akizungumza leo Jumanne Machi 4,2025 wodini katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Jasmini amesema walipoanza safari alilala na aliposhutuka alisikia kelele za abiria wenzake.

Hata hivyo, amesema alipotaka kunyanyuka kutoka alipokuwa alishindwa kwa sababu alikuwa amefika chini.

 “Nilikuwa nishabanwa miguu, halafu nilikuwa nimepakata mtoto mdogo wa mwaka mmoja na miezi saba, mtoto naye akawa ameshafunikwa na kiti, ikanibidi nipambane mwenyewe kwa sababu mashuhuda walikuwa hawajafika kutupa msaada.”

“Ilibidi nipambane kumsaidia mwanangu, ile napambana nikajikuta nimebakia na mguu mmoja, mmoja umebakia kwenye kiti, ikabidi niiname nivutane na mtoto, nikashika miguu na mabega hadi mtoto akatoka. Lakini mtoto alikuwa hoi na kichwa kimetapakaa damu,”amesema.

Amesema watu wanaotoa msaada walipotokea aliwaomba wamsaidie mtoto wake apate huduma mapema kutokana na hali aliyokuwa nayo.

“Mimi mwenyewe nikasema nisharidhika najiona mguu sina, teteeni uhai wa huyu mtoto, wakamchukua Mungu alivyokuwa mkubwa mtoto akawa amevilia tu na damu hakuumia popote,”amesema Jasmini.

Jasmini ambaye alikuwa akitokea Dodoma kwa wifi yake akielekea Kigoma anakofanya kazi mumewe, amesema hakuwa na fahamu baada ya hapo hadi alipokuja kushituka yuko hospitali leo saa 2.00 asubuhi.

Amesema hali yake inaendelea vizuri tofauti na jana baada ya kupata matibabu ya haraka tangu walipofika hospitalini hapo.

Mwanafunzi wa shahada ya sheria mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Oda Bagwanya, amesema migogoro kati ya abiria na kondakta ilianza mapema kabla ya gari kuondoka Dodoma.

Amesema gari walilokuwa wanatakiwa kupanda lilikuwa inatakiwa kuanza safari saa 1.00, lakini wakawa wanazungushwa tu baada ya kuuliza walielezwa kuwa dereva na kondakta wake ni Waislamu hivyo wamekwenda kufuturu.

“Baadaye wanatuambia kuwa gari iko car wash (mahali pa kuoshea magari) lakini baadaye tunaambiwa gari imechanganya dizeli na petroli kwa hiyo kuna lingine inakuja kwa ajili ya kuanza safari. Gari hilo ndio lilikuwa linafika likitokea Kigoma kuja Dodoma.”

“Siti hazikuwa katika ubora, idadi ya abiria ilikuwa kubwa kuzidi uwezo wa siti. Migogoro ikawa mingi. Tunaanza safari ilikuwa ni saa 3.40 usiku imefika saa 4 kama na dakika 19 ama 20 gari ikagonga lori ambalo lilikuwa mbele yetu,”amesema.

Idadi ya waliokufa yaongezeka

Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Stanley Mahundo amesema jana saa 5.00 usiku walipokea majeruhi 55 na vifo vilikuwa ni watu sita vikijumuisha wanawake watatu na waliobaki ni wanaume.

Hata hivyo, amesema leo Machi 4,2025, katika hatua za matibabu waliofariki dunia wameongezeka kufikia wanane ambao ni mwanaume na mwanamke.

“Sababu walikuwa na majeraha makubwa ambayo pamoja na jitihada zote tulizozifanya katika hospitali yetu hatukuweza kuokoa maisha yao.”

 “Lakini hao 24 waliobaki afya zao zinaendelea kuimarika na wanaendelea kupata matibabu,”amesema.

“Tunapozungumza leo jumla ya wagonjwa 25 wamesharuhusiwa kwenda majumbani mwao baada ya kufanyiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Majeraha mengi waliyoyapata yalikuwa ni ya kawaida,”amesema.

Amesema majeruhi wengi wamekatika sehemu ya viungo vyao vya miguu na mikono kutokana na kukandamizwa na gari baada ya kupinduka.

“Kwa jitihada kubwa za Hospitali ya Mkoa wa Dodoma majeruhi wengi tuliwaokoa kwa kuwapa matibabu ya haraka usiku ule hadi kufikia leo asubuhi jumla ya wagonjwa 25 walikuwa wamefanyiwa upasuaji mkubwa,”amesema.

Amesema, “upasuaji huo ni wa kuzuia na kutibu majeraha yaliyokuwa yanatoa damu nyingi. Tunashukuru uwekezaji mkubwa uliofanyika ambao unawezesha watu wanapofika wanapata huduma kwa haraka,”amesema.

Amesema miili minne kati ya minane ambayo ni ya Peter Demeye, Jenipher Tinda, Edither Leonard na Edward John imekabidhiwa kwa ndugu zao baada ya kuitambua.

Amesema waliobakia wanaendelea kuwasiliana na ndugu zao ili waende kuwatambua.

Polisi wazungumza

Awali, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishina Msaidizi Mwandamizi,  Anania  Amo alisema kuwa  ajali hiyo ilitokea Machi 3,2025 saa 4.00 usiku katika eneo hilo.

Alisema ajali hiyo ilitokea wakati basi la kampuni ya AN Classic linalofanya safari zake kutoka Dodoma kupitia Tabora kuelekea Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma kuanguka wakati likitaka kulipita lori la mizigo.

“Lilianza safari kutoka Dodoma kwenda Kigoma na lilipofika maeneo ya Chigongwe wakati analiover take (anataka kulipita) lori moja la mizigo aliligonga na kukosa mwelekeo na kuanguka,”alisema.

Alisema kati ya watu watano waliofariki dunia wanaume watatu na wanawake wawili huku majeruhi wakiwa 49.

Kamanda Amo alisema majeruhi 26 ni wanaume na wanawake 23 na kuwa 48 walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Dodoma huku mmoja akipelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya matibabu zaidi.