
Dar es Salaam. Simba imeanza michuano ya Kombe la Shirikisho kibabe kwa kuifumua Kilimanjaro Wonders kwa mabao 6-0, huku ikiandika rekodi mbili katika hatua ya 64 Bora kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa Simba kwenye kombe hilo msimu huu, lakini ukiwa pia wa kwanza wa wachezaji wengi wa kikosi hicho ambao walisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu.
Rekodi ya kwanza iliyowekwa na timu hiyo ni kufunga bao la mapema likiwekwa sekunde 18 baada ya filimbi ya kwanza ya kuanzisha mchezo, kisha kufunga mabao 6-0, ikiwa ni idadi kubwa ya mabao katika hatua hiyo msimu huu ikikamilisha timu ya 32 iliyotinga hatua inayofuata ikizifuata Yanga na Azam zilizotangulia.
Katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja, Simba ilionyesha mapema kuwa na uchu wa ushindi kuanzia dakika ya kwanza ilipofunga bao kupitia kwa Valentino Mashaka kabla ya kuongeza mengine na kufanya iende mapumziko ikiwa mbele ya mabao 4-0.
Mashaka aliandika rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi katika hatua hiyo kwa msimu huu akitengenezewa krosi safi na beki wa kushoto Valentin Nouma kabla ya mvua ya mabao kuendelea kumiminika kwenye lango la Kilimanjaro ambayo ilionekana kuwa na kikosi cha vijana wadogo.
Kiungo mshambuliaji wa Simba Ladack Chasambi alifunga bao la pili dakika ya tatu akimalizia krosi ya beki wa kulia David Kameta ‘Duchu’ baada ya kugongeana vizuri kwenye shambulizi la bao hilo kabla ya dakika sita baadaye beki wa Wonders, Patrick Sebastian kujifunga wakati akiokoa shuti la Nouma kabla ya Joshua Mutale kuandika bao la nne dakika ya 21.
Kipindi cha pili Simba bado ikaendelea kuliandama lango la Kilimanjaro ikipata bao la tano kupitia kwa mshambuliaji Steven Mukwala kwa kichwa akimalizia krosi ya Duchu kabla ya Edwin Balua kupiga la sita.
Duchu kama Mwenda
Jana beki mpya wa Yanga ambaye ni beki wa zamani wa Simba Israel Mwenda alianza kwa mara ya kwanza na kutengeneza mabao mawili na jana Duchu naye alimlipa akitengeneza mabao mawili kwa timu yake ukiwa ni mchezo wake wa kwanza anacheza msimu huu.
Zilizofuzu
Simba sasa imeungana na vigogo Yanga, Azam na nyingine zilizokamilisha idadi ya timu 32, zikiwamo Mbeya City, Green Warriors, TMA Stars,JKT TZ, Cosmopolitan, Polisi TZ, Towns Stars, Stand United,
KenGold, Namungo, Transit Camp, Biashara United, Mtibwa Sugar, Songea United na Singida BS.
Nyingine ni; Mashujaa, Fountain Gate, Coastal Union, Leo Tena, Pamba Jiji, KMC, Geita Gold, Giraffe Academy, Mbeya Kwanza, Kiluvya FC, TZ Prisons, Kagera Sugar, Bigman FC na Tabora Utd.