
Simba haitanii. Ikiwa imeshatinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, mabosi wa klabu hiyo hawajalala kwani wameanza kusaka mastaa wa msimu ujao kwa kumvutia waya kiungo raia wa Guinea, Balla Moussa Conte.
Conte ni yule kiungo wa CS Sfaxien ya Tunisia aliyekichafua pale kati katika mchezo wa ugenini wa Kombe la Shirikisho, wakati Simba ikishinda bao 1-0 mbele ya wenyeji.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Simba Fadlu Davids akamtuma kipa Moussa Camara kwenda kuchukua mawasiliano ya raia mwenzake huyo na kweli buana wamempigia simu ili kuanza mipango ya kumshusha Msimbazi.
Conte amelifichulia Mwananchi kuwa, bosi mmoja wa juu wa Simba amempigia simu akiulizia juu ya mkataba wake na utayari wake wa kuja kujiunga na timu hiyo.
Hata hivyo, kiungo huyo alisema hatua hiyo haitakuwa kwa msimu huu unaoendelea na kwamba mazungumzo yao yataendelea na dili hilo ni kwa ajili ya msimu ujao.
“Ni kweli Simba wamenipigia lakini haitakuwa kuja huko sasa labda msimu ujao, bado hatujamalizia mazungumzo, ukiwatafuta wao watakueleza zaidi,” alifichua Conte, huku taarifa kutoka ndani ya Simba ni kwamba Fadlu amesisitiza kuendelea kufuatiliwa kwa kiungo huyo endapo kiwango chake kitaendelea kama sasa kwani anamhitaji katika kikosi kijacho.
Bosi mmoja wa Simba ameliambia mwananchi, Fadlu ana hesabu kali akitaka kuendelea kukisuka kikosi chake likiwemo eneo la kiungo.
“Kocha anamtaka sana huyo Conte, tunaendelea na mawasiliano naye lakini tutaona tutafikia wapi kwa kuwa bado ana mkataba na klabu yake,” alisema bosi huyo.
“Huyu ni chaguo la kocha (Fadlu) unajua hii ni awamu ya pili tu tumefanya lakini kwenye awamu ya tatu sasa ndio mtaona watu kama hawa kina Conte wanashuka.”