Simon Msuva atia neno usajili wa Gomes

WINGA wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Al Talaba ya Iraq, Saimon Msuva amezungumzia usajili wa mshambuliaji wa Singida Black Stars aliyekuwa akicheza kwa mkopo Fountain Gate, Seleman Mwalimu ‘Gomes’ kwenda Wydad Casablanca ya Morocco chini ya Rulani Mokwena amesema mara atakapopenya kikosini basi atacheza sana.

Msuva ambaye ameshawahi kupita Wydad amefunguka hayo siku chache baada ya Singida BS kumuuza Gomes nchini humo kwa mkataba wa miaka minne na nusu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema amepokea kwa furaha taarifa za Gomes kutua Morocco na anaamini ameenda wakati sahihi, huku akimuasa kuachana na mambo ya nje ya uwanja na kumtaka azingatie zaidi kazi iliyompeleka huko.

“Gomes ni mchezaji mzuri bado ni kijana ukiangalia kocha aliyepo anapenda wachezaji wenye uharaka kama ilivyo kwake namwamini akipata nafasi atafanya kitu sahihi, pia anatakiwa kupambana kwa sababu ameenda timu kubwa ambayo inashiriki michuano mikubwa, juhudi binafsi zitamjenga.”

“Namtakia kila la kheri Wydad ni timu nzuri itampa mafanikio ambayo yatakuwa chachu pia kwake na timu ya taifa, mimi nimepita hapo nikafungua milango wengine wakaja naamini yeye pia atafanya hivyo, imani yangu kwake atafanya vitu vikubwa.’’

Msuva alisema Wydad ni timu kubwa Afrika na kila mmoja anafahamu mapambano yake na bila kuangalia nini kinafanyika nje ya uwanja, ndiyo siri kubwa ya kufanikisha mipango na namna ambavyo ataweza kufungua njia kwa nyota wengine wa kitanzania kupata nafasi ya kucheza huko.

Nyota huyo mwenye mabao sita ya Ligi Kuu Bara akipitwa mabao mawili kinara wa upachikaji mabao Elvis Rupia wa Singida Black Stars aliyefunga manane, amesajiliwa na Wydad kwa ada ya uhamisho ya Sh891 milion huku mshahara wake kwa mwezi ukiwa ni Sh6 milioni, pia kutakuwa na bonasi ya kupata kiasi cha fedha kwa kila goli atakalofunga.

Mshambuliaji huyo kinda ambaye ana miaka 19 kwa mujibu wa taarifa zilizolipotiwa na mitandao mbalimbali ya Morocco amesajiliwa na timu hiyo kwenye kikosi cha timu ya vijana lakini anaweza kutumika timu ya kikosi cha kwanza.