
MABAO mawili aliyofunga mshambuliaji wa Geita Gold, Andrew Simchimba katika ushindi wa timu hiyo wa 3-0, dhidi ya Mbeya Kwanza Jumatatu ya Machi 17, yamemfanya kufikisha 15, ikiwa ni idadi sawa na ya kinara Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar.
Wengine ni Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ wa TMA aliyefunga mabao 13, Naku James (Mbuni FC) mwenye 11, huku Yusuph Mhilu wa Geita Gold, Boniphace Maganga (Mbeya Kwanza) na William Thobias anayeichezea Mbeya City wakifunga manane kila mmoja wao.
Simchimba aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwamo za Azam FC, Singida Black Stars ambayo zamani Ihefu na Coastal Union, alisema licha ya kasi yake katika kufunga ila kipaumbele cha kwanza ni kukirejesha kikosi hicho katika Ligi Kuu.
“Mwenendo wetu ni mzuri na nafasi tuliyopo inaridhisha ingawa tunahitaji sana kupambana kwa sababu hata washindani wetu wanaonyesha upinzani ambao kama tusipokuwa makini tunaweza kutoka nje ya malengo yetu tuliyojiwekea msimu huu,” alisema.
Nyota huyo alisema moja ya malengo yao makubwa ni kushika nafasi ya kwanza na kupanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja.