
Rais Donald Trump wa Marekani amesema mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine yataanza baada ya kufanya mazungumzo ya simu ya muda mrefu na yenye tija na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Televisheni ya FOX News imeripoti mazungumzo kati ya Trump na Putin yamefanyika jana Jumatano Februari 12,2025, asubuhi kisha kufuatiwa na mazungumzo na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy.
Simu ya Putin kwa Trump ambayo ni mazungumzo ya kwanza yanayojulikana kati ya marais hao tangu Trump alipoingia madarakani mwezi uliopita, imefanyika wakati Trump akieleza wazi kwa washauri wake kuwa anataka kumaliza mgogoro kati ya Urusi na Ukraine, haraka iwezekanavyo.
Maofisa wa Serikali ya Trump walisema walitarajia kubadilishana wafungwa Jumanne kungeweza kuwa ishara nzuri ya juhudi mpya za kumaliza vita hivyo vinavyoingia mwaka wa nne.
Wakati viongozi hao wawili wakifanya tena mawasiliano baada ya ukimya wa muda mrefu kati ya Ikulu ya Washington DC na Kremlin, mpango wa Trump wa kusuluhisha mgogoro huo unaanza kupata sura ya kufanikiwa zaidi.
Katika maelezo ya mazungumzo yao aliyoyachapisha kwenye Mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema:
“Tulijadili kuhusu Ukraine, Mashariki ya Kati, nishati, akili bandia, nguvu ya dola ya Marekani na mada nyingine mbalimbali.”
“Tulikubaliana kushirikiana kwa karibu sana, ikiwa ni pamoja na kutembeleana kati ya mataifa yetu. Pia tumekubaliana timu zetu zitaanza mazungumzo mara moja, na tutaanza kwa kumpigia simu Rais Zelensky wa Ukraine kumfahamisha kuhusu mazungumzo haya, jambo ambalo nitalifanya hivi sasa,” Trump aliandika.
Marekani na Urusi katika maelezo yao ya simu hiyo, viongozi hao walionyesha nia na msimamo wa maridhiano.
“Rais Putin hata alitumia kaulimbiu yangu yenye nguvu sana ya kampeni, ‘Common Sense.’ Sote tunaamini kwa dhati katika hilo,” Trump aliandika, akidokeza rais huyo wa zamani wa Kikosi cha Kijasusi cha Russia (KGB) alikuwa amechagua maneno yake kwa uangalifu ili kumfurahisha kiongozi wa Marekani.
Kwa upande wa Ikulu ya Kremlin ilisema Trump na Putin walizungumza kwa takriban dakika 90.
Kwa wiki kadhaa, Trump alikuwa ameonyesha nia ya kuzungumza na Putin ili kushughulikia mgogoro wa Ukraine.
Wakati maofisa wa Marekani wakisafiri kwenda barani Ulaya wiki hii, tayari wameanza kutoa misimamo ya wazi kuhusu namna vita vya Ukraine vinavyoweza kamalizika.
Akizungumza kwenye kongamano mjini Brussels, nchini Ubelgiji, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth alisema wazo la Ukraine kujiunga na Nato siyo halisi tena, na kwamba Marekani haitotoa kipaumbele tena cha usalama wa Ulaya na Ukraine huku utawala wa Trump ukielekeza juhudi zake katika kulinda mipaka yake na kuzuia vita ya kiuchumi na kijeshi dhidi ya China.
Wakati huohuo, Trump amezungumzia uwezekano wa kufanikisha makubaliano na Zelensky ambapo Ukraine itatoa madini adimu yenye thamani kama malipo kwa msaada wa Marekani.
Trump alizungumza na Zelensky mchana, muda mfupi baada ya mazungumzo yake na Putin.
Awali, Rais Joe Biden wa Marekani ambaye ni mtangulizi wa Trump hakuwahi kuzungumza na Rais Putin juu ya hatima ya kufikia makubaliano ya kumaliza vita hiyo akiamini kuwa hakukuwa na faida yoyote kuzungumza na kiongozi aliyemtaja kuwa mhalifu wa kivita.
Rais wa mwisho wa Marekani kutembelea Urusi alikuwa, Barack Obama aliyetembelea taifa hilo mwaka 2013. Obama alitembelea nchi hiyo alipohudhuria mkutano wa G20. Wakati huo, Putin naye alihudhuria mazungumzo ya Umoja wa Mataifa Marekani mwaka 2015.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.