Simbu mzigoni Boston Marathon leo

Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu amesema amejiandaa vyema kushinda mbio za Boston Marathon zitakazofanyika leo Jumatatu jijini Boston, Marekani.

Mbio hizo zitaanza ya saa 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki ambapo Simbu ana medali kadhaa ikiwemo ya shaba ya mashindano ya dunia ambayo yalifanyika London, Uingereza, 2017 pamoja na ya fedha ya Jumuiya ya Madola ambayo alipata 20222 Birmigham Uingereza.

Simbu pia aliwahi kuingia nane bora ya marathoni za Olimpiki mara mbili mfululizo 2016 akishika nafasi ya tano huko Rio De jeneiro, Brazil kwa kutumia saa 2:11:15 na mwaka 2020 jijni Tokyo, Japan akimaliza wa saba kwa saa 2:11:35.

Nyota huyo atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wababe tisa wa riadha duniani akiwemo Sisay Lema wa  Ethiopian ambaye anatetea medali ya dhahabu aliyoshinda katika mbio za mwaka jana akitumia muda wa saa 2:06:17.

Pia akitambia rekodi binafsi ya kutumia muda wa saa 2:01:48 katika mbio za Valencia Marathon 2023 ambayo ilimfanya ashike nafasi ya nne katika chati ya wanariadha waliotumia muda mfupi zaidi kumaliza mbio ndefu.

Mwamba mwingine ambaye anatazamiwa kumtoa jasho ni mshindi mara mbili wa mbio hizo, Mkenya Evance Chebet ambaye mwaka jana alimaliza wa tatu pamoja na mshindi wa mbio za Chicago Marathon, John Korir.

Nyota huyo kutoka timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), mwenye cheo cha sajenti atakutana pia na kigingi cha bingwa wa dunia 2024, Mkenya Victor Kiplangat pamoja na washindi namba mbili na tatu mbio za Berlin Marathon 2024, Mkenya Cybrian Kotut na Muethiopia Haymanot Alew.

Simbu ambaye kwa sasa yupo katika mtazamo mzuri wa ukimbiaji akitambia muda mzuri wa saa 2:04:38 ambao aliupata katika mbio za Valencia Marathon mwaka jana, amesema kutokana na maandalizi ambayo amefanya anaamini leo atalipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa  kuongoza na kuwashinda wababe wa mbio hizo kwa dunia.

“Natambua kutakuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanariadha wengine ndio maana nimefanya maandalizi ya kutosha ambayo yatanifanya kushinda,” amesema Simbu.

Ameongeza kuwa kutokana na uzoefu alionao katika mbio ndefu za dunia ambazo ameshiriki, hana shaka hata kidogo kuhusu uwezo wake wa kufanya kweli na kutimiza malengo yake ambayo ni kushinda.

Kocha wa timu ya JWTZ, Antony Mwingereza amesema matumaini kwa Simbu kufanya vizuri leo ni makubwa kutokana na maandalizi ambayo walifanya, lakini pia mazingira ambayo nyota huyo anayo kwa sasa.

“Sina wasiwasi hata kidogo na uwezo wa Simbu. Tulifanya maandalizi ya kutosha kikubwa tu Watanzania wamuombee afanye kweli,” amesema Mwingereza.

Kapteni Christopher Masanga ambaye ni meneja wa timu ya riadha ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, amemtaka mwanariadha huyo kuongeza jitihada ambazo zitamfanya kufanikisha malengo ambayo ni kushinda Boston Marathon.

Mshindi wa kwanza wa mbio za Boston Marathon atavuna kitita cha Dola 150,000; wa pili Dola 75,000 wa tatu 40,000 huku wanne akivuna Dola 25,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *